Hekima ya Sulemani 6

Hekima ya Sulemani 6

ASILI, TABIA NA KAZI YA HEKIMA. NJIA ZA KUJIPATIA HEKIMA

Wafalme watafute hekima

1Hekima ndiyo bora kupita nguvu,

Na mwenye busara kuliko shujaa.

Basi, enyi wafalme, sikilizeni; enyi waamuzi wa miisho ya dunia jifunzeni;

2sikieni ninyi mtawalao watu wengi, na kujisifia umati wa mataifa.

3Kwa maana mlipewa falme zenu na BWANA, na milki zenu na Aliye Juu ambaye atazichunguza kazi zenu, na kuyahojihoji mashauri yenu;[#Rum 13:1]

4kwa sababu, kisha kuwa wakuu wa ufalme wake, hamhukumu kwa adili, wala kuishika torati, wala kulifuata shauri la Mungu.

5Yeye atawajia ghafla kwa kitisho, madhali hukumu bila huruma huwaangukia wenye cheo;

6mradi mtu mnyonge aweza kusamehewa katika rehema, bali wakuu watakabiliwa na hukumu hasa.

7Kwa kuwa BWANA, Mfalme wa wote, hatajizuia kwa ajili ya mtu yeyote, wala hajali ukuu, kwa sababu ndiye Yeye aliyewafanya wadogo na wakuu pia.

8Naye huwazingatia watu wote pasipo upendeleo. Walakini uchunguzi ulio halisi huwajilia wenye uwezo.

9Kwa hiyo, enyi wafalme, nawaambia ninyi maneno yangu, ili mjifunze hekima, msije mkapotea njiani.

10Maana wale waliotunza kwa utakatifu mambo yale yaliyo matakatifu watahesabiwa kuwa watakatifu wenyewe; nao wale waliofundishwa hayo wataona neno la kujiteta.

11Basi fanyeni shauku ya maneno yangu; yatafuteni, na kwa malezi yake mtapata adabu.

Maelezo juu ya Hekima

12Hekima hung'aa, wala hafifii;

Huonekana upesi nao wampendao.

Hupatikana nao wamtafutao.

13Hutangulia kujionesha kwao wamtakao,

14Amtafutaye mapema hana kazi ngumu;

Atamkuta ameketi mlangoni pake.

15Kumtia fikirani ni ufahamu mkamilifu;

Naye mwenye kukesha kwa ajili yake

Atakuwa mara hana masumbufu.

16Yeye huzunguka zunguka mwenyewe,

Akiwatafuta wao wanaomstahili;

Njiani hujidhihirisha kwao kwa upendo.

Hukutana nao katika kila kusudi;

17Mwanzo wake hasa ni kutaka malezi;

Na kuangalia malezi ni kumpenda.

18Kumpenda ni kuzishika sheria zake

Kuzitii sheria zake ni kuuimarisha unyofu;

19Na unyofu hutuleta karibu na Mungu.

20Basi kutaka Hekima huwaongoza watu wapate kumiliki.

21Nanyi, enyi wafalme wa watu, ikiwa mnapendezwa na viti vya enzi na fimbo za enzi, heshimuni Hekima mpate kumiliki milele.

Sulemani aeleza maana ya Hekima

22Lakini mimi nitawajulisha Hekima, asili yake na chanzo chake ni nini, wala sitawaficheni siri zake; bali kutokea awali ya kuumbwa ulimwengu nitatafuta habari zake, na kuzidhihirisha kwa wazi, bila kuyaepuka yaliyo kweli.

23Lakini mimi sitachukua husuda yenye kununa kuwa mwenzangu njiani, kwa maana husuda haina urafiki na Hekima;

24lakini wingi wa wenye hekima ni wokovu kwa ulimwengu, na mfalme mwenye ufahamu huwaletea watu wake raha.

25Kwa hiyo ninyi mpate malezi kwa maneno yangu, na hivyo mtafaidiwa pia.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya