Zaburi 21

Zaburi 21

Shukrani kwa ushindi

1Ee BWANA, mfalme atazifurahia nguvu zako,

Na wokovu wako ataufanyia shangwe nyingi sana.

2Umempa haja ya moyo wake,[#Yn 11:42]

Wala hukumzuilia matakwa ya midomo yake.

3Maana umemsogezea baraka za heri,

Umemvika taji la dhahabu safi kichwani pake.

4Alikuomba uhai, ukampa,[#2 Sam 7:19]

Muda mrefu wa siku nyingi, milele na milele.

5Utukufu wake ni mkuu kwa wokovu wako,

Heshima na adhama waweka juu yake.

6Maana umemfanya kuwa baraka za milele,

Wamfurahisha kwa furaha ya uso wako.

7Kwa kuwa mfalme humtumainia BWANA,[#Zab 91:2]

Na kwa fadhili zake Aliye Juu hatatikisika.

8Mkono wako utawapata adui zako wote,

Mkono wako wa kulia utawapata wanaokuchukia.

9Utawafanya kuwa kama tanuri ya moto,[#Kum 32:22]

Wakati wa ghadhabu yako.

BWANA atawameza kwa ghadhabu yake,

Na moto utawateketeza.

10Matunda yao utayaharibu na kuyaondoa katika nchi,

Na wazao wao katika wanadamu.

11Wakipanga kukutenda mabaya,

Kwa miango ya hila, hawatafanikiwa.

12Kwa maana utawatimua utawafanya wakimbie,

Kwa upote wa uta wako utazilenga nyuso zao.

13Ee BWANA, utukuzwe kwa nguvu zako,[#Ufu 15:3,4]

Nasi tutaimba na kuuhimidi uwezo wako.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya