The chat will start when you send the first message.
1Nikauambia moyo wangu, Haya, nitakujaribu kwa njia ya furaha basi ujifurahishe kwa anasa. Na tazama, hayo nayo yakawa ubatili.[#Zab 10:6,11; Lk 12:19; Isa 50:11]
2Nikasema juu ya kicheko, Ni wazimu; na juu ya furaha, Yafaa nini?[#Mit 14:13; Mhu 7:6; Isa 22:12,13; Amo 6:5,6]
3Moyoni mwangu nikapeleleza jinsi ya kuuburudisha mwili kwa mvinyo, na (moyo wangu ungali ukiniongoza kwa hekima) jinsi ya kushikana na upumbavu, hata niyaone yaliyo mema ya kuwafaa wanadamu, ili wayafanye hayo chini ya mbingu siku zote za maisha yao.[#Mhu 1:17; Isa 22:13; Amo 6:3-6; 1 Pet 4:3]
4Nikajifanyia mambo makuu; nikajijengea nyumba; nikajipandia mashamba ya mizabibu;[#1 Fal 10:23-27; 2 Nya 9:22-27]
5nikajifanyia bustani na viunga, na kuipanda humo miti yenye matunda ya kila namna;
6nikajifanyia mabwawa ya maji, ya kuunyweshea msitu mlimopandwa miti michanga.
7Nami nikanunua watumwa na wajakazi, nikawa na watumwa waliozaliwa nyumbani mwangu; tena nikawa na mali nyingi za ng'ombe na kondoo, kuliko wote walionitangulia katika Yerusalemu;[#1 Fal 4:23]
8tena nikajikusanyia fedha na dhahabu, na tunu za kifalme na za kutoka katika majimbo. Nikajipatia waimbaji, wanaume kwa wanawake, nao wale ambao wanadamu wanawatunuka, masuria wengi sana.[#1 Fal 10:10,14-22; 9:28]
9Basi nikawa mkuu, nikaongezeka kupita wote walionitangulia katika Yerusalemu; pia hekima yangu nikakaa nayo.[#1 Nya 29:25; Mhu 1:16]
10Wala sikuyanyima macho yangu chochote yalichokitamani; wala sikuuzuia moyo wangu katika furaha yoyote; maana moyo wangu ulifurahi kwa sababu ya kazi yangu yote, na hii ilikuwa sehemu yangu katika kazi yangu yote.[#Mhu 3:22]
11Kisha nikaziangalia kazi zote zilizofanywa kwa mikono yangu, na taabu yote niliyotaabika katika kuzitenda; na tazama, yote ni ubatili na kufukuza upepo, wala faida hakuna chini ya jua.
12Nikageuka ili kuipambanua hekima, na wazimu na upumbavu. Kwa maana mtu amfuataye mfalme afanye nini? Lilo hilo tu lililokwisha kufanywa.[#Mhu 1:17]
13Ndipo nilipoona ya kuwa kweli hekima hupita upumbavu, kwa kadiri nuru ipitavyo giza;
14macho yake mwenye hekima yamo kichwani mwake, lakini mpumbavu huenda gizani; ila hata hivyo nikatambua ya kwamba ni tukio moja la mwisho liwapatalo wote sawasawa.[#Mhu 8:1; 9:2]
15Nikasema moyoni mwangu, Kama limpatavyo mpumbavu, ndivyo litakavyonipata mimi nami; basi, kwa nini nikawa na hekima zaidi? Nikasema moyoni mwangu ya kuwa hayo nayo ni ubatili.
16Maana hakuna kumbukumbu la milele la mwenye hekima, wala la mpumbavu; kwa sababu siku zijazo wote pia watakuwa wamekwisha kusahauliwa. Na mwenye hekima, jinsi gani anavyokufa sawasawa na mpumbavu!
17Basi, nikauchukia uhai; kwa sababu kazi inayotendeka chini ya jua ilikuwa mbaya kwangu; yaani, mambo yote ni ubatili na kufukuza upepo.
18Nami nikaichukia kazi yangu yote niliyojishughulisha nayo chini ya jua; maana sina budi kumwachia yeye atakayenifuata.[#Zab 49:10]
19Naye ni nani ajuaye kama huyo atakuwa mwenye hekima au mpumbavu? Hata hivyo atatawala juu ya kazi yangu yote niliyojishughulisha nayo, ambamo ndani yake mimi nimeonesha hekima chini ya jua. Hayo nayo ni ubatili.[#1 Fal 12:13; 1 Tim 6:10]
20Kwa hiyo nikageuka kukata tamaa moyoni mwangu juu ya kazi yangu yote niliyojishughulisha nayo chini ya jua.
21Maana kuna mtu ambaye kazi yake ni kwa hekima, na kwa maarifa, na kwa ustadi; naye atamwachia mtu asiyeshughulika nayo kuwa sehemu yake. Hayo tena ni ubatili, nayo ni baa kuu.
22Kwa maana mtu hupata nini kwa kazi yake yote, na kwa juhudi ya moyo wake alivyojitahidi chini ya jua?[#Mhu 1:3]
23Kwa kuwa siku zake zote ni masikitiko, na kazi yake ni huzuni; naam, hata usiku moyoni mwake hamna raha. Hayo nayo ni ubatili.[#Ayu 5:7; 14:1]
24Mwanadamu hapati jema kupita kula na kunywa, na kuiburudisha roho yake kwa mema katika kazi yake. Hayo nayo niliona ya kwamba hutoka mkononi mwa Mungu.[#Mhu 3:13; 5:17; 9:7; Isa 56:12; Lk 12:19; 1 Kor 15:32]
25Kwa maana ni nani awezaye kula au kujiburudisha kuliko mimi?
26Kwa sababu Mungu humpa yeye aliyemridhia hekima na maarifa na furaha; bali mkosaji humpa taabu, ili kukusanya na kututa, apate kumpa huyo ambaye Mungu amridhia. Hayo nayo ni ubatili na kufukuza upepo.[#Ayu 32:8; Mit 2:6]