Sira 42

Sira 42

Kuona fahari

1Haya ndiyo mambo ambayo hutaona haya kutenda,

wala usitende dhambi kwa kuogopa watu watasema nini:

2Usione haya kufuata sheria ya Mungu Mkuu na agano lake,

usione haya kutoa uamuzi wa haki kuwahukumu wenye hatia.

3Usione haya kuwajibika na mwenzako wa kazi na msafiri,

na kugawana urithi na rafiki.

4Usione haya kutumia mizani na vipimo halali,

5kujipatia faida kwa wafanyabiashara,

kuwafunza watoto nidhamu ya hali ya juu,

kumchapa vikali mtumishi mwovu.

6Kama mkeo haaminiki, mfiche mambo yako,

na penye watu wengi fungia vitu vyako ndani.

7Chochote unachotoa, ujue idadi na kipimo chake,

weka katika maandishi mapato na matumizi.

8Usione haya kumfunza mjinga na mpumbavu

au mzee agombanaye na vijana.

Hivyo utakuwa kweli umeelimishwa,

nawe utapata kibali mbele ya watu wote.

9Baba mwenye binti hukesha kwa siri kwa ajili yake;

wasiwasi wa baba juu ya binti humzuia kulala.

10Akiwa bado msichana baba yake anaogopa ataharibiwa,

au atapata mimba akiwa bado nyumbani kwake;

au akiwa ameolewa baba yake anaogopa kwamba anaweza kuwa tasa.

11Mchunge sana binti aliye mtundu,

la sivyo atakufanya uchekwe na maadui zako,

ukawa kioja mjini na mwenye jina baya kwa watu,

ukaaibishwa naye mbele ya umati wa watu.

Wanawake

12Usikodolee macho uzuri wa mtu yeyote,

wala kukaa kuzungumza na wanawake.

13Maana nondo hutoka katika mavazi,

na ubaya wa mwanamke hutoka kwa mwanamke.

14Afadhali uovu wa mwanamume kuliko wema wa mwanamke;

mwanamke ndiye asababishaye aibu na fedheha.

Utukufu wa Mungu ulimwenguni

15Sasa, nitawakumbusha kazi za Bwana,

na kutangaza yale niliyoyaona:

Kazi za Bwana hufanyika kwa neno lake.

16Jua hutazama kila kitu chini kwa miali yake,

kazi ya Bwana imejaa utukufu wake.

17Hakuna hata mmoja wa malaika wake Bwana

awezaye kutaja matendo yake yote ya ajabu

ambayo Bwana Mwenyezi-Mungu ameyaimarisha.

ili ulimwengu uwe imara katika utukufu wake.

18Yeye huchunguza vilindi na mioyo ya watu,

na kuiona mipango yao ya hila.

Maana Mungu Mkuu anajua elimu yote ile,

na anazijua ishara za nyakati.

19Yeye hutangaza yaliyotukia na yajayo,

na kufunua chochote kilichofichika.

20Hakuna wazo linaloweza kumponyoka,

hakuna hata neno moja liwezalo kujificha mbali naye.

21Yeye amepanga fahari za hekima yake.

Yeye ndiye peke yake aliye tangu milele hata milele.

Hawezi kuongezewa kitu au kupokonywa kitu;

wala hahitaji mtu yeyote kuwa mshauri wake.

22Jinsi gani zipendezavyo kazi zake!

Jinsi gani zingaavyo kuziona!

23Vitu hivyo vyote vipo na vyadumu milele,

na kila vinapohitajiwa humtii kila mara.

24Viumbe vyote vimepangwa viwiliviwili

kila kimoja kikiwa kinyume cha kingine;

na hakuna alichofanya kisicho kamili.

25Kitu kimoja huukamilisha uzuri wa kingine.

Nani anaweza kuchoka kuangalia utukufu wake?

Swahili Common Language DC Bible: Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki © Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya, 1995, 2001. Haki zote zimehifadhiwa.  
Published by: Bible Society of Tanzania