Waebrania 1

Waebrania 1

Mungu Amesema Kupitia Mwanaye

1Zamani Mungu alisema na baba zetu kwa kuwatumia manabii. Alisema nao mara nyingi na kwa njia nyingi tofauti.

2Lakini sasa katika siku hizi za mwisho Mungu amesema nasi tena kupitia Mwana wake. Mungu aliuumba ulimwengu wote kupitia Mwana wake. Na alimchagua Mwana kumiliki mambo yote.

3Huyo Mwana huuonesha utukufu wa Mungu. Yeye ni nakala halisi ya asili yake Mungu, na huviunganisha vitu vyote pamoja kwa amri yake yenye nguvu. Mwana aliwasafisha watu kutoka katika dhambi zao. Kisha akaketi upande wa kuume wa Mungu, aliye Mkuu huko Mbinguni.[#1:3 Mahali pa heshima na mamlaka (nguvu).]

4Mwana akawa mkuu zaidi kuliko malaika, na Mungu akampa jina lililo kuu zaidi kuliko lolote katika majina yao.

5Mungu kamwe hajamwambia malaika yeyote maneno haya:

“Wewe ni Mwanangu.

Mimi leo hii nimekuwa Baba yako.”

Mungu pia kamwe hajasema juu ya malaika,

“Nitakuwa Baba yake,

naye atakuwa mwanangu.”

6Na kisha, pale Mungu anapomtambulisha Mwanaye mzaliwa wa kwanza ulimwenguni, anasema,[#1:6 Hii inaweza kumaanisha ulimwengu ambamo Yesu alizaliwa (tazama Lk 2:1-14) au inaweza kuwa na maana ile ile kama katika 2:5, yaani, ulimwengu unaokuja; ambamo Kristo ametajwa kama mfalme baada ya kufufuka kwake (tazama Flp 2:9-11).]

“Basi malaika wote wa Mungu wamwabudu yeye.”

7Hivi ndivyo Mungu alivyosema kuhusu malaika:

“Yeye huwabadilisha malaika zake kuwa upepo

na watumishi wake kuwa miali ya moto.”

8Lakini hivi ndivyo alivyosema kuhusu Mwana wake:

“Mungu, ufalme wako utadumu milele na milele.

Unatumia mamlaka yako kwa haki.

9Unapenda kilicho sahihi na kuchukia kilicho na makosa.

Hivyo Mungu, Mungu wako, amekuchagua wewe,

na amekupa heshima na furaha zaidi kupita yeyote aliye kama wewe.”

10Pia Mungu alisema,

“Ee Bwana, mwanzo uliiumba dunia,

na mikono yako ikaliumba anga.

11Vitu hivi vitatoweka, lakini wewe utaendelea kuwepo.

Vyote vitachakaa kama mavazi makuu kuu.

12Utavikunja hivyo kama koti,

navyo vitabadilishwa kama mavazi.

Lakini wewe hubadiliki,

na uhai wako hautafikia mwisho.”

13Na Mungu hakuwahi kusema haya kwa malaika:

“Ukae mkono wangu wa kuume

hadi nitakapowaweka adui zako chini ya uwezo wako.”

14Malaika wote ni roho ambao humtumikia Mungu nao hutumwa kuwasaidia wale watakaoupokea wokovu.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International