The chat will start when you send the first message.
1Mwana mwerevu wa kweli humfurahisha baba yake,
lakini mwana mpumbavu humpatia mama yake majonzi.
2Malimbiko yaliyopatwa kwa uovu hayafai kitu,
lakini wongofu huponya kufani.
3Bwana hatamwacha mwongofu, afe kwa njaa,
lakini tamaa zao wasiomcha huzikumba.
4Afanyaye kazi na kulegeza mikono hapati kitu,
lakini mikono yao wajihimizao hupata mali.
5Avunaye siku za kipupwe ni mwenye akili,
lakini alalaye siku za mavuno hujipatia soni.
6Mbaraka hukikalia kichwa cha mwongofu,
lakini vinywani mwao wasiomcha Mungu yamo makorofi.
7Ukumbuko wa mwongofu huleta mbaraka,
lakini majina yao wasiomcha Mungu huoza.
8Mwerevu wa moyo huonyeka,
lakini mjinga anayejisemea tu hujiangamiza.
9Aendeleaye pasipo kukosa huenda na kutulia,
lakini azipotoaye njia zake hujulikana.
10Akonyezaye kwa jicho hukasirisha,
naye mjinga anayejisemea tu hujiangamiza.
11Kinywa cha mwongofu ni kisima cha uzima,
lakini vinywani mwao wasiomcha Mungu yamo makorofi.
12Uchukivu huleta magomvi,
lakini upendo huyafunika makosa yote.
13Midomoni mwake mtambuzi huoneka werevu wa kweli,
lakini apotelewaye na akili hupaswa na fimbo mgongoni.
14Werevu wa kweli hulimbika ujuzi,
lakini kinywa chake mjinga ni mwangamizo ulio karibu.
15Mali zake mkwasi ni boma lake lenye nguvu,
lakini ukosefu wao wanyonge kuwalegeza mioyo.
16Kazi yake mwongofu humwelekeza penye uzima,
lakini mapato yake asiyemcha Mungu humkosesha.
17Aangaliaye akikanywa yumo katika njia ya kwenda uzimani,
lakini akataaye maonyo hujipoteza.
18Mwenye uchukivu moyoni husema madanganyifu,
naye aenezaye masingizio ni mpumbavu.
19Asemaye maneno mengi hakosi kuwa mpotovu,
lakini ajuaye kuizuia midomo yake ni mjuzi kweli.
20Ulimi wa mwongofu ni fedha zilizochaguliwa,
lakini mioyo yao wasiomcha Mungu haina kima.
21Midomo ya mwongofu hulisha wengi,
lakini wajinga hufa kwa kupotelewa na akili.
22Mbaraka ya Bwana huwapatia watu mali,
lakini masumbuko ya mtu hayaziongezi kamwe.
23Kwake mpumbavu ni kama mchezo kufanya mabaya, ayawazayo moyoni,
lakini mtu mwenye utambuzi hufanya yenye werevu wa kweli.
24Asiyemcha Mungu anayoyaogopa, ndiyo yanayomjia,
lakini waongofu hupewa wayatakayo.
25Upepo mkali unapopitia, asiyemcha Mungu hayupo tena,
lakini mwongofu anao msingi wa kale na kale.
26Kama siki inavyoyatendea meno na kama moshi unavyoyatendea macho,
ndivyo, mvivu anavyowatendea waliomtuma.
27Kumcha Bwana huziongeza siku za kuwapo,
lakini miaka yao wasiomcha Mungu hukatwa.
28Kungojea kwao waongofu hugeuka kuwa furaha,
lakini matumaini yao wasiomcha Mungu hupotea.
29Njia ya Bwana ni ngome yake amchaye Mungu,
lakini ni mwangamizo wao wafanyao maovu.
30Mwongofu hatukusiki kale na kale,
lakini wasiomcha Mungu hawatakaa katika nchi.
31Kinywa cha mwongofu huchipuza yenye werevu wa kweli,
lakini ulimi usemao mapotovu utang'olewa.
32Midomo ya mwongofu huyajua yapendezayo,
lakini vinywa vyao wasiomcha Mungu hujua mapotovu.