Warumi 12

Maisha mapya katika Kristo

1Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana.[#Rum 6:11,13; 1 Pet 2:5; Yn 4:24]

2Wala msifuate kanuni za dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.[#Efe 4:23; 5:10,17; Rum 1:28; Gal 1:4]

3Kwa maana kwa neema niliyopewa namwambia kila mtu aliyeko kwenu asinuie makuu kupita ilivyompasa kunuia; bali awe na nia ya kiasi, kama Mungu alivyomgawia kila mtu kiasi cha imani.[#1 Kor 12:11; Efe 4:7]

4Kwa kuwa kama vile katika mwili mmoja tuna viungo vingi, wala viungo vyote havitendi kazi moja;[#1 Kor 12:12]

5Vivyo hivyo na sisi tulio wengi tu mwili mmoja katika Kristo, na viungo, kila mmoja kwa mwenzake.[#1 Kor 12:27; Efe 4:25]

6Basi kwa kuwa tuna karama zilizo mbalimbali, kwa kadiri ya neema tuliyopewa; ikiwa ni unabii, tutoe unabii kwa kadiri ya imani;[#1 Kor 12:4-11]

7ikiwa ni huduma, tuwemo katika huduma yetu; mwenye kufundisha, katika kufundisha kwake;[#1 Pet 4:10,11]

8mwenye kuonya, katika kuonya kwake; mwenye kukirimu, kwa moyo mweupe; msimamizi, na asimamie kwa bidii; anayerehemu, na arehemu kwa furaha.[#Mt 6:3; 2 Kor 8:2; 9:7]

Sifa za Mkristo

9Pendo na lisiwe na unafiki lichukieni lililo ovu, mkilishika lililo jema.[#1 Pet 1:22; 1 Tim 1:5; Amo 5:15]

10Kwa pendo la udugu, mpendane ninyi kwa ninyi; kwa heshima mkiwatanguliza wenzenu;[#2 Pet 1:7; Flp 2:3]

11kwa bidii, bila kulegea; mkiwa na juhudi katika roho zenu; mkimtumikia Bwana;[#Ufu 3:15; Mdo 18:25]

12kwa tumaini, mkifurahi; katika dhiki, mkisubiri; mkidumu katika kusali;[#1 The 5:17]

13kwa mahitaji ya watakatifu, mkifuata ukarimu; katika kukaribisha wageni mkijitahidi.[#Ebr 13:2]

14Wabarikini wanaowaudhi; barikini, wala msilaani.[#Mt 5:44; Lk 6:28; Mdo 7:59; 1 Kor 4:12]

15Furahini pamoja nao wafurahio; lieni pamoja nao waliao.[#Zab 35:13]

16Mpatane nia zenu ninyi kwa ninyi. Msinuie yaliyo makuu, lakini mkubali kushughulishwa na mambo manyonge. Msiwe watu wa kujivunia akili.[#Mit 3:7; Rum 15:5; 11:20]

17Msimlipe mtu ovu kwa ovu. Angalieni yaliyo mema machoni pa watu wote.[#Isa 5:21; 1 The 5:15]

18Ikiwezekana, kwa upande wenu, mkae katika amani na watu wote.[#Mk 9:50; Ebr 12:14]

19Wapenzi, msijilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu; maana imeandikwa, Kisasi ni juu yangu mimi; mimi nitalipa, anena Bwana.[#Kum 32:35; Law 19:18; Mt 5:39; 2 The 1:6,7; Rum 13:4; Ebr 10:30]

20Lakini, Adui yako akiwa na njaa, mlishe; akiwa na kiu, mnyweshe; maana ufanyapo hivyo, utampalia makaa ya moto kichwani pake.[#Mit 25:21-22; Mt 5:44]

21Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya