The chat will start when you send the first message.
1Mche utamea shinani mwa Isai,
kijiti kilichotoka mizizini mwake kitazaa matunda;
2nayo Roho ya Bwana itamkalia:
ni roho yenye werevu wa kweli na utambuzi,
ni roho yenye mizungu na uwezo,
ni roho ya kumjua Bwana nayo ya kumcha.
3Naye atapendezwa na kumcha Bwana,
hataamua kwa hayo, macho yake yatakayoyaona,
wala hatakata mashauri kwa hayo,
masikio yake yatakayoyasikia.
4Atawaamulia wanyonge kwa wongofu,
nao wakiwa atawakatia mashauri yanyokayo,
nazo nchi atazipiga kwa fimbo ya kinywa chake,
nao wasiomcha Mungu atawaua kwa pumzi itokayo midomoni mwake.
5Wongofu utakuwa mkanda wake wa kujifunga,
nao welekevu utakuwa mshipi wa kiunoni pake.
6Hapo mbwa wa mwitu watafikia kwenye wana wa kondoo,
nao chui watalala pamoja na wana wa mbuzi,
hata ndama na simba na ng'ombe mnono watalisha pamoja,
wakichungwa na mtoto mdogo.
7Ng'ombe na kukuu watakula pamoja,
nao watoto wao watalala pamoja,
nao simba watakula majani makavu.
8Watoto wachanga watacheza penye mashimo ya pili,
nao watoto walioacha maziwa ya mama
watapeleka vidole vyao machoni kwa nyoka za moto.
9Hawatafanya mabaya wala mapotovu
katika milima yangu yote mitakatifu;
kwani nchi zitajaa watu wamjuao Bwana,
kama maji yanavyofurika baharini.
10Siku ile ndipo, wamizimu watakapolitafuta shina la Isai,
maana litakuwa bendera, makabila ya watu yakayotwekewa,
nayo makao yake yatakuwa yenye utukufu.
11Siku ile itakuwa mara ya pili, Bwana akiukunjua mkono wake, awakomboe waliosalia kwao walio ukoo wake, awatoe katika nchi zilizo za Asuri na za Misri za chini na za juu na za Nubi na za Elamu na za Sinari na za Hamati nako kwenye visiwa vilivyoko baharini.
12Hivyo atawatwekea wamizimu bendera,
awakusanye Waisiraeli waliotawanyika,
awaokote nao wanawake wa Kiyuda waliopotea,
atawakusanya na kuwatoa pande zote nne za nchi.
13Hapo ndipo, wivu wa Waefuraimu utakapokomea,
nao waliowasonga Wayuda watang'olewa;
Waefuraimu hawatawaonea Wayuda wivu tena,
wala Wayuda hawatawasonga Waefuraimu.
14Wataruka pamoja kama ndege,
watue mabegani kwa Wafilisti upande wa baharini,
nako upande wa maawioni kwa jua watawateka wakaao huko;
nchi za Edomu na za Mowabu watazichukua kwa mikono yao,
nao wana wa Amoni watawatii.
15Hata ulimi wa bahari ya Misri Bwana atautia mwiko, ukauke;
nalo lile jito kubwa atalikunjulia mkono wake,
alifokee kwa moto wa makali yake, litokee vijito saba,
watu waweze kupita pasipo kuvua viatu.
16Hivyo patakuwa na njia yao walio sao la ukoo wake,
itakuwa, kama ilivyokuwa kwao Waisiraeli siku ile,
alipowatoa katika nchi ya Misri.