The chat will start when you send the first message.
1Walikuwepo baadhi ya manabii na walimu katika kanisa la Antiokia. Walikuwa Barnaba, Simeoni (ambaye pia aliitwa Nigeri), Lukio (kutoka mji wa Kirene), Manaeni (aliyekua pamoja na Mfalme Herode), na Sauli.[#13:1 Ni neno la Kilatini linalomaanisha weusi au nyeusi.; #13:1 Huyu ni Herode Antipa, mwana wa Herode Mkuu. Huyu ni Herode wa nne. Baada ya Herode Mkuu kufa, ufalme wake uligawanywa kwa wanaye wanne. Tazama katika Orodha ya Maneno.]
2Watu hawa wote kwa pamoja walikuwa wanamwabudu Bwana na wamefunga Roho Mtakatifu alipowaambia, “Nitengeeni Barnaba na Sauli ili wanifanyie kazi maalumu. Wao ndio niliowachagua kuifanya kazi hiyo.”
3Hivyo kanisa lilifunga na kuomba. Wakaweka mikono yao juu ya Barnaba na Sauli, wakaagana nao na kuwaacha waende.
4Barnaba na Sauli walitumwa na Roho Mtakatifu. Walikwenda katika mji wa Seleukia. Kutoka hapo walitweka tanga na kusafiri mpaka kwenye kisiwa cha Kipro.
5Barnaba na Sauli walipofika kwenye mji wa Salami, walihubiri ujumbe wa Mungu katika masinagogi ya Kiyahudi. Yohana ambaye pia anaitwa Marko alikuwa pamoja nao ili kuwasaidia.
6Walisafiri wakitisha kisiwa chote mpaka kwenye mji wa Pafo. Huko walimkuta mwanaume wa Kiyahudi aliyeitwa Bar-Yesu aliyekuwa akifanya uchawi. Alikuwa nabii wa uongo.
7Alikaa daima karibu na Sergio Paulo, aliyekuwa gavana na mtu makini sana. Sergio Paulo aliwaalika Barnaba na Sauli waende kumtembelea kwa sababu alitaka kusikia ujumbe wa Mungu.
8Lakini mchawi Elima (Bar-Yesu kama alivyoitwa kwa Kiyunani) alizungumza kinyume nao ili kuwapinga, akijaribu kumzuia gavana asimwamini Yesu.
9Kisha Sauli (ambaye pia anajulikana kama Paulo), akiwa amejaa Roho Mtakatifu, alimkazia macho Elima
10na kusema, “Ewe mwana wa Ibilisi, uliyejaa uongo na aina zote za hila za uovu! Wewe ni adui wa kila kilicho cha kweli. Hautaacha kuzibadili kweli za Bwana kuwa uongo?
11Sasa Bwana atakugusa na utakuwa asiyeona. Hautaweza kuona kitu chochote kwa muda, hata mwanga wa jua.”
Ndipo kila kitu kikawa giza kwa Elima. Akazunguka kila mahali na akapotea. Alikwenda kila mahali akijaribu kumpata mtu wa kumshika mkono ili amwongoze.
12Gavana alipoyaona haya, akaamini. Akayashangaa mafundisho kuhusu Bwana.
13Paulo na watu waliokuwa pamoja naye walitweka tanga na kusafiri kwa merikebu kutoka Pafo mpaka Perge, mji uliokuwa Pamfilia. Hapo Yohana Marko aliwaacha na akarudi Yerusalemu.
14Waliendelea na safari yao kutoka Perge na kwenda Antiokia, mji karibu na Pisidia.
Siku ya Sabato walikwenda katika sinagogi la Kiyahudi na kuketi chini.
15Sheria ya Musa na maandishi ya manabii vilisomwa. Kisha viongozi wa sinagogi wakawatumia ujumbe Paulo na Barnaba, wakisema, “Ndugu zetu, ikiwa mna kitu chochote cha kusema kitakachowasaidia watu hapa, tafadhali semeni.”
16Paulo akasimama, akanyoosha mkono wake ili wamsikilize, akasema, “Watu wa Israeli nanyi nyote msio Wayahudi mnaomwabudu Mungu wa kweli, tafadhali nisikilizeni!
17Mungu wa Israeli aliwachagua baba zetu. Na watu wetu walipoishi Misri kama wageni, aliwafanya wakuu. Kisha akawatoa katika nchi ile kwa nguvu kuu.
18Aliwavumilia kwa miaka arobaini walipokuwa jangwani.
19Mungu aliangamiza mataifa saba katika nchi ya Kanaani na kuwapa nchi yao watu wake.
20Yote haya yalitokea katika kipindi cha kadiri ya miaka mia nne na hamsini.[#13:20 Yaani miaka 400 ya kuishi Misri, miaka 40 ya kusafiri jangwani na miaka 10 ya kuteka nchi.]
Baada ya hili, Mungu akawapa watu wetu waamuzi kuwaongoza mpaka wakati wa nabii Samweli.
21Ndipo watu wakaomba kuwa na mfalme. Mungu akawapa Sauli, mwana wa Kishi. Sauli alitoka katika kabila la Benjamini. Alikuwa mfalme kwa miaka arobaini.
22Baada ya Mungu kumwondoa Sauli katika ufalme, Mungu alimfanya Daudi kuwa Mfalme wao. Hiki ndicho Mungu alisema kuhusu Daudi: ‘Daudi, mwana wa Yese, ni mtu ambaye Mimi mwenyewe nimemchagua. Atafanya kila kitu nitakachotaka afanye.’
23Kama alivyoahidi, Mungu amemleta mmoja wa wazao wa Daudi katika Israeli ili awe Mwokozi wao, mzao huyo wa Daudi ni Yesu.
24Kabla Yesu hajaja, Yohana aliwaambia watu wote wa Israeli wanachopaswa kufanya. Waliwaambia wabatizwe kuonesha kuwa walitaka kubadili maisha yao.
25Yohana alipokuwa anamaliza kazi yake, alisema, ‘Mnadhani mimi ni nani? Mimi siyo Masihi. Masihi atakuja baadaye, nami sistahili kuwa mtumwa wake wa kufungua kamba za viatu vyake.’[#13:25 Kwa maana ya kawaida, “Mimi” (yaani, “yeye” au “Yule anayestahili”), Hii inamaanisha yule aliyechaguliwa na kutumwa na Mungu. Linganisha na Yh 1:20. Tazama katika Orodha ya Maneno.]
26Ndugu zangu, wana katika familia ya Abrahamu na ninyi watu wengine ambao pia mnamwabudu Mungu wa kweli, sikilizeni! Habari kuhusu wokovu huu imeletwa kwetu.
27Wayahudi waishio Yerusalemu na viongozi wao hawakutambua kuwa Yesu ni Mwokozi. Maneno ambayo manabii waliandika kuhusu yeye yalikuwa yakisomwa kila siku ya Sabato, lakini hawakuyaelewa. Walimhukumu Yesu. Walipofanya hivi, waliyatimiliza maneno ya manabii.
28Hawakupata sababu ya msingi kwa nini Yesu afe, lakini walimwomba Pilato amwue.
29Wayahudi hawa walimtendea Yesu mambo yote mabaya ambayo Maandiko yalisema yangempata Yesu. Kisha walimteremsha Yesu kutoka msalabani na kumweka kaburini.
30Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu!
31Baada ya hili, kwa siku nyingi, wale waliofuatana na Yesu kutoka Galilaya mpaka Yerusalemu walimwona. Wao sasa ni mashahidi wake kwa watu wetu.
32Tunawahubiri Habari Njema kuhusu ahadi ambayo Mungu aliiweka kwa baba zetu.
