1 Wafalme 13

1 Wafalme 13

Yeroboamu anaonywa na mfumbuaji.

1Mara akatokea mtu wa Mungu. Naye alitoka Yuda kuja Beteli kwa kuagizwa na Bwana. Akatokea papo hapo, Yeroboamu aliposimama penye meza ya kutambikia, avukize.

2Kwa kuagizwa na Bwana akapaza sauti kwa ajili ya hiyo meza ya kutambikia, akasema: Meza ya kutambikia! Meza ya kutambikia! Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Tazama! Nyumbani mwa Dawidi atazaliwa mwana, jina lake Yosia; yeye atachinja juu yako kuwa ng'ombe za tambiko watambikaji wa vijumba vya vilimani wanaovukiza juu yako; ndipo, watakapoteketeza juu yako mifupa ya watu.[#2 Fal. 23:16.]

3Siku hiyohiyo akawapa hata kielekezo akisema: Hiki ndicho kielekezo, Bwana alichokisema: Mtaona meza hii ya kutambikia ikipasuka, majivu ya mafuta yaliyoko juu yake yamwagike.

4Mfalme alipolisikia neno hili la yule mtu wa Mungu, alilolisema na kupaza sauti kwa ajili ya meza ya kutambikia ya Beteli, Yeroboamu akaunyosha mkono wake akisimama penye ile meza ya kutambikia, akasema: Mkamateni! Ndipo, mkono wake, aliomnyoshea, ulipokauka, asiweze kuurudisha kwake.

5Nayo meza ya kutambikia ikapasuka, nayo majivu ya mafuta yaliyokuwa juu yake yakamwagika hapo mezani pa kutambikia; ndicho kielekezo, yule mtu wa Mungu alichowapa kwa kuagizwa na Bwana.

6Mfalme akaomba na kumwambia yule mtu wa Mungu: Mlalamikie Bwana Mungu wako usoni pake na kuniombea, mkono wangu upate kurudi kwangu! Yule mtu wa Mungu alipomlalamikia Bwana usoni pake, ndipo, mkono wa mfalme uliporudi kwake, ukawa, kama ulivyokuwa kwanza.[#2 Mose 8:8,12.]

7Mfalme akamwambia yule mtu wa Mungu: Njoo, twende pamoja nyumbani, upate kutulia kidogo, nami nikupe tunzo.

8Yule mtu wa Mungu akamwambia mfalme: Ijapo, unipe nusu ya nyumba yako, sitakwenda na wewe, wala sitakula mkate, wala sitakunywa maji mahali hapa.[#4 Mose 22:18.]

9Kwani ndivyo, nilivyoagizwa na neno la Bwana kwamba: Usile huko mkate, wala usinywe maji, wala usiirudie njia ile, uliyokwenda nayo!

10Akaenda zake na kushika njia nyingine, hakuirudia njia ile, aliyokuja nayo alipokwenda Beteli.

Yule mfumbuaji anaponzwa, afe.

11Huko Beteli alikaa mfumbuaji mzee; wanawe huyu wakaja, wakamsimulia matendo yote, yule mtu wa Mungu aliyoyatenda Beteli siku hiyo, nayo maneno, aliyomwambia mfalme. Walipokwisha kumsimulia haya baba yao,

12baba yao akawauliza: Amekwenda na kushika njia gani? Wanawe walipomwonyesha njia, yule mtu wa Mungu aliyetoka Yuda aliyoishika,

13akawaambia wanawe: Nitandikieni punda! Walipkwisha kumtandikia punda, akampanda,

14akamfuata yule mtu wa Mungu, akamkuta, akikaa chini ya mkwaju, akamwuliza: Kumbe wewe ndiwe mtu wa Mungu aliyetoka Yuda? Akamwambia: Ni mimi.

15Akamwambia: Nifuate kwenda nyumbani, ule chakula!

16Akamjibu: Siwezi kurudi na wewe wala kuingia mwako; sitakula chakula kwako, wala sitakunywa maji mahali hapa,

17kwani nimeambiwa na neno la Bwana: Usile huko chakula, wala usinywe maji huko, wala usirudi na kuishika njia ile, uliyokuja nayo![#1 Fal. 13:9.]

18Ndipo, yule alipomwambia: Mimi mami ni mfumbuaji kama wewe; nami malaika ameniambia kwa kuagizwa na Bwana kwamba: Umrudishe kwako nyumbani, ale chakula, anywe maji! Lakini huko alimwongopea.

19Akarudi naye, akala chakula nyumbani mwake, akanywa maji.

20Ikawa, wao walipokaa mezani, ndipo, neno la Bwana lilipomjia yule mfumbuaji aliyemrudisha,

21akamwambia yule mtu wa Mungu aliyetoka Yuda na kupaza sauti akisema: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Kwa kuwa hukukitii kinywa cha Bwana, usiliangalie agizo, Bwana Mungu wako alilokuagiza,

22ukarudi, ukala chakula, ukanywa maji mahali hapo, alipokuambia: usile chakula, wala usinywe maji hapo! basi, kwa hiyo maiti yako haitaingia kaburini kwa baba zako.

23Alipokwisha kula chakula na kunywa maji, yule akamtandikia punda huyu mfumbuaji, aliyemrudisha.

24Alipokwenda zake, simba akamwona njiani, akamwua, nayo maiti yake ikalala njiani hivyo, ilivyoangushwa, naye punda akasimama kando yake, hata simba akasimama kando ya maiti.[#1 Fal. 20:36.]

25Mara watu waliopita wakaiona maiti, ilivyolala njiani, naye simba aliyesimama kando yake maiti, wakaja, wakayasimulia mle mjini, yule mfumbuaji mzee alimokaa.

26Yule mfumbuaji aliyemrudisha njiani alipoyasikia akasema: Huyu ni yule mtu wa Mungu asiyekitii kinywa cha Bwana; kwa hiyo Bwana amemtolea simba, amwue na kumvunjavunja kwa neno la Bwana, alilomwambia.

27Kisha akawaambia wanawe kwamba: Nitandikieni punda! Wakamtandikia.

28Alipokwenda, akaiona ile maiti, ilivyolala njiani, punda na simba wakisimama kando ya maiti; yule simba hakuila hiyo maiti, wala hakumrarua punda.

29Mfumbuaji akaichukua maiti ya yule mtu wa Mungu, akaiweka juu ya punda, akairudisha, aje nayo mjini mwake mfumbuaji mzee, amwombolezee, kisha amzike.

30Alipokwisha kuilaza maiti kaburini kwake, wakaiombolezea kwamba: A, ndugu yangu![#Yer. 22:18.]

31Alipokwisha kumzika, akawaambia wanawe kwamba: Nitakapokufa, sharti mnizike humu kaburini, yule mtu wa Mungu alimozikwa, mifupa yangu mwilaze kando ya mifupa yake.

32Kwani litatimia kweli lile neno, alilolisema na kupaza sauti kwa kuagizwa na Bwana kwa ajili ya meza ya kutambikia iliyoko Beteli na kwa ajili ya vijumba vyote vya kutambikia vilivyoko vilimani juu katika miji ya Samaria.

33Lakini hayo yalipofanyika, Yeroboamu hakurudi na kuiacha njia yake mbaya, akaweka tena watu wo wote kuwa watambikaji wa vilimani; aliyependezwa naye akamjaza gao, awe mtambikaji wa vilimani.[#1 Fal. 12:31; 2 Mose 28:41.]

34Neno hilo ndilo lilioukosesha mlango wa Yeroboamu, likauangamiza na kuutowesha huku nchini.[#1 Fal. 12:30.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania