The chat will start when you send the first message.
1Yehoshafati akalala na babaze, akazikwa pamoja na babaze katika mji wa Daudi; Yehoramu mwanawe akatawala mahali pake.
2Naye alikuwa na ndugu, wana wa Yehoshafati, Azaria, Yehieli, Zekaria, Azaria, Mikaeli, na Shefatia; hao wote walikuwa wana wa Yehoshafati mfalme wa Yuda.[#21:2 Makala ya Kiebrania ni Israeli.]
3Baba yao akawapa zawadi kubwa, za fedha, za dhahabu, na za tunu, pamoja na miji yenye maboma katika Yuda; lakini ufalme akampa Yehoramu, kwa sababu alikuwa mzaliwa wa kwanza.
4Basi Yehoramu alipoinuliwa juu ya ufalme wa babaye, na kujiimarisha, akawaua nduguze wote kwa upanga, na baadhi ya wakuu wa Israeli pia.[#Mwa 4:8; Amu 9:5; 1 Yoh 3:12]
5Yehoramu alikuwa na umri wa miaka thelathini na miwili alipoanza kutawala, akatawala miaka minane huko Yerusalemu.
6Akaiendea njia ya wafalme wa Israeli, kama walivyofanya nyumba ya Ahabu; kwa kuwa alikuwa amemwoa binti Ahabu; akafanya maovu machoni pa BWANA.[#2 Fal 8:18; 2 Nya 18:1; 22:2; Neh 13:26]
7Walakini BWANA hakupenda kuiharibu nyumba ya Daudi, kwa sababu ya agano alilolifanya na Daudi, na kama alivyomwahidi kuwa atampa taa, yeye na wazao wake siku zote.[#2 Sam 7:12,13; 1 Fal 11:36; 2 Fal 8:19; Zab 132:11]
8Wakati wa enzi zake Edomu wakaasi utawala wa Yuda, wakajifanyia mfalme.[#Mwa 27:40; 2 Fal 8:20; 9:22; Zab 106:39; Ufu 17:1-5]
9Ndipo Yehoramu akavuka na makamanda wake, na magari yake yote pamoja naye; akaondoka usiku, akawapiga Waedomi waliomzunguka yeye na hao makamanda wa magari.
10Hivyo Edomu wakaasi utawala wa Yuda hata leo; wakati huo uo nao Libna wakaasi utawala wake: kwa sababu alikuwa amemwacha BWANA, Mungu wa baba zake.[#Mwa 27:40]
11Tena ndiye aliyetengeneza mahali pa juu katika milima ya Yuda, na kuongoza wakazi wa Yerusalemu kukosa uaminifu na kufanya Yuda ipotoke.[#Law 17:7; 20:5]
12Barua kutoka nabii Eliya ilimjia, ikisema, BWANA, Mungu wa Daudi baba yako, asema hivi, Kwa kuwa hukuziendea njia za Yehoshafati baba yako, wala njia za Asa mfalme wa Yuda;
13lakini umeiendea njia ya wafalme wa Israeli, ukawaongoza Yuda na wakazi wa Yerusalemu kwenye kukosa uaminifu, kama walivyofanya nyumba ya Ahabu; tena umewaua ndugu zako wa nyumba ya baba yako, waliokuwa wema kuliko wewe;[#Kut 34:15; 2 Fal 9:22]
14tazama, BWANA atawapiga pigo kubwa watu wako, na watoto wako, na wake zako, na mali yako yote;
15nawe utakuwa na ugonjwa mkuu kwa maradhi ya matumbo, yatakapotokea matumbo yako kwa sababu ya ugonjwa huo siku kwa siku.
16BWANA akawaamsha roho Wafilisti, na Waarabu walioelekeana na Wakushi juu ya Yehoramu,[#2 Sam 24:1; 1 Fal 11:14,23; 2 Nya 22:1]
17nao wakakwea juu ya Yuda, wakaipenya, wakaichukua mali yote iliyoonekama nyumbani mwa mfalme, na wanawe pia, na wakeze; asibakizwe mtoto hata mmoja, ila Ahazia, aliyekuwa mdogo miongoni mwa wanawe.[#2 Nya 24:7; #21:17 Au, Yehoahazi.]
18Na baada ya hayo yote BWANA akampiga matumbo kwa ugonjwa usioponyeka.
19Ikawa baada ya siku, kufika mwisho wa mwaka wa pili, matumbo yake yakatokea kwa sababu ya ugonjwa wake, akafa akiwa kwenye maumivu makali. Wala watu wake hawakuwasha moto kuombolezea kifo chake kama walivyowafanyia baba zake.
20Alikuwa na umri wa miaka thelathini na miwili alipoanza kutawala, akatawala huko Yerusalemu miaka minane; akafariki bila kutamaniwa; wakamzika mjini mwa Daudi, ila si katika makaburi ya wafalme.