WaYer 1

WaYer 1

1Kwa sababu ya dhambi zenu mlizozitenda mbele ya Mungu mnachukuliwa mateka Babeli na Nebukadreza, mfalme wa Wababeli.[#Yer 29:1]

Watu kuwa Uhamishoni kwa Muda Mrefu

2Nanyi mtakapofika Babeli mtakaa huko miaka mingi, muda mrefu, hata vizazi saba; na baada yake nitawatoa huko kwa amani.

3Sasa, huko Babeli, mtaona miungu ya fedha na dhahabu na mti ikichukuliwa mabegani, ambayo yawatia mataifa hofu.

4Angalieni basi, msifanane na hao wageni, wala msiingie hofu

5kwa sababu ya miungu hiyo mtakapoona umati wa watu wanaoitangulia na kuifuata wakiiabudu. Bali semeni ninyi mioyoni mwenu; Ee BWANA, lazima yetu ni kukuabudu wewe.

6Maana malaika wangu yupo pamoja nanyi, na yeye mwenyewe anawatunza nafsi zenu.

7Kweli ulimi wake umesuguliwa na fundi, nayo yenyewe imefunikwa dhahabu na fedha, lakini ni miungu ya uongo tu, wala haiwezi kunena.

Miungu Haisaidii chochote

8Naam, hutwaa dhahabu, kama kwa mwali apendaye mapambo, na kufanya taji kwa vichwa vya miungu yao.

9Hata pengine makuhani huiiba dhahabu na fedha ya miungu yao na kujitwalia wenyewe au hata kuwapa makahaba.

10Tena, huipamba miungu ya fedha na dhahabu na mti kwa nguo kana kwamba ni wanadamu; lakini hata hivi haiwezi kujiponya na kutu na nondo,

11ingawa imevikwa nguo za urujuani. Na watu huifuta uso kwa sababu ya vumbi la hekaluni lililoitua kwa wingi.

12Na huo usioweza kumwua mtu aliyeukosa hushika fimbo ya enzi kana kwamba u mwamuzi wa nchi.

13Pia, mkononi mwake mna upanga na shoka, bali hauwezi kujiokoa panapo vita au wanyang'anyi.

14Hivyo mtajua ya kuwa siyo miungu; basi msiigope.

15Na kama chombo kitumikacho na watu hakina faida yoyote kilipovunjika, ndivyo ilivyo miungu yao; iliposimamishwa hekaluni

16macho yake hujaa vumbi kwa miguu ya watu waingiao.

17Na kama vile uwanda ufungwavyo imara ambamo amefungiwa mtu aliyemwasi mfalme akahukumiwa kufa, ndivyo makuhani wayafungavyo mahekalu yao kwa milango na makufuli, na makomeo, ili miungu isichukuliwe na wanyang'anyi.

18Huiwashia taa nyingi kuliko wazitumiazo wenyewe, ingawa haiwezi kuona hata moja.

19I sawasawa na boriti za hekalu, wadudu watokao ardhini huila pamoja na mavazi yake, na watu husema mioyo yao imeliwa!

20Inapotiwa masizi usoni kwa moshi utokao hekaluni haioni kitu;

21na juu ya vichwa vyake hutua popo, mbayuwayu, na ndege, hata paka pia.

22Hivyo mtajua ya kuwa siyo miungu, basi msiiogope.

23Ijapokuwa imepambwa dhahabu ipate kupendeza, lakini mtu asipoifuta kutu haitang'aa, maana haijui inapoingia uchafu.

24Vitu visivyo na pumzi hununuliwa, hata kwa bei kubwa sana!

25Huchukuliwa mabegani kwa sababu haina miguu; na hivyo hudhihirisha watu ya kuwa haiwezi kitu. Wao pia waitumikiao hutahayarika, maana kama wakati wowote ikianguka chini haiwezi kujiinua yenyewe;

26wala mtu akiisimamisha haiwezi kusogea; au, kama ikiwekwa pogo, haiwezi kujisawazisha. Hata hivyo, hutolewa dhabihu, kama wafu watolewavyo.

27Na vile vitu vilivyotolewa sadaka makuhani huviuza na kuvitumia, na wake zao kadhalika huitia nyama chumvi na kuiweka akiba. Bali maskini na wanyonge hawapewi kitu chochote. Mwanamke aliyeingia mwezini, na mwanamke aliyejifungua, huzigusa dhabihu zake.

28Basi, kwa hayo mtajua ya kuwa siyo miungu; kwa hiyo msiogope.

29Yawezaje kuitwa miungu, madhali hata wanawake huweka nyama mbele ya miungu ya fedha na dhahabu na mti?

30Na hekaluni makuhani huketi katika viti, wamerarua nguo zao na kunyoa vichwa vyao na ndevu zao, na kuacha wazi vichwa vyao.

31Huomboleza na kulia mbele ya miungu yao, kama watu wafanyavyo kwenye kilio.

32Pamoja na hayo, makuhani huivua nguo ili kuvika wake zao na watoto wao.

33Kama ikitendwa mabaya au kama ikitendwa mema, haiwezi kulipa; haiwezi kusimamisha mfalme wala kumshusha.

34Kadhalika, haiwezi kutoa utajiri au umaskini; mtu akiiwekea nadhiri asiitimize haitaitaka kwake kamwe.

35Haiwezi kumponya mtu na mauti, wala kumwokoa mnyonge mikononi mwa mwenye nguvu.

36Haiwezi kufanya kipofu aone tena, wala kuponya mtu aliye katika shida.

