Matendo 18

Matendo 18

1BAADA ya mambo haya Paolo akatoka Athene akalika Korintho.

2Akamwona Myahudi mmoja, jina lake Akula, mzalia wa Ponto; nae amekuja kutoka inchi ya italia siku za karibu, pamoja na Priskilla mkewe, kwa sababu Klaudio amewaamuru Wayahudi wote watoke Rumi.

3Akafika kwao; na kwa kuwa kazi yake na kazi yao ni moja, akakaa kwao, akafanya kazi yake, kwa maana walikuwa mafundi wa kufanyiza khema.

4Akatoa hoja zake katika sunagogi killa sabato akawavuta Wayahudi na Wayunani waamini.

5Hatta Sila na Timotheo walipotelemka kutoka Makedonia, Paolo akashurutishwa rohoni mwake, akiwashuhudia Wayahudi ya kwamba Yesu ni Kristo.

6Walipopingamana nae na kutukana, akakungʼuta mavazi yake, akawaambia, Damu yenu na iwe juu ya vichwa vyenu: mimi ni safi: langu sasa nitakwenda kwa watu wa mataifa.

7Akaondoka huko akaingia katika nyumba ya mtu mmoja jina lake Yusto, mcha Mungu, ambae nyumba yake ilikuwa mpaka mmoja na sunagogi.

8Na Krispo, mkuu wa sunagogi, akamwamini Bwana pamoja na nyumba yake yote. Wakorintho wengi wakasikia, wakaamini, wakabatizwa.

9Bwana akamwambia Paolo kwa njozi nsiku, Usiogope, bali nena, wala usinyamaze,

10kwa kuwa mimi ni pamoja nawe, wala hapana mtu atakaekushambulia illi kukudhuru; kwa matina mimi nina watu wengi katika mji huu.

11Akakaa huko muda wa mwaka mmoja na miezi sita akawafundisha neno la Mungu.

12Hatta Gallio alipokuwa Prokonsuli wa Akaya, Wayahudi wakamwendea Paolo kwa nia moja, wakamleta mbele ya kiti cha hukumu,

13wakisema, Mtu huyu huwavuta watu illi wamwabudu Mungu kinyume cha sharia yetu.

14Na Paolo alipotaka kufunua kinywa chake, Gallio akawaambia Wayahudi, Kama lingetendeka tendo la dhuluma au la hila mbaya, enyi Wayahudi, ingekuwa haki kuchukuliana nanyi;

15bali ikiwa ni hoja juu ya maneno na majina na sharia yenu, liangalieni ninyi wenyewe, maana mimi sitaki kuwa mwamuzi wa mambo hayo.

16Akawafukuza mbele ya kiti cha hukumu.

17Na Wayunani wote wakamshika Sosthene, mkuu wa sunagogi, wakampiga mbele ya kiti cha hukumu. Na Gallio hakuyaona mambo hayo kuwa kitu.

18Paolo akazidi kukaa huko siku nyingi, kiisha akaagana na ndugu akatweka kwenda Shami; na Priskilla na Akula wakaenda pamoja nae, alipokwisha kunyoa kichwa chake katika Kenkrea; maana alikuwa ana nadhiri.

19Wakalika Efeso, akawaacha huko. Yeye mwenyewe akaingia katika sunagogi, akahujiana na Wayahudi.

20Walipotaka akae wakati mwingi zaidi, hakukubali:

21bali aliagana nao, akisema. Sina buddi kufanya siku kuu hii inayokuja Yerusalemi: lakini nitarejea kwenu, Mungu akinijalia.

22Akatweka, akatoka Efeso, na alipokwisha kushuka Kaisaria, akapanda juu, akawasalimu Kanisa, akatelemkia Antiokia.

23Hatta akiisha kukaa huko siku kadha wa kadha akaondoka, akapita kati ya inchi ya Galatia na Frugia, mji kwa mji, akiwatia moyo wanafunzi.

24Bassi Myahudi mmoja, jina lake Apollo, mzalia wa Iskanderia, mtu wa elimu, akalika Efeso; nae alikuwa hodari wa maandiko.

25Mtu huyu alikuwa amefundishwa njia ya Bwana; na kwa kuwa roho yake ilikuwa ikiwaka, alianza kunena na kufundisha kwa usahihi khabari za Bwana; nae alijua ubatizo wa Yohana tu.

26Akaanza kunena bila khofu katika sunagogi: hatta Akula na Priskilla walipomsikia wakamchukua kwao, wakamweleza njia ya Bwana kwa usahihi zaidi.

27Na alipotaka kuvuka bahari aende hatta Akaya, ndugu wakamhimiza, wakamwandikia barua kwa wanafunzi wale wamkaribishe; nae alipofika akawasaidia sana wale waliokwisha kuamini kwa neema ya Mungu.

28Kwa maana aliwashinda Wayahudi kabisa kabisa mbele ya watu wote, akiwaonyesha kwa maneno ya maandiko ya kuwa Yesu ni Kristo.

Swahili New Testament © Bible Society of Tanzania, 1921.
Published by: Bible Society of Tanzania