Zaburi 57

Zaburi 57

Sifa na hakikisho katika mateso

1Unirehemu, Ee Mungu, unirehemu mimi,[#Isa 26:20]

Maana nafsi yangu imekukimbilia Wewe.

Nitaukimbilia uvuli wa mbawa zako,

Hadi misiba hii itakapopita.

2Nitamwita MUNGU Aliye Juu,[#Zab 138:8]

Mungu anitimiziaye mambo yangu.

3Atanitumia msaada toka mbinguni na kuniokoa,[#Zab 144:5; 40:11]

Atawaaibisha wale wanaotaka kunishambulia.

Mungu atazituma

Fadhili zake na kweli yake.

4Nafsi yangu i kati ya simba,[#Mit 30:14; Zab 64:3]

Nitastarehe kati yao waliowaka moto.

Wanadamu meno yao ni mikuki na mishale,

Na ndimi zao ni upanga mkali.

5Ee Mungu, utukuzwe juu ya mbingu,[#Zab 108:5]

Na juu ya nchi yote uwe utukufu wako.

6Wameweka wavu ili kuninasa miguu;[#Zab 9:15]

Nimevunjika moyo;

Wamechimba shimo njiani mwangu;

Lakini wao wenyewe wametumbukia humo!

7Ee Mungu, moyo wangu ni thabiti,[#Zab 108:1]

Moyo wangu ni thabiti.

Nitaimba, nitaimba kwa sauti nzuri,

8Amka, ee moyo wangu.[#Amu 5:12]

Amka, kinanda na kinubi,

Nitaamka alfajiri.

9Ee Bwana, nitakushukuru kati ya watu,

Nitakuimbia sifa kati ya mataifa.

10Maana fadhili zako ni kubwa hata mbinguni,[#Zab 108:4]

Na uaminifu wako hata mawinguni.

11Ee Mungu, utukuzwe juu ya mbingu,

Na juu ya nchi yote uwe utukufu wako.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya