Waamuzi 13

Waamuzi 13

Kuzaliwa kwa Samsoni

1Wana wa Israeli wakafanya tena yaliyo mabaya mbele za macho ya BWANA, BWANA akawatia katika mikono ya Wafilisti, muda wa miaka arubaini.[#Amu 2:11; 3:7; 4:1; 6:1; 10:6; 1 Sam 12:9]

2Palikuwa na mtu mmoja wa Sora, wa jamaa ya Wadani; jina lake akiitwa Manoa; na mkewe alikuwa tasa, hakuzaa watoto.[#Yos 15:33; 19:41]

3Malaika wa BWANA akamtokea yule mwanamke, akamwambia, Tazama, wewe sasa u tasa, huzai; lakini utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto wa kiume.[#Mwa 16:7-13; 22:16; Kut 3:2-6; Amu 6:12; Hos 12:3-5; Mal 3:1; Lk 1:11,13,28,31; Mdo 7:30]

4Basi sasa, jihadhari, nakuomba, usinywe divai wala kileo, wala usile kitu kilicho najisi;[#Hes 6:2,3; Lk 1:15]

5kwani tazama, utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanamume; na wembe usipite juu ya kichwa chake; maana mtoto huyo atakuwa mnadhiri wa Mungu tangu tumboni; naye ataanza kuwaokoa Israeli na mikono ya Wafilisti.[#Hes 6:1-5; 1 Sam 1:11; 7:13; 2 Sam 8:1; 1 Nya 18:1]

6Ndipo yule mwanamke akaenda akamwambia mume wake, akisema, Mtu wa Mungu alinijia, na uso wake ulikuwa kama uso wa malaika wa Mungu, wa kutisha sana; nami sikumwuliza, Umetoka wapi? Wala hakuniambia jina lake;[#Kum 33:1; 1 Sam 2:27; 9:6; 1 Fal 17:24; Mt 28:3; Lk 9:29; Mdo 6:15]

7lakini aliniambia, Tazama, utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto wa kiume; basi sasa, usinywe divai wala kileo, wala usile kitu kilicho najisi. Maana mtoto huyo atakuwa Mnadhiri wa Mungu tangu tumboni, hadi siku ya kufa kwake.

8Ndipo huyo Manoa akamwomba BWANA, akisema, Ee Bwana, nakuomba, yule mtu wa Mungu uliyemtuma na aje kwetu mara ya pili, atufundishe hayo yatupasayo kumfanyia huyo mtoto atakayezaliwa.

9Mungu akasikia sauti ya Manoa; naye malaika wa Mungu akamwendea yule mwanamke tena alipokuwa anaketi shambani; lakini mumewe, Manoa, hakuwapo pamoja naye.

10Basi huyo mwanamke akaenda haraka, akapiga mbio, na kumwambia mumewe, akisema, Tazama, huyo mtu amenitokea, huyo aliyenijia siku ile.

11Basi Manoa akainuka, akamfuata mkewe, na kumfikia mtu huyo, akamwuliza, Je! Wewe ndiwe mtu yule aliyenena na huyu mwanamke? Akasema, Ndio, ni mimi.

12Manoa akasema, Basi sasa hayo maneno yako yatakapotimia, je! Huyo mtoto atakuwa wa namna gani, na kazi yake itakuwa ni nini?

13Malaika wa Mungu akamwambia Manoa, “Hebu huyo mwanamke ajihadhari na yote niliyomwambia.”

14Asile kitu chochote kitokacho katika mzabibu, wala asinywe divai, wala mvinyo, wala asile kitu chochote kilicho najisi; hayo yote niliyomwamuru na ayatunze.

15Kisha Manoa akamwambia huyo malaika wa BWANA, Nakuomba, tukuzuie, ili tupate kuandaa mwana-mbuzi kwa ajili yako.[#Mwa 18:5; Amu 6:18]

16Lakini malaika wa BWANA akamwambia Manoa, “Ijapokuwa unanizuia, sitakula chakula chako; lakini kama unataka kuandaa sadaka ya kuteketezwa, inakupasa kumsogezea BWANA”. Kwa kuwa Manoa hakujua ya kwamba yeye ni malaika wa BWANA.

17Manoa akamwambia huyo malaika wa BWANA, Jina lako ni nani, ili kwamba hapo hayo maneno yako yatakapotimia nipate kukutukuza?

18Huyo malaika wa BWANA akamwambia, Kwa nini unaniuliza jina langu, na jina hilo ni la ajabu?[#Mwa 32:30; Isa 9:6]

19Basi Manoa akamtwaa yule mwana-mbuzi, pamoja na sadaka ya unga, akamtolea BWANA hapo juu ya mwamba; huyo malaika akatenda la ajabu; Manoa na mkewe wakaangalia.[#Amu 6:19,20; 1 Fal 18:30-38]

20Kwa maana, ikawa, mara huo muali wa moto ulipopaa juu mbinguni kutoka pale madhabahuni, huyo malaika wa BWANA akapaa katika mwali wa moto wa madhabahu; nao Manoa na mkewe wakaangalia; wakaanguka kifudifudi.[#Law 9:24; 1 Nya 21:16; Eze 1:28; Dan 10:9; Hos 12:4,5; Mt 17:6]

21Lakini malaika wa BWANA hakumtokea Manoa tena, wala mkewe. Ndipo Manoa alipojua ya kwamba ndiye malaika wa BWANA.[#Amu 6:22]

22Manoa akamwambia mkewe, Hakika yetu tutakufa sisi, kwa sababu tumemuona Mungu.[#Mwa 32:30; Kut 33:20; Kum 4:3; 5:26; Amu 6:22; Isa 6:5]

23Lakini mkewe akamwambia, Kama BWANA angetaka kutuua hangepokea sadaka ya kuteketezwa, wala sadaka ya unga, mikononi mwetu, wala hangetuonesha mambo hayo yote, wala hangetuambia mambo kama hayo wakati huu.[#Zab 25:14; Mit 3:22; Yn 14:20-23]

24Basi yule mwanamke akamzaa mtoto wa kiume akamwita jina lake Samsoni, mtoto huyu akakua, BWANA akambariki.[#Ebr 11:32; 1 Sam 3:19; Lk 1:80; 2:52]

25Roho ya BWANA ikaanza kumtaharakisha katika Mahane-dani, katikati ya Sora na Eshtaoli.[#Amu 3:10; 6:34; 11:29; 1 Sam 11:6; Mt 4:1; Yn 3:34; Yos 15:33]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya