The chat will start when you send the first message.
1Lisikieni neno la BWANA, enyi wana wa Israeli; kwa maana BWANA ana shutuma nao wakaao katika nchi, kwa sababu hapana kweli, wala fadhili, wala kumjua Mungu katika nchi.[#Mik 6:2; Yer 4:22]
2Hapana neno ila kuapa kwa uongo, na kuvunja ahadi, na kuua, na kuiba, na kuzini; huruka mpaka, na kumwaga damu mfululizo.
3Kwa ajili ya hayo nchi itaomboleza, na kila mtu akaaye ndani yake atadhoofika, pamoja na wanyama wa porini na ndege wa angani; naam, samaki wa baharini pia wataangamizwa.[#Amo 8:8; Sef 1:3]
4Lakini asishindane mtu, wala mtu asikemee; maana watu wako ni kama wao washindanao na kuhani.[#Kum 17:12]
5Na wewe utajikwaa wakati wa mchana, na nabii naye atajikwaa pamoja nawe wakati wa usiku; nami nitamwangamiza mama yako.[#Yer 6:4]
6Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa; kwa kuwa wewe umeyakataa maarifa, mimi nami nitakukataa wewe, usiwe kuhani kwangu mimi; kwa kuwa umeisahau sheria ya Mungu wako, mimi nami nitawasahau watoto wako.
7Kadiri walivyozidishwa, kwa kadiri iyo hiyo walinitenda dhambi; nami nitageuza utukufu wao kuwa aibu.
8Hujilisha dhambi ya watu wangu, hujifurahisha moyo kwa uovu wao.
9Hata itakuwa, kama walivyo watu, ndivyo atakavyokuwa kuhani; nami nitawaadhibu kwa ajili ya njia zao, na kuwalipa kwa matendo yao.
10Nao watakula, lakini hawatashiba; watafanya zinaa, lakini hawataongezeka; kwa sababu wameacha kumwangalia BWANA.[#Mik 6:14; Hag 1:6]
11Uzinzi na divai mpya huondoa fahamu za wanadamu.[#Isa 28:7]
12Watu wangu hutaka shauri kwa kipande cha mti, na fimbo yao huwatolea uaguzi; maana roho ya uzinzi imewapotosha, wakawacha Mungu wao.[#Yer 2:27; Isa 44:20; Ufu 17:2]
13Hutoa dhabihu juu ya vilele vya milima, na kufukiza uvumba juu ya vilima, chini ya mialoni na milibua na miela, kwa kuwa uvuli wake ni mwema; kwa sababu hiyo binti zenu huzini, na bibi arusi zenu hufanya uasherati.[#Ayu 31:9,10; Amo 7:17; Rum 1:28]
14Sitawaadhibu binti zenu wazinipo, wala bibi arusi zenu wafanyapo uasherati; maana wenyewe huenda kando pamoja na wanawake wazinzi, hutoa dhabihu pamoja na makahaba; na watu hawa wasiofahamu wataangamia.
15Ingawa wewe, Israeli, unafanya uzinzi, lakini asiasi Yuda; nanyi msiende Gilgali wala msipande mpaka Beth-aveni, wala msiape mkisema, Aishivyo BWANA.[#Hos 9:15; Amo 4:4; 8:14]
16Kwa maana Israeli ametenda kwa ukaidi, kama ndama mkaidi; sasa je! BWANA atawalisha kama mwana-kondoo katika mahali penye malisho mazuri.[#4:16 Katika Kiebrania ni penye nafasi.]
17Efraimu amejiungamanisha na sanamu; mwache.[#Mit 15:14]
18Kileo chao kimegeuka kuwa uchungu; huzini daima; wakuu wake hupenda aibu.
19Upepo umemfunika kwa mbawa zake; nao watatahayarika kwa sababu ya dhabihu zao.