The chat will start when you send the first message.
1Mwanangu, usikilize werevu wangu ulio wa kweli!
Utegee utambuzi wangu sikio lako,
2upate kuyaangalia mawazo ya moyo,
midomo yako nayo iulinde ujuzi!
3Kwani midomo ya mwanamke mgeni hudondosha asali,
kinywa chake nacho huteleza kuliko mafuta.
4Lakini mwisho hutokeza uchungu ulio mkali kuliko wa shubiri,
hukata kuliko upanga wenye makali pande mbili.
5Miguu yake hushukia kifo,
kuzimuni ndiko, mwenendo wake unakoelekea,
6asiishike njia iendayo uzimani iliyo sawa,
wala asijue, jinsi mapito yake yanavyopotea.
7Sasa wanangu, nisikieni!
Msiyaache maneno ya kinywa changu!
8Iangalie njia yako, impitie mbali,
usipafikie karibu pa kuingia nyumbani mwake,
9usiwape wengine yaliyo utukufu wako,
wala miaka yako isikatwe na mtu asiyeona huruma!
10Wageni wasijishibishe mali zako, nguvu yako ilizokupatia,
wala mapato, uliyoyasumbukia, yasipelekwe nyumbani mwa wengine!
11Mwisho ukikufikia, utapiga kite;
nyama na nguvu za mwili wako zitakapokuwa zimeishilizwa,
12ndipo, utakaposema: Kumbe nilichukizwa nilipoonywa,
moyo wangu ukakataa kuchapwa!
13Sikuzisikia sauti za wafunzi wangu,
wala sikuwategea sikio langu walionifundisha.
14Ikasalia kidogo, wote mzima nikashikwa na mabaya,
nilipokuwa katikati ya mkutano wao wakatao mashauri.
15Yanywe maji ya shimo lako wewe,
nayo maji yabubujikayo katika kisima chako!
16Je? Chemchemi zako zitawanyike nje?
navyo vijito vya maji vitawanyike viwanjani?
17La, sharti maji yao yawe yako peke yako,
yasiwe ya wageni pamoja na wewe!
18Kisima chako na kibarikiwe,
upate kufurahia mke wa ujana wako!
19Anafanana na kulungu mke apendezaye,
tena na paa mke afurahishaye,
maziwa yake yakuchangamshe siku zote,
kwa upendo wake na uwe pasipo kukoma kama mtu alewaye.
20Mwanangu, mbona unataka kujilewesha kwa mwanamke mgeni?
Mbona unataka kukumbatia kifua cha mwanamke wa mwingine?
21Kwani machoni pa Bwana njia za kila mtu ziko waziwazi,
yeye ndiye anayeyatengeneza mapito ya kila mtu.
22Manza, alizozikora mwenyewe, zitamnasa asiyemcha Mungu,
akamatwe na kamba za makosa yake.
23Huyo atakufa, kwa kuwa hakuonyeka,
kwa ujinga wake mwingi atapepesuka, aanguke.