Yesaya 25

Yesaya 25

Utukufu wa ufalme wa Mungu.

1Bwana, wewe ndiwe Mungu wangu, na nikutukuze,

na nilishukuru Jina lako, kwani umefanya mataajabu,

mashauri yako ya kale hayakugeuka, yametimia kweli.

2Kwani mji umeugeuza kuwa chungu la mawe,

mji wenye boma ukawa mabomoko,

majumba ya wageni hayafikiwi tena,

kwani mji hautajengwa kale na kale.

3Kwa hiyo watu wenye nguvu wanakutukuza,

nayo miji ya watu wa kimizimu

waliokuwa wenye ukorofi inakuogopa.

4Kwani umekuwa ngome ya wanyonge

na ngome ya wakiwa, waliposongeka,

ukawa kimbilio penye kimbunga na kivuli penye jua kali,

kwani kufoka kwao wakorofi ni kama kimbunga ukutani,

5au kama jua kali jangwani.

Makelele ya wageni ukayanyamazisha;

kama jua kali linavyoshindwa na kivuli cha wingu,

ndivyo, shangwe za wakorofi zilivyonyenyekezwa.

6Bwana Mwenye vikosi atayafanyia makabila yote ya watu

karamu ya manono huku mlimani,

itakuwa karamu yenye mvinyo kali

na vilaji vyenye mafuta ya kiini,

nazo mvinyo hizo zitakuwa zimechujwa.

7Mlimani huku atayatowesha mabuibui ya nyuso,

ni mabuibui yaliyoyafunika makabila yote ya watu,

hata mafuniko, yaliyotandwa juu ya wamizimu wote.

8Kufa nako atakumeza,

kutoweke kale na kale;

kisha Bwana Mungu atayafuta

machozi nyusoni pao wote,

nayo matwezo yao walio ukoo wake

atayaondoa katika nchi zote, kwani Bwana amevisema.

9Siku ile watasema: Mtazameni huyu!

Ndiye Mungu wetu, tuliyemngojea, atuokoe;

huyu ndiye Bwana, tuliyemngojea.

Na tushangilie! Na tuufurahie wokovu wake!

10Kwani mkono wake Bwana utatulia mlimani huku,

lakini Wamoabu watakanyagwa kwao,

kama majani makavu yanavyokanyagwa majini penye mavi.

11Ijapo wapanue mikono yao mle ndani,

kama mwogeleaji anavyoipanua, apate kuogelea.

lakini kwa kuwa walijikuza, yeye atawainamisha chini

pamoja na mikono yao ihimizayo mizungu ya bure.

12Hata maboma yenu yenye kuta ndefu atayanyenyekeza,

akiyainamisha na kuyaangusha chini uvumbini.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania