The chat will start when you send the first message.
1Lakini Sauli, akizidi kutisha na kuwaza kuwaua wanafunzi wa Bwana, akamwendea Kuhani Mkuu,[#Mdo 22:3-21; 26:9-20; #Mdo 8:3]
2akataka ampe barua za kuenda Dameski zilizoandikwa kwa masinagogi, ili akiona watu wa Njia hii, waume kwa wake, awafunge na kuwaleta Yerusalemu.
3Hata alipokuwa akisafiri, ikawa anakaribia Dameski; ghafula ikamwangaza kote kote nuru kutoka mbinguni.[#1 Kor 15:8]
4Akaanguka chini, akasikia sauti ikimwambia, Sauli, Sauli, mbona waniudhi?
5Akasema, U nani wewe, Bwana? Naye akasema, Mimi ndimi Yesu unayeniudhi wewe.[#Mdo 5:39]
6Lakini simama, uingie mjini, nawe utaambiwa yakupasayo kutenda.
7Na wale watu waliosafiri pamoja naye wakasimama kimya, wakiisikia sauti, wasione mtu.
8Sauli akainuka katika nchi, na macho yake yalipofumbuka, hakuona kitu; wakamshika mkono wakamleta mpaka Dameski.
9Akawa siku tatu haoni; hali, wala hanywi.
10Basi palikuwapo Dameski mwanafunzi jina lake Anania. Bwana akamwambia katika maono, Anania. Akasema, Mimi hapa, Bwana.[#Mdo 10:17; 16:9]
11Bwana akamwambia, Simama, enenda zako katika njia iitwayo Nyofu, ukaulize katika nyumba ya Yuda mtu aitwaye Sauli, wa Tarso; maana, angalia, anaomba;[#Mdo 21:39]
12naye amemwona mtu, jina lake Anania, akiingia, na kumwekea mikono juu yake, apate kuona tena.
13Lakini Anania akajibu, Bwana, nimesikia habari za mtu huyu kwa watu wengi, mabaya mengi aliyowatenda watakatifu wako Yerusalemu;
14hata hapa ana amri itokayo kwa wakuu wa makuhani awafunge wote wakuitiao Jina lako.[#1 Kor 1:2; Mdo 22:16; 2 Tim 2:22]
15Lakini Bwana akamwambia, Nenda tu; kwa maana huyu ni chombo kiteule kwangu, alichukue Jina langu mbele ya Mataifa, na wafalme, na wana wa Israeli.[#Rum 1:5; Mdo 25:13; 27:24; 2 Kor 4:7]
16Maana nitamwonyesha yalivyo mengi yatakayompasa kuteswa kwa ajili ya Jina langu.[#Mdo 23:29; 2 Kor 11:23-28]
17Anania akaenda zake, akaingia mle nyumbani; akamwekea mikono akisema, Ndugu Sauli, Bwana amenituma, Yesu, yeye aliyekutokea katika njia uliyoijia, upate kuona tena, ukajazwe Roho Mtakatifu.
18Mara vikaanguka machoni pake vitu kama magamba, akapata kuona, akasimama, akabatizwa;
19akala chakula, na kupata nguvu.
Akawa huko siku kadha wa kadha pamoja na wanafunzi walioko Dameski.
20Mara akamhubiri Yesu katika masinagogi, kwamba yeye ni Mwana wa Mungu.
21Na wote waliosikia wakashangaa, wakasema, Siye huyu aliyewaharibu walioliitia Jina hili huko Yerusalemu? Na hapa alikuwa amekuja kwa kusudi hilo, awafunge na kuwapeleka kwa wakuu wa makuhani?[#Mdo 8:1; 9:1,14; 26:10]
22Sauli akazidi kuwa hodari, akawatia fadhaa Wayahudi waliokaa Dameski, akithibitisha ya kuwa huyu ndiye Kristo.[#Mdo 18:28]
23Hata siku nyingi zilipopita, Wayahudi wakafanya shauri ili wamwue;[#2 Kor 11:32-33; #Mdo 23:12-29]
24lakini hila yao ikajulikana na Sauli. Wakamvizia malangoni mchana na usiku wapate kumwua.[#Mdo 23:16]
25Wanafunzi wake wakamtwaa usiku wakamshusha ukutani, wakimtelemsha katika kapu.
26Na Sauli alipofika Yerusalemu, alijaribu kujiunga na wanafunzi, nao walikuwa wakimwogopa wote, wasisadiki ya kuwa yeye ni mwanafunzi.[#Gal 1:17-19]
27Lakini Barnaba akamtwaa, akampeleka kwa mitume, akawaeleza jinsi alivyomwona Bwana njiani, na ya kwamba alisema naye, na jinsi alivyohubiri kwa ushujaa katika Dameski kwa jina la Yesu.[#Mdo 9:20]
28Naye akawa pamoja nao katika Yerusalemu akiingia na kutoka.
29Akahubiri kwa jina la Bwana kwa ushujaa, akinena na kuhojiana na Wayahudi wa Kiyunani. Nao wakajaribu kumwua.
30Lakini ndugu walipopata habari wakamchukua mpaka Kaisaria, wakampeleka aende Tarso.[#Mdo 11:25; Gal 1:21]
31Basi kanisa likapata raha katika Uyahudi wote na Galilaya na Samaria, likajengwa, likiendelea na kuongezeka katika kicho cha Bwana, na faraja ya Roho Mtakatifu.
32Hata Petro alipokuwa akizunguka-zunguka pande zote akawatelemkia na watakatifu waliokaa Lida.
33Akamwona mtu mmoja huko, jina lake Ainea, mtu huyo amelala kitandani miaka minane; maana alikuwa amepooza.
34Petro akamwambia, Ainea, Yesu Kristo akuponya; ondoka, ujitandikie. Mara akaondoka.
35Na watu wote waliokaa Lida na Sharoni wakamwona, wakamgeukia Bwana.
36Na mwanafunzi mmoja alikuwako Yafa, jina lake Tabitha, tafsiri yake ni Dorkasi (yaani paa); mwanamke huyu alikuwa amejaa matendo mema na sadaka alizozitoa.
37Ikawa siku zile akaugua, akafa; hata walipokwisha kumwosha, wakamweka orofani.
38Na kwa kuwa mji wa Lida ulikuwa karibu na Yafa, nao wanafunzi wamesikia ya kwamba Petro yuko huko, wakatuma watu wawili kwake, kumsihi na kusema, Usikawie kuja kwetu.
39Petro akaondoka akafuatana nao. Alipofika, wakampeleka juu orofani wajane wote wakasimama karibu naye, wakilia na kumwonyesha zile kanzu na nguo alizozishona Dorkasi wakati ule alipokuwa pamoja nao.
40Petro akawatoa nje wote, akapiga magoti, akaomba, kisha akaelekea yule maiti, akanena, Tabitha, ondoka. Naye akafumbua macho yake, na alipomwona Petro akajiinua, akaketi.[#Mk 5:40,41]
41Akampa mkono, akamwinua; hata akiisha kuwaita wale watakatifu na wajane akamweka mbele yao, hali yu hai.[#Mdo 9:32]
42Ikajulikana katika mji mzima wa Yafa; watu wengi wakamwamini Bwana.
43Basi Petro akakaa siku kadha wa kadha huko Yafa, nyumbani mwa mtu mmoja, jina lake Simoni, mtengenezaji wa ngozi.[#Mdo 10:6]