The chat will start when you send the first message.
1Basi, ndugu zangu, wapendwa wangu, ninaowaonea shauku, furaha yangu, na taji yangu, hivyo simameni imara katika Bwana, wapenzi wangu.[#2 Kor 1:14; 1 The 2:19,20]
2Namsihi Euodia, namsihi na Sintike, wawe na nia moja katika Bwana.
3Naam, nataka na wewe pia, mjoli wa kweli, uwasaidie wanawake hao; kwa maana waliishindania Injili pamoja nami, na Klementi naye, na wale wengine waliotenda kazi pamoja nami, ambao majina yao yamo katika kitabu cha uzima.[#Zab 69:28; Lk 10:20]
4Furahini katika Bwana sikuzote; tena nasema, Furahini.[#Flp 3:1; 2 Kor 13:11]
5Upole wenu na ujulikane na watu wote. Bwana yu karibu.[#Ebr 10:37; Yak 5:8,9]
6Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu.[#Mt 6:25-34; Kol 4:2; 1 Pet 5:7; Zab 145:18; Yn 14:27]
7Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.[#Kol 3:15]
8Hatimaye, ndugu zangu, mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote yenye kupendeza, yo yote yenye sifa njema; ukiwapo wema wo wote, ikiwapo sifa nzuri yo yote, yatafakarini hayo.[#Rum 12:17]
9Mambo mliyojifunza kwangu na kuyapokea, na kuyasikia na kuyaona kwangu, yatendeni hayo; na Mungu wa amani atakuwa pamoja nanyi.[#1 The 5:23; Rum 16:20; 1 Kor 14:33]
10Nalifurahi sana katika Bwana, kwa kuwa sasa mwisho mmehuisha tena fikira zenu kwa ajili yangu, kama vile mlivyokuwa mkinifikiri hali yangu lakini hamkupata nafasi.
11Si kwamba nasema haya kwa kuwa nina mahitaji; maana nimejifunza kuwa radhi na hali yo yote niliyo nayo.[#1 Tim 6:6]
12Najua kudhiliwa, tena najua kufanikiwa; katika hali yo yote, na katika mambo yo yote, nimefundishwa kushiba na kuona njaa, kuwa na vingi na kupungukiwa.[#2 Kor 6:10]
13Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.[#2 Kor 12:10; 2 Tim 4:17]
14Lakini mlifanya vema, mliposhiriki nami katika dhiki yangu.
15Nanyi pia, ninyi wenyewe mnajua, enyi Wafilipi, ya kuwa katika mwanzo wa Injili, nilipotoka Makedonia, hakuna kanisa lingine lililoshirikiana nami katika habari hii ya kutoa na kupokea, ila ninyi peke yenu.[#2 Kor 11:9]
16Kwa kuwa hata huko Thesalonike mliniletea msaada kwa mahitaji yangu, wala si mara moja.[#Mdo 17:1]
17Si kwamba nakitamani kile kipawa, bali nayatamani mazao yanayozidi kuwa mengi, katika hesabu yenu.[#1 Kor 9:11]
18Lakini ninavyo vitu vyote na kuzidi, tena nimejaa tele; nimepokea kwa mkono wa Epafrodito vitu vile vilivyotoka kwenu, harufu ya manukato, sadaka yenye kibali, impendezayo Mungu.[#Kut 29:18; Eze 20:41; Flp 2:25]
19Na Mungu wangu atawajazeni kila mnachokihitaji kwa kadiri ya utajiri wake, katika utukufu, ndani ya Kristo Yesu.
20Sasa atukuzwe Mungu, Baba yetu, milele na milele. Amina.
21Mnisalimie kila mtakatifu katika Kristo Yesu. Ndugu walio pamoja nami wawasalimu.
22Watakatifu wote wawasalimu, hasa wao walio wa nyumbani mwa Kaisari.[#Flp 1:13]
23Neema ya Bwana Yesu Kristo na iwe pamoja na roho zenu.