1 Samweli 22

1 Samweli 22

Daudi na wafuasi wake wakiwa Adalumu

1Basi Daudi akaondoka huko, akakimbilia pango la Adulamu; na ndugu zake na watu wote wa ukoo wa baba yake waliposikia habari hiyo, wakamwendea huko.[#Zab 57:1; 142:1; Yos 12:15; 2 Sam 23:13; 1 Fal 17:3; Mik 1:15; Ebr 11:38]

2Na kila mtu aliyekuwa katika hali ya dhiki, na kila mtu aliyekuwa na deni, na watu wote wenye uchungu mioyoni mwao, wakakusanyika kwake; naye akawa jemadari wao; nao waliokuwa pamoja naye walikuwa kama watu mia nne.[#Amu 11:3]

3Kutoka huko Daudi akaenda Mispa ya Moabu; akamwambia mfalme wa Moabu, Tafadhali wakubalie baba yangu na mama yangu watoke huko waliko, wakakae kwenu, hata nitakapojua Mungu atakalotenda kwa ajili yangu.[#Mwa 47:11; Kut 20:12; Law 19:3; Kum 5:16; Mit 10:1; 23:24; Mt 19:19; Yn 19:25-27; Efe 6:2; 1 Tim 5:4]

4Akawaleta mbele ya mfalme wa Moabu, nao wakakaa pamoja naye wakati wote Daudi alipokuwa ngomeni.

5Kisha nabii Gadi akamwambia Daudi, Usikae hapa ngomeni; ondoka, ukaende mpaka nchi ya Yuda. Ndipo Daudi akaondoka, akaenda zake, akakaa katika msitu wa Herethi.[#2 Sam 24:11; 1 Nya 21:9; 2 Nya 29:25]

Sauli awaua manabii huko Nobu

6Kisha Sauli akasikia ya kwamba Daudi ameonekana, na wale watu waliokuwa pamoja naye. Basi Sauli alikuwa akikaa Gibea, chini ya mkwaju katika mahali palipoinuka, naye alikuwa na mkuki wake mkononi, na watumishi wake wote wakimzunguka.

7Naye Sauli akawaambia watumishi wake waliomzunguka, Sikieni sasa, enyi Wabenyamini; je! Huyu mwana wa Yese atawapa ninyi kila mmoja mashamba, na mashamba ya mizabibu, atawafanya kuwa wakuu wa watu maelfu, na wakuu wa watu mamia;[#1 Sam 8:14]

8hata ninyi nyote mkanifitinia, wala hapana mtu anifunuliaye habari hii mwanangu afanyapo agano na mwana wa Yese, wala hapana mmoja wenu anayenisikitikia, wala kunifunulia ya kuwa mwanangu amemchochea mtumishi wangu, anivizie kama hivi leo?[#1 Sam 20:2; 18:3; 23:16-18]

9Ndipo akajibu Doegi, Mwedomi, aliyesimama karibu na watumishi wa Sauli, akasema, Mimi nilimwona mwana wa Yese akienda Nobu, kwa Ahimeleki, mwana wa Ahitubu.[#1 Sam 21:1,7; 14:3]

10Naye akamwuliza BWANA kwa ajili yake, akampa vyakula, akampa na ule upanga wa Goliathi, Mfilisti.[#Hes 27:21; 1 Sam 21:6,9]

11Ndipo mfalme akatuma watu waende kumwita Ahimeleki, kuhani, mwana wa Ahitubu, na jamaa yote ya baba yake, hao makuhani, waliokuwako huko Nobu; nao wakaenda kwa mfalme wote pia.

12Sauli akasema, Sikia sasa, Ewe mwana wa Ahitubu. Naye akaitika, Mimi hapa, bwana wangu.

13Sauli akamwuliza, Mbona mmefanya fitina juu yangu, wewe na mwana wa Yese? Kwa maana umempa mikate, na upanga, nawe umemwuliza Mungu kwa ajili yake, ili aniasi na kunivizia kama hivi leo?

14Basi Ahimeleki akamjibu mfalme, akasema, Katika watumishi wako wote ni nani aliye mwaminifu kama Daudi, aliye mkwewe mfalme, tena msiri wako, mwenye heshima nyumbani mwako?[#1 Sam 19:4,5; 20:32; 24:11; Mit 31:9]

15Je! Mimi nimeanza leo tu kumwuliza Mungu kwa ajili yake? Hasha! Mfalme asinidhanie mimi, mtumishi wake neno hili, Wala jamaa yote ya baba yangu, kwa maana mimi, mtumishi wako siyajui hayo yote, yaliyopungua au yaliyozidi.

16Naye mfalme akasema, Kufa utakufa, Ahimeleki, wewe na jamaa yote ya baba yako.

17Kisha mfalme akawaambia askari walinzi waliosimama karibu naye Geukeni, mkawaue hao makuhani wa BWANA, kwa sababu mkono wao u pamoja na Daudi, na kwa sababu walijua ya kuwa amekimbia, wasiniarifu. Lakini watumishi wa mfalme walikataa kunyosha mkono na kuwaangukia makuhani wa BWANA.[#Kut 1:17; Mdo 4:19; 5:29]

18Basi mfalme akamwambia Doegi, Geuka wewe, uwaangukie hao makuhani. Basi Doegi, Mwedomi, akageuka, akawaangukia makuhani, akaua siku ile watu themanini na watano wenye kuvaa naivera ya kitani.[#Zab 12:5; Mit 28:15; 1 Sam 2:31; Kut 28:40]

19Kisha akaupiga Nobu, mji wa makuhani, kwa makali ya upanga, wanaume na wanawake, watoto na wanyonyao, na ng'ombe, na punda, na kondoo.[#Neh 11:32; Isa 10:32; Ayu 20:19,20; Zab 10:1-18; Isa 26:13]

20Na katika wana wa Ahimeleki, mwana wa Ahitubu, akaokoka mtu mmoja tu, aliyeitwa Abiathari, akamkimbilia Daudi.[#1 Sam 23:6; Amu 9:5; 1 Sam 2:33; Ayu 1:15,19]

21Naye Abiathari akamweleza Daudi ya kwamba Sauli amewaua makuhani wa BWANA.

22Daudi akamwambia Abiathari, Siku ile alipokuwako Doegi, Mwedomi, nilijua hakika ya kuwa atamwambia Sauli; mimi nimewapatia watu wote wa jamaa ya baba yako kifo.

23Kaa wewe pamoja nami, usiogope; kwa maana yeye atafutaye roho yangu, ndiye atafutaye na roho yako; nawe utakaa kwangu salama.[#1 Fal 2:26; Mt 24:9; Yn 15:20,21; 16:2; Ebr 12:1-3]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya