Mifano 17

Mifano 17

Werevu na ujinga unavyosema.

1Kula kitonge kikavu cha wali na kutulia ni kwema,

kuliko karamu za nyumbani mlimo na magomvi tele.

2Mtumishi mwenye akili humshinda mwana wa bwana wake atwezaye,

hugawanya mali zilizoachawa na Bwana pamoja na ndugu zake yule.

3Chungu cha kuyeyushia hujaribu fedha, nayo tanuru hujaribu dhahabu,

lakini aijaribuye mioyo ni Bwana.

4Mtenda mabaya husikiliza midomo isemayo mapotovu,

mwongo naye hutega sikio penye ulimi usemao mateto.

5Afyozaye maskini humsimanga aliyemwumba,

afurahiaye mwangamizo hana budi hupatilizwa.

6Kilemba cha wazee ni wana wa wana wao,

nao utukufu wa wana ndio wazazi wao.

7Mjinga hapaswi na maneno mazuri,

sembuse mkuu na maneno ya uwongo!

8Matunzo ni kama kito kipendezacho machoni pake ayatoaye,

po pote anapojielekeza hufanikiwa.

9Afunikaye makosa hutafuta kupendwa,

lakini azushaye mambo ya kale hutenganisha rafiki waliopendana.

10Mtambuzi akikanywa husikia zaidi

kuliko mpumbavu akipigwa fimbo mia.

11Mbaya anayoyatafuta ni ukatavu tu,

kwa hiyo kwake hutumwa mjumbe mshupavu.

12Kukutana na chui mke aliyenyang'anywa watoto ni kwema

kuliko kukutana na mpumbavu aufuataye ujinga wake.

13Mtu aliyepata mema akiyalipa kwa kufanya mabaya,

basi, nyumbani mwake yeye mabaya hayakomeki.

14Kuzua magomvi ni kufungua maji, yajiendee tu;

kwa hiyo acha magomvi ukiwa hujakenua meno bado.

15Kumkania akosaye na kumsingizia asiyekosa,

kote kuwili humtapisha Bwana.

16Je? Fedha mkononi mwa mpumbavu ni za nini?

Za kununua werevu wa kweli? Tena akili haziko!

17Rafiki hupenda siku zote,

naye huzaliwa penye masongano, awe ndugu kweli.

18Mtu aliyepotelewa na akili ni yule anayepeana mkono na mwingine,

anayejitoa kwa mwingine kuwa dhamana ya mwenziwe.

19Apendaye ugomvi hupenda kupotoa,

aukuzaye mlango wake hutafuta mbomoko.

20Mwenye moyo mdanganyifu hapati mema,

naye mwenye ulimi wa upotovu huangushwa na mabaya.

21Azaaye mpumbavu hujipatia majonzi,

hata babake mjinga hapati furaha.

22Moyo wenye furaha husaidia vema kupona magonjwa,

lakini roho ipondekayo hukausha kiini cha mifupa.

23Asiyemcha Mungu huchukua mapenyezo na kuyaficha kifuani,

ayapotoe mashauri, yasifuate njia zilizo sawa.

24Machoni pake mtambuzi upo werevu wa kweli,

lakini macho ya mpumbavu hutembea mapeoni kwa nchi.

25Mwana mpumbavu humsikitisha baba yake,

naye mama yake aliyemzaa humpatia machungu.

26Mtu asiyekosa haifai humtoza fedha,

wala hupiga wakuu kwa ajili ya unyofu wao.

27Ayazuiaye maneno yake ni mwenye ujuzi wa kweli,

naye aitulizaye roho yake ni mtu mtambuzi.

28Naye mjinga akinyamaza huwaziwa kuwa mwerevu wa kweli,

aifumbaye midomo yake ni mtambuzi.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania