The chat will start when you send the first message.
1Basi kulikuwa na vita siku nyingi kati ya nyumba ya Sauli na nyumba ya Daudi; Daudi akaendelea akasitawi, lakini nyumba ya Sauli ikaendelea kudhoofika.[#Zab 46:9; Isa 2:4; Mik 4:3; Mt 10:35,36; Gal 5:17; Efe 6:12]
2Naye Daudi akazaliwa wana huko Hebroni; mzaliwa wake wa kwanza alikuwa Amnoni, wa Ahinoamu wa Yezreeli;[#1 Nya 3:1; 1 Sam 25:43]
3na wa pili wake Danieli, wa Abigaili mkewe Nabali wa Karmeli; na wa tatu Absalomu, mwana wa Maaka binti Talmai, mfalme wa Geshuri,[#2 Sam 13:37; 1 Sam 27:8]
4na wa nne Adoniya, mwana wa Hagithi; na wa tano Shefatia, mwana wa Abitali;[#1 Fal 1:5; 2:13-25]
5na wa sita Ithreamu, wa Egla, mkewe Daudi. Hawa walizaliwa kwa Daudi huko Hebroni.
6Ikawa, wakati vilipokuwapo vita kati ya nyumba ya Sauli na nyumba ya Daudi, Abneri akajipatia nguvu nyumbani kwa Sauli.[#2 Sam 2:8,9; 2 Nya 25:8]
7Basi Sauli alikuwa na suria, jina lake akiitwa Rispa, binti Aya; Ishboshethi akamwuliza Abneri, Kwa nini umeingia kwa suria ya babangu?[#2 Sam 21:8,10]
8Basi Abneri akakasirika kwa maneno ya Ishboshethi, akasema, Je! Mimi ni kichwa cha mbwa, aliye wa Yuda? Hata leo hivi nawafanyia fadhili nyumba ya Sauli babako, na ndugu zake, na rafiki zake, nisikutie wewe mkononi mwa Daudi; nawe hata hivyo unanitia hatiani leo kwa mwanamke huyu.[#Kum 23:18; 1 Sam 24:15; 2 Sam 16:9]
9Mungu amfanyie Abneri vivyo hivyo, na kuzidi, nisipomtendea Daudi kama vile BWANA alivyomwapia;[#1 Sam 15:28; 16:1,12; 1 Nya 12:23; Rut 1:17; 1 Fal 19:2; Zab 78:70; 89:19,20; Mdo 13:22]
10kuupitisha ufalme toka nyumba ya Sauli, na kukisimamisha kiti cha Daudi juu ya Israeli, na juu ya Yuda, toka Dani mpaka Beer-sheba.[#Amu 20:1; 2 Sam 17:11; 1 Fal 4:25]
11Wala hakuweza kumjibu Abneri tena, kwa sababu alimwogopa.
12Basi Abneri akatuma wajumbe kwa Daudi mahali alipokuwapo, akisema, Nchi hii ni ya nani? Fanya agano nami, na tazama, mkono wangu utakuwa pamoja nawe, ili kuwaleta Israeli wote kwako.
13Daudi akasema, Vema, nitafanya agano nawe, lakini nina sharti moja nitakalo kwako, nalo ni hili; Hutaniona uso wangu, isipokuwa uniletee Mikali, binti Sauli, hapo ujapo kuniona uso wangu.[#Mwa 43:3; 44:23,26; 1 Sam 18:20]
14Basi Daudi akatuma wajumbe kwa Ishboshethi, mwana wa Sauli, kusema, Nipe mke wangu Mikali, niliyemposa kwa govi mia moja za Wafilisti.[#1 Sam 18:25,27]
15Basi Ishboshethi akatuma watu, akamnyang'anya Paltieli, mwana wa Laisha, mumewe, mwanamke huyo.
16Huyo mumewe akafuatana naye, huku akilia, akamfuata mpaka Bahurimu. Ndipo Abneri akamwambia, Haya, rudi. Naye akarudi.[#2 Sam 19:16]
17Basi Abneri akafanya mashauri na wazee wa Israeli, akasema, Zamani mlitaka Daudi awamiliki;
18basi, sasa, fanyeni hayo; kwa maana BWANA amemtaja Daudi, akisema, kwa mkono wa mtumishi wangu, Daudi, nitawaokoa watu wangu Israeli katika mikono ya Wafilisti, na katika mikono ya adui zao wote.
19Tena Abneri alinena masikioni mwa Benyamini; kisha Abneri akaenda ili kunena masikioni mwa Daudi huko Hebroni maneno yote yaliyoonekana kuwa mema machoni pa Israeli, na machoni pa nyumba yote ya Benyamini.[#1 Nya 12:29]
20Basi Abneri akamwendea Daudi huko Hebroni, akiwa na watu ishirini. Daudi akamfanyia karamu Abneri, na watu wote waliokuwa pamoja naye.
21Kisha Abneri akamwambia Daudi, Nitaondoka, niende zangu; nami nitamkusanyia bwana wangu mfalme Israeli wote, ili wafanye agano nawe, ukamiliki juu ya wote inaowatamani roho yako. Basi Daudi akamruhusu Abneri; naye akaenda zake kwa amani.[#Kum 14:26; 1 Fal 11:37; Zab 20:4]
22Na tazama, watumishi wa Daudi pamoja na Yoabu walitoka jeshini, wakaleta nyara nyingi pamoja nao; lakini Abneri hakuwako Hebroni kwa Daudi; maana alikuwa amemruhusu, naye amekwisha kwenda zake kwa amani.
23Hata Yoabu, na jeshi lote waliokuwa pamoja naye, walipofika, watu wakamwambia Yoabu, wakisema, Abneri, mwana wa Neri, alikuja kwa mfalme, naye amemruhusu, naye amekwenda zake kwa amani.
24Basi Yoabu akamwendea mfalme, akasema, Umefanyaje? Tazama, Abneri amekuja kwako; mbona umemruhusu, naye amekwisha kwenda zake?
25Wewe unamjua Abneri, mwana wa Neri, ya kuwa alikuja ili kukudanganya, apate kujua kutoka kwako, na kuingia kwako, akajue yote uyatendayo.[#Hes 27:17; Kum 28:6; 1 Sam 29:6; Zab 121:8; Isa 37:28]
26Naye Yoabu alipotoka kwa Daudi, akatuma wajumbe kumfuata Abneri, wakamrudisha kutoka kisima cha Sira; lakini Daudi alikuwa hana habari.
27Basi Abneri alipokuwa amerudi Hebroni, Yoabu akamchukua kando hadi katikati ya lango, ili aseme naye kwa faragha; akampiga mkuki wa tumbo huko, hadi akafa; kwa ajili ya damu ya Asaheli, ndugu yake.[#1 Fal 2:5; 2 Sam 20:9,10; Mwa 4:8; 2 Sam 2:23; 4:6]
28Hata baadaye Daudi aliposikia, akasema, Mimi na ufalme wangu hatuna hatia milele mbele za BWANA, kwa sababu ya damu ya Abneri, mwana wa Neri;
29na imwangukie Yoabu kichwani pake, na nyumba yote ya babaye, tena hiyo nyumba ya Yoabu isikose kuwa na mtu mwenye kutoka damu, au aliye na ukoma, au mwenye kutegemea fimbo, au mwenye kuanguka kwa upanga au mwenye kuhitaji chakula.[#Amu 9:54-57; 1 Fal 2:32,33; Zab 7:11,16; 94:22,23; Mit 2:22; 5:22; Law 15:2]
30Basi Yoabu, na Abishai nduguye, walimwua Abneri, kwa sababu yeye alimwua ndugu yao Asaheli katika vita huko Gibeoni.[#2 Sam 2:23]
31Kisha Daudi alimwambia Yoabu, na watu wote waliokuwa pamoja naye, Rarueni nguo zenu, mkajivike nguo za magunia, mkamlilie Abneri. Naye mfalme Daudi akaifuata jeneza.[#2 Sam 1:2,11; Yos 7:6; Amu 11:35; 2 Fal 19:1; Mwa 37:34; Ayu 16:15; Yoe 1:8]
32Wakamzika Abneri katika Hebroni; naye mfalme akapaza sauti yake, akalia kaburini kwa Abneri, nao watu wote wakalia.[#1 Sam 31:4; 2 Sam 1:12; 18:33; Mit 24:17]
33Ndipo mfalme akamwomboleza Abneri, akasema,[#2 Sam 13:13; Mhu 2:15,16]
Ilimpasaje Abneri kufa afavyo mpumbavu?
34Mikono yako haikufungwa,
Wala miguu yako haikutiwa pingu;
Aangukavyo mtu mbele ya wana wa uovu, ndivyo ulivyoanguka.
Na watu wote wakaongeza kumlilia.
35Wakaja na watu wote wamshurutishe Daudi kula chakula, kukiwa bado mchana; lakini Daudi akaapa, akasema Mungu anitendee vivyo hivyo, na kuzidi, nikionja mkate, au kingine chochote kabla ya jua kutua.[#2 Sam 12:17; Yer 16:7; Rut 1:17; 2 Sam 1:12]
36Wakaangalia watu wote, yakawa mema machoni pao; kama yalivyokuwa mema machoni pao yote aliyoyatenda mfalme.
37Wakajua watu wote, na Israeli wote, siku ile, ya kuwa si nia ya mfalme kwamba auawe Abneri, mwana wa Neri.
38Kisha mfalme akawaambia watumishi wake, Hamjui ya kuwa mkuu mmoja, naye ni mtu mkubwa ameanguka leo katika Israeli?
39Nami leo nimedhoofika, hata nijapotiwa mafuta niwe mfalme; na watu hao, wana wa Seruya, ni wagumu kwangu mimi; BWANA amlipie mwovu kulingana na uovu wake.[#2 Sam 19:7,13; 1 Fal 2:5,6,33,34; Zab 28:4; 62:12; 2 Tim 4:14]