37Haiwezi kuhurumia mjane wala kufadhili yatima.

38Vyafanana na mawe yaliyochongwa katika mlima, hivi vitu vya mti vilivyofunikwa dhahabu na fedha; nao wavihudumiao watafedheheshwa.

39Basi, yawezaje mtu kudhani au kusema kwamba ni miungu, madhali hata Wakaldayo wenyewe huidharau?

Upumbavu wa Kuabudu Sanamu

40Ambao, wakimwona mtu bubu asiyeweza kusema, humleta na kumtaka amlilie Beli, kana kwamba ni mungu awezaye kufahamu?

41Lakini wao wenyewe hawawezi kutambua hayo yote na kuiacha miungu hiyo, kwa sababu hawana akili.[#Isa 46:1]

42Wanawake kuketi njiani, wamejifunga kamba, wakifukuza makapi badala ya uvumba;

43na kama mmoja wao akivutwa na mtu apitaye, na kulala naye, humdhihaki mwenzake kwa kuwa hakustahilishwa kama yeye mwenyewe, wala kamba yake haikuvunjwa.

44Kila litendwalo juu yake ni la uongo, basi, awezaje mtu kudhani au kusema kwamba i miungu?

45Hufanyizwa na seremala au sonara; haiwezi kutokea kitu kingine ila kile kilichoazimiwa nao.

46Na hao walioifanyiza hawakai miaka mingi; vitakaaje, basi, vitu vilivyofanyizwa nao?

47Hakika wamewaachia watakaowafuata vitu vya uongo na lawama.

48Maana wakipatwa na vita au baa, makuhani hushauriana juu ya mahali pa kujificha pamoja nayo.

49Basi, imekuwaje watu hawatambui ya kuwa hiyo siyo miungu, ambayo haiwezi kujiponya na vita au baa?

50Basi, kwa kuwa ni ya mti tu na kufunikwa dhahabu na fedha, itajulikana halafu kuwa ni ya uongo, hata itakuwa dhahiri kwa mataifa yote na wafalme kama hiyo si miungu ila ni kazi ya mikono ya wanadamu, wala hamna kazi ya Mungu ndani yake.

51Ni nani, basi, asiyeweza kuijua ya kuwa si miungu?

52Madhali haiwezi kusimamisha mfalme katika nchi, wala kuwapa watu mvua.

53Wala haiwezi kujitetea yenyewe, wala kumponya aliyeonewa, maana haina uwezo; hufanana na kunguru kati ya mbingu na nchi.

54Maana, kama mtoto ukiiangukia nyumba ya miungu ya mti, au iliyofunikwa dhahabu au fedha, makuhani wake watakimbia na kujiokoa, bali hiyo yenyewe itateketea kama boriti.

55Zaidi ya hayo, hawezi kushindana na mfalme au adui;

56Basi, mtu awezaje kuikubali au kuidhania kuwa ni miungu?

57Tena, miungu hiyo ya mti, iliyofunikwa fedha au dhahabu, haiwezi kujiepusha na wezi au wanyang'anyi. Wenye nguvu watainyang'anya dhahabu yake na fedha, na nguo ilizovikwa, na kwenda nazo, wala haitaweza kujisaidia.

58Kwa hiyo ni afadhali kuwa mfalme aoneshaye utu wake, au chombo cha nyumbani kifaacho kwa matumizi ya mwenyewe, kuliko kuwa miungu ya uongo kama hiyo. Hata mlango wa nyumba ulindao vitu vya nyumbani hafaa kuliko hiyo miungu ya uongo; au nguzo ya mti katika nyumba kuu kuliko hiyo miungu ya uongo.

59Maana jua na mwezi na nyota zitoazo nuru na kutumwa kufanya kazi zake zinatii.

60Nao umeme unapomeremeta hupendeza macho; na kadhalika upepo huvuma kila mahali.

61Tena, Mungu anapoyaamuru mawingu yapite juu ya dunia yote, hufanya yalivyoagizwa. Na moto upelekwao kutoka juu kuiteketeza milima na misitu, hufanya ulivyoamriwa.

62Bali hiyo haiwezi kufananishwa na viumbe hivyo kwa uzuri wala kwa uwezo.

63Kwa sababu hiyo haimpasi mtu kudhani wala kusema kwamba ni miungu, madhali haiwezi kuamua mashauri wala kuwafaa watu.

64Basi, kwa kuwa mnajua kama hiyo si miungu msiiogope.

65Mradi haiwezi kulaani wafalme wala kuwabariki;

66haiwezi kuonesha ishara mbinguni katikati ya mataifa, wala kung'aa kama jua au kuitoa nuru kama mwezi.

67Bora wanyama kuliko hiyo, maana wao waweza kujificha kichakani na kujisaidia.

68Bali hatuoni dalili yoyote ya kuonesha kama hiyo ni miungu; basi, msiiogope.

69Kama mti mkavu katika shamba la matango, ambao haulindi kitu, ndivyo ilivyo miungu yao ya mti, na iliyofunikwa dhahabu na fedha.

70Au, kwa mfano mwingine, inafanana na mchongoma wa shambani ambao kila ndege kuutua, au mzoga uliotupwa nje gizani.

71Basi, kwa urujuani na kitani safi inayooza juu yake, ninyi mtaijua kuwa si miungu, na halafu hiyo yenyewe itaoza na kuwa lawama katika nchi.

72Basi, afadhali mtu wa haki asiye na sanamu, maana yeye atakuwa mbali na lawama.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya