The chat will start when you send the first message.
1Sedekia, mwana wa Yosia, akawa mfalme mahali pake Konia, mwana wa Yoyakimu, aliyemweka Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, kuwa mfalme wa Yuda.[#2 Fal. 24:17.]
2Yeye na watumishi wake na watu wa nchi yake hawakuyasikia maneno ya Bwana, aliyoyasema kwa kumtumia mfumbuaji Yeremia.
3Mfalme Sedekia akamtuma Yukali, mwana wa Selemia, na Sefania, mwana wa mtambikaji Masea, kwenda kwa Yeremia kumwambia: Tuombee kwake Bwana Mungu wetu![#Yer. 42:2; Yes. 37:4.]
4Kwani Yeremia alikuwa akiingia, tena akitoka kwa watu, hawakumfunga katika nyumba ya kifungo.
5Ndipo, vikosi vya Farao vilipotoka Misri; Wakasidi waliousonga Yerusalemu walipousikia uvumi wao, wakaondoka hapo Yerusalemu.
6Neno la Bwana likamjia mfumbuaji Yeremia kwamba:
7Hivi ndivyo, Bwana Mungu wa Isiraeli anavyosema: Haya ndiyo, mmwambie mfalme wa Yuda aliyewatuma kwangu kuniuliza: Tazama! Vikosi vya Farao vilivyotoka kwao kuja kuwasaidia wamekwisha kurudi katika nchi yao ya Misri.
8Lakini Wakasidi watarudi, waupigie mji huu vita; nao watauteka na kuuteketeza kwa moto.
9Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Msijidanganye wenyewe na kusema: Wakasidi wataondoka kwetu kwenda zao! Kwani hawatakwenda.
10Kwani kama mngevipiga vikosi vyote vya Wakasidi wanaopigana nanyi, wakasalia kwao watu wenye vidonda tu, wangeinuka kila mtu katika hema lake, wauteketeze mji huu kwa moto.
11Ikawa, vikosi vya Wakasidi vilipoondoka Yerusalemu kwa kuvikimbia vikosi vya Farao,
12ndipo, Yeremia naye alipotoka Yerusalemu kwenda katika nchi ya Benyamini, alichukue fungu lake lililoko kule kwa watu wa huko katikati.[#Yer. 32:9.]
13Alipofika penye lango la Benyamini, kulikuwako mkuu wa walinzi, jina lake Iria, mwana wa Selemia, mwana wa Hanania, akamkamata mfumbuaji Yeremia kwamba: Utawaangukia Wakasidi wewe!
14Yeremia akajibu: Ni uwongo! Mimi siwaangukii Wakasidi, lakini hakumsikia; ndipo, Iria alipomkamata Yeremia na kumpeleka kwa wakuu.
15Wakuu wakamtolea Yeremia ukali, wakampiga; kisha wakamtia kifungoni nyumbani mwa mwandishi Yonatani, kwani walikuwa wakiitumia kuwa nyumba ya kifungo.[#Yer. 20:2.]
16Hivi ndivyo, Yeremia alivyoingia katika ile nyumba yenye mashimo yaliyochimbuliwa upande wa ndani chini; ndimo, Yeremia alimokaa siku nyingi.
17Kisha mfalme Sedekia akatuma kumchukua; mfalme akamwuliza nyumbani mwake penye njama kwamba: Liko neno lililotoka kwa Bwana? Yeremia akasema: Liko; kisha akamwambia: Utatiwa mkononi mwa mfalme wa Babeli.[#Yer. 34:21.]
18Yeremia akamwuliza mfalme Sedekia: Nimekukosea nini au watumishi wako au watu wa ukoo huu, mkinitia kifungoni?
19Wako wapi wafumbuaji wenu waliowafumbulia kwamba: Mfalme wa Babeli hatafika kwenu wala katika nchi hii?
20Sasa sikiliza, bwana wangu mfalme, nayo malalamiko yangu na yakuangukie usoni: Usinirudishe nyumbani mwa Yonatani, nisife mle!
21Mfalme Sedekia alipotoa amri, wakamfunga Yeremia tena uani penye kifungo, akapewa kila siku mkate wa ngano uliotoka huko, wachoma mikate wanakokaa, mpaka mikate ilipotoweka mjini. Ndivyo, Yeremia alivyopata kukaa uani penye kifungo.[#Yer. 32:2.]