33Sisi ni wazao wao, na Mungu ameitimiza ahadi hii kwa ajili yetu. Mungu aliitimiza ahadi hii kwa kumfufua Yesu kutoka kwa wafu. Tunasoma pia kuhusu hili katika Zaburi 2:
‘Wewe ni Mwanangu.
Leo nimekuwa baba yako.’
34Mungu alimfufua Yesu kutoka kwa wafu. Yesu hatarudi kaburini na kuwa mavumbi. Hivyo Mungu alisema,
‘Nitawapa ahadi ya kuaminiwa na
takatifu niliyoiahidi kwa Daudi.’
35Lakini Zaburi nyingine inasema,
‘Hautaruhusu Mtakatifu wako aoze kaburini.’
36Daudi aliyatenda mapenzi ya Mungu alipokuwa hai. Kisha alikufa na kuzikwa kama baba zake wote. Na mwili wake ulioza kaburini!
37Lakini yule ambaye Mungu alimfufua kutoka kwa wafu hakuoza kaburini.
38-39Ndugu zangu, eleweni yale tunayowaambia. Mnaweza kupata msamaha wa dhambi kupitia huyu Yesu. Sheria ya Musa haikuwatoa kutoka katika dhambi zenu. Lakini mnaweza kuwa huru mbali na hukumu.
40Hivyo iweni waangalifu! Msiruhusu walichosema manabii kikawatokea ninyi:
41‘Sikilizeni enyi watu wenye mashaka!
Mnaweza kushangaa,
lakini sasa nendeni na mfe.
Kwa sababu kipindi cha wakati wenu,
nitafanya kitu ambacho hamtaamini.
Hata kama kitafafanuliwa kwenu!’”
42Paulo na Barnaba walipokuwa wanaondoka kwenye sinagogi, watu waliwaomba warudi tena Sabato inayofuata ili wawaeleze zaidi kuhusu mambo haya.
43Baada ya mkutano, watu wengi, Wayahudi na wale waliobadili dini zao na kufuata dini ya Kiyahudi, waliwafuata Paulo na Barnaba; nao waliwatia moyo watu hawa waendelee kuitumaini neema ya Mungu.
44Siku ya Sabato iliyofuata, karibu watu wote katika mji walikusanyika ili wasikie neno la Bwana.
45Wayahudi waliokuwepo pale walipowaona watu wote hawa, wakaingiwa na wivu sana. Wakakashifu na kubishia kila kitu alichosema Paulo.
46Lakini Paulo na Barnaba walihubiri kwa ujasiri. Walisema, “Tulikuwa tuuhubiri ujumbe wa Mungu kwenu ninyi Wayahudi kwanza, lakini mmekataa kusikiliza. Mmeweka wazi kuwa hamstahili kuupata uzima wa milele. Hivyo tutakwenda sasa kwa wale wasio Wayahudi.
47Hivi ndivyo Bwana alivyotuambia kufanya:
‘Nimewafanya ninyi mwanga kwa ajili ya mataifa mengine,
kuwaonesha watu ulimwenguni kote njia ya wokovu.’”
48Wasio Wayahudi waliposikia Paulo akisema hivi, walifurahi sana. Waliuheshimu ujumbe wa Bwana, na wengi wao wakauamini. Hawa ni wale waliochaguliwa kuupata uzima wa milele.
49Na hivyo ujumbe wa Bwana ulihubiriwa katika nchi yote.
50Lakini Wayahudi pale walisababisha baadhi ya wanawake muhimu waifuatayo dini na viongozi wa mji kuwakasirikia na kuwachukia Paulo na Barnaba na wakawafukuza mjini.
51Hivyo Paulo na Barnaba wakakung'uta mavumbi ya miguu yao. Kisha wakaenda katika mji wa Ikonia.[#13:51 Ilionesha kuwa walimaliza kuzungumza na watu hawa.]
52Lakini wafuasi wa Bwana katika Antiokia walijaa furaha na walijazwa Roho Mtakatifu.