Sira 39

Sira 39

1Lakini anayepania kujifunza sheria ya Mungu Mkuu,

hutafuta hekima ya watu wa kale,

na kushughulikia waliyosema manabii.

2Huyahifadhi mazungumzo ya watu mashuhuri,

na kupambanua magumu ya mifano.

3Hutafuta maana zilizofichika za methali,

na methali za kutatiza kwake si kitu.

4Huyo huwatumikia wakuu,

na huonekana mbele ya watawala;

husafiri nchi za kigeni

na amepata kujua wema na ubaya wa watu.

5Asubuhi huamka kwa moyo na bidii

na kutafuta kumwomba Bwana aliyemuumba;

humwekea Mungu Mkuu maombi yake,

hufungua kinywa kusali,

na kuomba msamaha kwa dhambi zake.

6Kama Bwana aliye mkuu anataka

atamjaza mtu huyo busara,

naye atabubujika maneno ya hekima

na kumshukuru Bwana katika sala.

7Ataelekeza mashauri na maarifa yake vizuri,

na kutafakari juu ya siri zake Bwana.

8Ataonesha maarifa yake aliyojifunza,

na kuionea fahari sheria ya agano la Bwana.

9Watu wengi watasifu maarifa yake,

nayo hayatasahaulika kamwe.

Kumbukumbu lake halitatoweka,

na jina lake litakumbukwa vizazi vyote.

10Mataifa yatatangaza hekima yake,

nayo jumuiya ya watu itasema sifa zake.

11Ataishi maisha marefu ataacha jina maarufu kuliko wengi;

na akifariki, kwake itakuwa imetosha.

Wimbo wa kumsifu Mungu

12Bado nina ya kusema niliyoyafikiria,

nami nimejaa kama mwezi mpevu.

13Nisikilizeni enyi watoto wema,

mkachanue kama waridi lililopandwa kando ya kijito.

14Toeni harufu nzuri kama ya ubani,

na kuchanua maua kama yungiyungi.

Tawanyeni angani harufu yenu na kuimba wimbo wa sifa;

msifuni Bwana kwa ajili ya matendo yake yote.

15Tangazeni ukuu wa jina lake,

mshukuruni kwa nyimbo za sifa,

mwimbieni kwa vinywa vyenu na vinubi.

Mnapomshukuru mwimbieni hivi:

16“Vitu vyote vimeumbwa na Bwana,

maana vyote ni vizuri sana.

Kila anachoamuru kitafanyika wakati wake.”

17Usiulize “Hiki ni kitu gani?” au, “Kwa nini hiki?”

Maana tutajifunza vyote wakati wake Bwana.

Kwa neno lake maji huacha kutiririka yakajirundika

kwa tamko la kinywa chake maji yalikaa ghalani mwake.

18Kwa amri yake kila anachopenda hufanyika,

hakuna awezaye kupunguza uwezo wake wa kuokoa.

19Matendo ya viumbe vyote ni wazi mbele yake,

hakuna kiwezacho kujificha mbele yake.

20Yeye huona tangu milele hata milele,

na hakuna kitu cha ajabu kwake.

21Usiulize “Hiki ni kitu gani?” au, “Kwa nini hiki?”

maana kila kitu kimeumbwa kwa matumizi yake.

22Baraka zake huijaza nchi kavu kama kwa mto,

huzilowanisha kama kwa mafuriko.

23Ghadhabu yake itayafukuza mataifa,

kama ageuzavyo maji mazuri kuwa ya chumvi.

24Kwa wanaomcha njia zake zimenyoka,

hali kwa waovu njia zake zina vikwazo.

25Tangu mwanzoni Mwenyezi-Mungu aliumba vitu vyema kwa ajili ya walio wema,

lakini kwa watu wabaya aliumba vitu vibaya na vyema.

26Mahitaji ya msingi kwa maisha ya mtu

ni maji, moto, chuma na chumvi;

unga, maziwa, asali, divai, mafuta na mavazi.

27Hivi vyote ni vizuri kwa wamchao Mungu,

lakini hugeuka kuwa maovu kwa wenye dhambi.

28Kuna pepo zilizoumbwa kuwaadhibu watu,

nazo zikikasirika zinaadhibu vikali.

Wakati wa hukumu zitaonesha nguvu yake,

na hivyo kuituliza hasira ya Muumba wao.

29Moto, mvua ya mawe, njaa na maradhi;

hivi vyote vimeumbwa kuwaadhibu watu.

30Meno ya wanyama wakali, nge na nyoka

na upanga unaowaadhibu wasiomcha Mungu kwa maangamizi.

31Vyote vitafurahi kutekeleza amri za Bwana;

vitakuwa tayari duniani kumhudumia,

na wakati utakapowadia havitaiasi amri yake.

32Kwa hiyo nimekuwa na hakika ya hayo tangu mwanzo;

nimeyawaza na kuwazua, nikayaandika.

33Kazi zote za Bwana ni njema,

naye huwapatia watu mahitaji yao yote wakati wake.

34Usiseme: “Kitu hiki ni kibaya kuliko kile,”

maana faida ya kila kitu itaonekena wakati wake.

35Sasa basi, imba sifa kwa moyo wote,

na kulisifu jina la Bwana.

Swahili Common Language DC Bible: Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki © Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya, 1995, 2001. Haki zote zimehifadhiwa.  
Published by: Bible Society of Tanzania