Mateo 2

Mateo 2

Wachunguza nyota wa maawioni kwa jua

1Yesu alipokwisha kuzaliwa Bet-Lehemu wa Uyuda wakati wa mfalme Herode, ndipo, walipofika Yerusalemu wachunguza nyota waliotoka upande wa maawioni kwa jua.[#Luk. 2:1-7.]

2Wakasema: Yuko wapi aliyezaliwa kuwa mfalme wa Wayuda? Kwani tumeiona nyota yake katika nchi ya maawioni kwa jua, basi, tumekuja kumwangukia.[#4 Mose 24:17; Yes. 60:6.]

3Mfalme Herode alipoyasikia haya akahangaika, nao Yerusalemu wote pamoja naye.

4Akawakusanya wote waliokuwa watambikaji wakuu na waandishi wa kwao akapeleleza kwao mahali, Kristo atakapozaliwa.

5Nao wakamwambia: Atazaliwa Beti-Lehemu wa Uyuda, kwani ndivyo, alivyoandika mfumbuaji:[#Mika 5:1; Yoh. 7:42.]

6Nawe Beti-Lehemu wa nchi ya Yuda,

hu mdogo kamwe katika majumbe ya Yuda.

Kwani mwako ndimo, atakamotoka mtawala

atakayewachunga walio ukoo wangu wa Isiraeli.

7Kisha Herode akawaita wale wachunguza nyota na kufichaficha, akazidi kuwauliza vema siku, ile nyota ilipooneka.

8Akawatuma Beti-Lehemu akisema: Nendeni, mkapeleleze sana habari za mtoto huyo! Mtakapomwona mnipashe habari, nami nipate kwenda nimwangukie.

9Nao walipokwisha msikia mfalme wakashika njia. Walipotazama, ile nyota, waliyoiona maawioni kwa jua, ikawatangulia, mpaka ikaja kusimama juu sawa ya mle alimokuwa yule mtoto.

10Walipoiona hiyo nyota wakafurahi furaha kubwa mno.

11Wakaingia nyumbani mle, wakamwona mtoto pamoja na mama yake Maria, wakamwangukia na kumnyenyekea. Walipokwisha wakayafungua malimbiko yao, wakamtolea mtoto tunu, dhahabu na uvumba na manemane.[#Sh. 72:10,15; Yes. 60:6.]

12Nao walipoonywa kwa ndoto, wasimrudie Herode, wakashika njia nyingine, wakaenda kwao.*

Kukimbilia Misri.

13Hao walipokwisha kwenda zao, malaika wa Bwana akamtokea Yosefu katika ndoto akisema: Inuka, mchukue mtoto na mama yake, ukimbilie Misri, ukakae huko, mpaka nitakapokuambia! Kwani Herode atamtafuta mtoto, amwangamize.

14Kisha akainuka, akamchukua mtoto na mama yake usiku, akaenda Misri.

15Akakaa huko, mpaka Herode alipokwisha kufa, lipata kutimia neno, Bwana alilolisema kwa mfumbuaji:[#Hos. 11:1.]

Misri ndiko, nilikomwitia mwanangu.

Kuuawa kwa watoto.

16Herode alipoona, ya kuwa wale wachunguza nyota wamemdanganya akakasirika sana, akatuma watu, wawaue watoto waume wote waliokuwako Beti-Lehemu na vilimani pake pote, waliokuwa wa miaka miwili nao waliopungua, kama alivyoipeleleza siku kwao wachunguza nyota.

17Ndipo, lilipotimia lililosemwa na mfumbuaji Yeremia kwamba:[#Yer. 31:15.]

18Sauti imesikiwa Rama, ni kilio na maombolezo mengi.

Raheli anawalilia watoto wake, hakutaka kubembelezwa,

kwani hawako.

Kurudi.

19Herode alipokwisha kufa, mara malaika wa Bwana akamtokea Yosefu kwa ndoto huko Misri, akamwambia:

20Inuka, umchukue mtoto na mama yake, uende katika nchi ya Isiraeli! Kwani wamekwisha kufa waliotafuta kumwua mtoto.[#2 Mose 4:19.]

21Ndipo, alipoinuka, akamchukua mtoto na mama yake, akaiingia nchi ya Isiraeli.

22Lakini aliposikia, ya kuwa Arkelao ametawala Yudea mahali pa Herode, baba yake, akaogopa kwenda huko. Basi akaagizwa kwa ndoto, aende zake pande za Galilea;

23kwa hiyo akaja, akakaa mji uitwao Nasareti, lipate kutimia lililosemwa na wafumbuaji:

Ataitwa Mnasareti.*

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania