The chat will start when you send the first message.
1Ikawa, Dawidi alipokaa nyumbani mwake, Dawidi akamwambia mfumbuaji Natani: Tazama, mimi ninakaa katika nyumba iliyojengwa kwa miangati, lakini Sanduku la Agano la Bwana linakaa chini ya mapazia tu.
2Natani akamwambia Dawidi: Yote yaliyomo moyoni mwako yafanye! Kwani Mungu yuko pamoja na wewe.
3Lakini usiku uleule neno la Mungu likamjia Natani kwamba:
4Nenda, umwambie mtumishi wangu Dawidi: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Wewe hutanijengea nyumba ya kukaa.
5Kwani sikukaa nyumbani tangu siku ile, nilipowaleta Waisiraeli huku milimani, mpaka siku hii ya leo, ila nilikuwa hemani huku, tena hamani huko, Kao langu likawa huku na huko.
6Je? Hapo pote, nilipokwenda pamoja na Waisiraeli wote, nilimwambia hata mmoja wao waamuzi wa Waisiraeli, niliowaagiza kuwachunga walio ukoo wangu, na kumwuliza neno la kwamba: Mbona hamnijengei nyumba ya miangati?
7kwa hiyo umwambie sasa mtumishi wangu Dawidi: Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Mimi nilikuchukua malishoni, ulipowafuata kondoo, uwe nwenye kuwatawala walio ukoo wangu wa Waisiraeli.
8Nikawa pamoja na wewe po pote, ulipokwenda, nikawaangamiza adui zako wote mbele yako; nitakupatia jina lililo sawa na majina ya wakubwa walioko huku nchini.
9Nao walio ukoo wangu wa Waisiraeli nitawapatia mahali, nitakapowapanda, wapate kukaa hapo pasipo kuhangaika tena, wala watu waovu wasiwakorofishe tena kama huko kwanza
10tangu siku zile nilipowaagiza waamuzi, wawatawale walio ukoo wangu wa Waisiraeli; nitawanyenyekeza adui zako wote, tena ninakuambia sasa: Bwana atakujengea nyumba.
11Itakuwa hapo, siku zako zitakapotimia, uende kulala pamoja na baba zako; ndipo, nitakapoinua nyuma yako mzao wako atakayetoka kwa wanao, niusimike ufalme wake.
12Yeye ndiye atakayenijengea nyumba, nami nitakisimamisha kiti chake cha kifalme, kipate kuwapo kale na kale.[#1 Mambo 22:10; 28:6.]
13Mimi nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu, nao upole wangu sitauondoa kwake, kama nilivyouondoa kwao waliokuwa mbele yako.
14Nitamsimamisha, awe nyumbani mwangu namo katika ufalme wangu kale na kale, nacho kiti chake cha kifalme kitakuwa kimesimamishwa kale na kale.
15Natani akamwambia Dawidi haya maneno yote sawasawa, kama alivyoyaona yote alipoyachunguza.
16Kisha mfalme Dawidi akaingia pake Bwana, akakaa hapo akisema: Bwana Mungu, mimi ni nani? Nao mlango wangu ni nini ukinileta, nifike hapa?[#1 Mose 32:10.]
17Lakini haya yakawa madogo machoni pako, Mungu, kwa hiyo umeyasema yatakayoujia mlango wa mtumishi wako katika siku zilizo mbali bado, ukanitazama kimtu na kunikweza, Bwana Mungu.
18Dawidi akuambie nini tena kwa hivyo, unavyomheshimu mtumishi wako? Wewe unamjua mtumishi wako.
19Bwana, kwa ajili ya mtumishi wako na kwa mapenzi ya moyo wako umeyafanya haya makubwa yote, uyajulishe haya matendo makubwa yote.
20Bwana, hakuna anayefanana na wewe, hakuna Mungu, asipokuwa wewe, kwa hayo yote, tuliyoyasikia kwa masikio yetu.
21Tena liko taifa moja tu huku nchini linalofanana na ukoo wako wa Waisiraeli? Hao ndio, Mungu aliokwenda kuwakomboa, wawe ukoo wake. Hapo ulijipatia Jina kwa matendo makubwa yaliyoogopesha, ulipowafukuza wamizimu mbele yao walio ukoo wako, uliowakomboa na kuwatoa Misri.
22Ukaupa ukoo wako wa Waisiraeli kuwa ukoo wako kale na kale, wewe Bwana ukawa Mungu wao.
23Sasa Bwana, neno hili, ulilolisema la mtumishi wako na la mlango wake, liwe limeshupaa kale na kale, ukifanya, kama ulivyosema.
24Ndivyo, Jina lako litakavyokuwa limeshupaa kwa kuwa kubwa kale na kale kwamba: Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, ni Mungu wa Isiraeli kweli, tena ndivyo, mlango wa mtumishi wako Dawidi utakavyokuwa wenye nguvu mbele yako.
25Kwani wewe, Mungu wangu, umelifunua sikio la mtumishi wako, asikie, ya kuwa utamjengea nyumba, kwa hiyo mtumishi wako ameiona njia hii ya kukutolea maombo haya.
26Sasa Bwana, wewe ndiwe Mungu; hayo mema, uliyomwambia mtumishi wako, na yapate kuwa. Sasa na ikupendeze kuubariki mlango wa mtumishi wako, uwepo kale na kale usoni pako! Kwani unayoyabariki wewe, Bwana, huwa yamebarikiwa kale na kale.