Hesabu 2

Hesabu 2

Amri ya kupiga kambi na kuingia

1BWANA akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia,

2Wana wa Israeli watapanga kila mtu penye bendera yake mwenyewe, na alama za nyumba za baba zao; kuikabili hema ya kukutania ndiko watakakopanga kwa kuizunguka pande zote.[#Hes 1:52; 24:2-9]

3Na hao watakaopanga upande wa mashariki, kwa kuelekea maawio ya jua, ndio wale wa bendera ya kambi ya Yuda, kwa majeshi yao; na mkuu wa wana wa Yuda atakuwa Nashoni mwana wa Aminadabu.[#Hes 10:14; Rut 4:20; 1 Nya 2:10; Mt 1:4; Lk 3:32,33]

4Na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa elfu sabini na nne na mia sita.

5Na hao watakaopanga karibu naye ni kabila la Isakari; na mkuu wa wana wa Isakari atakuwa Nethaneli mwana wa Suari;[#Hes 7:18,23]

6na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa elfu hamsini na nne na mia nne;[#Hes 26:25]

7na kabila la Zabuloni; na mkuu wa wana wa Zabuloni atakuwa Eliabu mwana wa Heloni;[#Mwa 49:13; Kum 33:18]

8na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa elfu hamsini na saba na mia nne.

9Hao wote waliohesabiwa katika kambi ya Yuda walikuwa elfu mia moja themanini na sita na mia nne, kwa makundi yao. Hao ndio watakaotangulia mbele.[#Hes 10:14; 1 Nya 5:2; Zab 78:52]

10Upande wa kusini kutakuwa na bendera ya kambi ya Reubeni kwa majeshi yao; na mkuu wa wana wa Reubeni atakuwa Elisuri mwana wa Shedeuri.[#Kum 33:6; 1 Nya 5:1]

11Na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa elfu arubaini na sita na mia tano.

12Na hao watakaopanga karibu naye ni kabila la Simeoni; na mkuu wa wana wa Simeoni atakuwa Shelumieli mwana wa Suri-shadai;

13na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa elfu hamsini na tisa na mia tatu;

14na kabila la Gadi; na mkuu wa wana wa Gadi atakuwa Eliasafu mwana wa Deueli;

15na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa elfu arubaini na tano, mia sita na hamsini.

16Wote waliohesabiwa katika kambi za Reubeni walikuwa elfu mia moja hamsini na moja na mia nne na hamsini, kwa majeshi yao. Nao ndio watakaofuata wakiwa kundi la pili.[#Hes 10:18; Mwa 49:3; 1 Nya 5:1]

17Ndipo hema ya kukutania itasafiri, pamoja na kambi za Walawi katikati ya kambi zote; kama wapangavyo kambi, watasafiri vivyo hivyo, kila mtu mahali pake, penye bendera zao.[#Mdo 7:44; Ebr 8:2; 1 Kor 14:40]

18Upande wa magharibi kutakuwa na bendera ya kambi ya Efraimu kwa majeshi yao; na mkuu wa wana wa Efraimu atakuwa Elishama mwana wa Amihudi.[#Mwa 48:14-20; Zab 80:1; Hos 11:3]

19Na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao walikuwa elfu arubaini na mia tano.

20Na karibu naye itakuwa kabila la Manase; na mkuu wa wana wa Manase atakuwa Gamalieli mwana wa Pedasuri;

21na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa elfu thelathini na mbili na mia mbili;

22tena kabila la Benyamini; na mkuu wa wana wa Benyamini atakuwa Abidani mwana wa Gideoni;[#Zab 68:27; Ufu 7:8]

23na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa elfu thelathini na tano na mia nne.

24Wote waliohesabiwa katika kambi ya Efraimu walikuwa elfu mia moja na nane na mia moja, kwa majeshi yao. Nao ndio watakaoondoka wakiwa kundi la tatu.[#Hes 10:22]

25Upande wa kaskazini kutakuwa na bendera ya kambi ya Dani kwa majeshi yao; na mkuu wa wana wa Dani atakuwa Ahiezeri mwana wa Amishadai.[#Kum 32:22]

26Na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa elfu sitini na mbili na mia saba.

27Na hao watakaopanga karibu naye ni kabila la Asheri; na mkuu wa wana wa Asheri atakuwa Pagieli mwana wa Okrani;

28na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa elfu arubaini na moja na mia tano;

29kisha kabila la Naftali; na mkuu wa wana wa Naftali atakuwa Ahira mwana wa Enani;[#Mwa 30:8; 49:21; 2 Fal 15:29; Ufu 7:6]

30na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa elfu hamsini na tatu na mia nne.

31Wote waliohesabiwa katika kambi ya Dani walikuwa elfu mia moja hamsini na saba na mia sita. Hao ndio watakaoondoka mwisho kwa kufuata bendera yao.[#Hes 10:25; #2:31 Katika Kiebrania ni ‘kufuata vikosi vyao’.]

32Hao ndio waliohesabiwa katika wana wa Israeli kwa nyumba za baba zao; wote waliohesabiwa katika kambi kwa majeshi yao, walikuwa elfu mia sita na tatu na mia tano na hamsini.[#Kut 12:37; 38:26; Hes 1:46; 11:21]

33Lakini Walawi hawakuhesabiwa katika wana wa Israeli; kama BWANA alivyomwagiza Musa.[#Hes 1:47; 26:57-62]

34Hivyo ndivyo walivyofanya wana wa Israeli; kama BWANA alivyomwamuru Musa; ndivyo walivyojipanga kufuata bendera zao, na ndivyo walivyosafiri, kila mtu kwa jamaa zao, kwa nyumba za baba zao.[#Kut 39:42; Hes 24:2,9; Zab 119:6; Isa 45:12; Lk 1:6; 1 Kor 14:40]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya