The chat will start when you send the first message.
1Basi mitume na ndugu waliokuwako katika Yudea wakapata habari ya kwamba watu wa Mataifa nao wamelipokea neno la Mungu.
2Na Petro alipopanda kwenda Yerusalemu, wale walio wa tohara wakashindana naye,[#Mdo 10:45]
3wakisema, Uliingia kwa watu wasiotahiriwa ukala nao.[#Gal 2:12; Efe 2:11]
4Petro akaanza kuwaeleza kwa taratibu, akasema,
5Nilikuwa katika mji wa Yafa, nikiomba, roho yangu ikazimia, nikaona maono; chombo kinashuka, kama nguo kubwa inateremshwa kutoka mbinguni kwa pembe zake nne, kikanifikia.[#Mdo 10:9-48]
6Nikakitazama sana, nikifikiri, nikaona wanyama wa nchi wenye miguu minne, na wanyama wa mwituni, wale watambaao, na ndege wa angani.
7Nikasikia na sauti ikiniambia, Ondoka, Petro, ukachinje ule.
8Nikasema, Hasha, Bwana, kwa maana kitu kilicho kichafu au kilicho najisi hakijawahi kuingia kinywani mwangu.
9Sauti ikanijibu mara ya pili kutoka mbinguni, Alivyovitakasa Mungu, usivinene wewe najisi.
10Jambo hili likatendeka mara tatu, kisha vitu vyote vikavutwa tena juu mbinguni.
11Na tazama, mara hiyo watu watatu wakasimama mbele ya nyumba tuliyokuwamo, waliotumwa kwangu kutoka Kaisaria.
12Roho akaniambia nifuatane nao, nisione tashwishi. Ndugu hawa sita nao wakaenda pamoja nami, tukaingia katika nyumba ya mtu yule;
13akatueleza jinsi alivyomwona malaika aliyesimama nyumbani mwake na kumwambia, Tuma watu kwenda Yafa ukamwite Simoni aitwaye Petro,
14atakayekuambia maneno ambayo yatakuokoa, wewe na nyumba yako yote.
15Ikawa nilipoanza kunena, Roho Mtakatifu akawashukia kama alivyotushukia sisi mwanzo.
16Nikalikumbuka neno lile la Bwana, jinsi alivyosema, Yohana alibatiza kwa maji kweli, bali ninyi mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu.[#Mdo 1:5]
17Basi ikiwa Mwenyezi Mungu amewapa wao karama ile ile aliyotupa sisi tuliomwamini Bwana Yesu Kristo, mimi ni nani niweze kumpinga Mungu?
18Waliposikia maneno haya wakanyamaza, wakamtukuza Mungu, wakisema, Basi, Mungu amewajalia hata mataifa nao toba liletalo uzima.[#Mdo 13:48; 14:27]
19Basi wale waliotawanyika kwa sababu ya ile dhiki iliyotukia kwa habari ya Stefano, wakasafiri hadi Foinike na Kipro na Antiokia, wasilihubiri lile neno ila kwa Wayahudi peke yao.[#Mdo 8:1-4]
20Lakini baadhi ya hao walikuwa watu wa Kipro na Kirene, nao walipofika Antiokia wakasema na Wayahudi wa Kigiriki, wakihubiri Habari Njema za Bwana Yesu.
21Mkono wa Bwana ukawa pamoja nao, watu wengi wakaamini, wakamwelekea Bwana.[#Mdo 2:47]
22Habari hizo za watu hao zikafika masikioni mwa kanisa lililokuwako katika Yerusalemu; wakamtuma Barnaba, aende hadi Antiokia.[#Mdo 4:36]
23Naye, alipofika na kuiona neema ya Mungu akafurahi, akawasihi wote waambatane na Bwana kwa moyo wote.[#Mdo 13:43]
24Maana alikuwa mtu mwema amejaa Roho Mtakatifu na imani; watu wengi wakaongezeka upande wa Bwana.[#Mdo 5:14; 6:5]
25Kisha akatoka akaenda Tarso kumtafuta Sauli;[#Mdo 9:30]
26hata alipokwisha kumwona akamleta Antiokia. Ikawa kwa muda wa mwaka mzima wakakusanyika pamoja na kanisa na kuwafundisha watu wengi. Na wanafunzi waliitwa Wakristo kwanza hapo Antiokia.[#Gal 2:11; Mdo 26:28; 1 Pet 4:16]
27Siku zizo hizo manabii waliteremka kutoka Yerusalemu hadi Antiokia.[#Mdo 13:1; 15:32]
28Na tulipokusanyika akasimama mmoja wao, jina lake Agabo, akaonesha kwa uweza wa Roho Mtakatifu kwamba njaa kubwa itakuja karibu katika dunia nzima, nayo ikatukia katika siku za Klaudio.[#Mdo 21:10]
29Na wale wanafunzi, kila mtu kwa kadiri ya alivyofanikiwa, wakaazimu kupeleka msaada kwa ndugu zao waliokaa Yudea.[#Gal 2:10]
30Wakafanya hivyo, wakawapelekea wazee kwa mikono ya Barnaba na Sauli.[#Mdo 12:25]