Yohana 12

Yohana 12

Mwanamke Ampa Yesu Heshima

(Mt 26:6-13; Mk 14:3-9)

1Siku sita kabla ya sikukuu ya Pasaka, Yesu alienda Bethania. Huko ndiko alikoishi Lazaro, yule mtu aliyefufuliwa na Yesu kutoka wafu.

2Hapo walimwandalia Yesu karamu ya chakula. Naye Martha alihudumu na Lazaro alikuwa mmoja wa watu waliokuwa wakila chakula pamoja na Yesu.

3Mariamu akaleta manukato ya thamani sana yaliyotengenezwa kwa nardo asilia kwenye chombo chenye ujazo wa nusu lita hivi. Akayamwaga manukato hayo miguuni mwa Yesu. Kisha akaanza kuifuta miguu ya Yesu kwa nywele zake. Harufu nzuri ya manukato hayo ikajaa nyumba nzima.[#12:3 Kwa maana ya kawaida, “” ni ratili ya Kirumi, sawa na gramu 327.]

4Yuda Iskariote, mmoja wa wafuasi wa Yesu, naye alikuwepo hapo.

5Yuda ambaye baadaye angemkabidhi Yesu kwa maadui zake akasema, “Manukato hayo yana thamani ya mshahara wa mwaka wa mtu. Bora yangeuzwa, na fedha hizo wangepewa maskini.”[#12:5 Wa mwaka wa mtu kwa hali halisi “ 300” (sarafu za fedha). Sarafu moja, ya Kirumi, ilikuwa ni wastani wa mshahara wa mtu wa siku moja.]

6Lakini Yuda hakusema hivyo kwa vile alikuwa anawajali sana maskini. Alisema hivyo kwa sababu alikuwa mwizi. Naye ndiye aliyetunza mfuko wa fedha za wafuasi wa Yesu. Naye mara kadhaa aliiba fedha kutoka katika mfuko huo.

7Yesu akajibu, “Msimzuie. Ilikuwa sahihi kwake kutunza manukato haya kwa ajili ya siku ya leo; siku ambayo maziko yangu yanaandaliwa.

8Nyakati zote mtaendelea kuwa pamoja na hao maskini. Lakini si kila siku mtakuwa pamoja nami.”[#12:8 Nyakati zote wataendelea kuwepo maskini pamoja nanyi. Tazama Kum 15:11.]

Mpango Dhidi ya Lazaro

9Wayahudi wengi wakasikia kwamba Yesu alikuwa Bethania, Kwa hiyo walienda huko ili wakamwone. Walienda pia ili kumwona Lazaro, yule ambaye Yesu alimfufua kutoka wafu.

10Viongozi wa makuhani nao wakafanya mpango wa kumuua Lazaro.

11Walitaka kumwua kwa sababu, Wayahudi wengi waliwaacha makuhani hao na kumwamini Yesu.

Yesu Aingia Yerusalemu Kama Mfalme

(Mt 21:1-11; Mk 11:1-11; Lk 19:28-40)

12Siku iliyofuata watu waliokuwamo Yerusalemu walisikia kwamba Yesu alikuwa anakuja huko. Hili ni kundi la watu waliokuja kusherehekea sikukuu ya Pasaka.

13Hawa walibeba matawi ya miti ya mitende na kwenda kumlaki Yesu. Pia walipiga kelele wakisema,

“‘Msifuni Yeye!’

‘Karibu! Mungu ambariki yeye

anayekuja kwa jina la Bwana!’

Mungu ambariki Mfalme wa Israeli!”

14Yesu akamkuta punda njiani naye akampanda, kama vile Maandiko yanavyosema,

15“Msiogope, enyi watu wa Sayuni![#12:15 Kwa maana ya kawaida, “binti Sayuni”, ina maana mji wa Yerusalemu. Tazama katika Orodha ya Maneno.]

Tazameni! Mfalme wenu anakuja.

Naye amepanda mwana punda.”

16Wafuasi wa Yesu hawakuyaelewa yale yaliyokuwa yanatokea wakati huo. Lakini Yesu alipoinuliwa juu kwenye utukufu, ndipo walipoelewa kuwa haya yalitokea kama ilivyoandikwa juu yake. Kisha wakakumbuka kwamba walifanya mambo haya kwa ajili ya Yesu.

17Siku Yesu alipomfufua Lazaro kutoka wafu na kumwambia atoke kaburini walikuwepo watu wengi pamoja naye. Hawa walikuwa wakiwaeleza wengine yale aliyoyafanya Yesu.

18Ndiyo sababu watu wengi walienda ili kumlaki Yesu; kwa kuwa walikuwa wamesikia habari za ishara hii aliyoifanya.

19Mafarisayo nao wakasemezana wao kwa wao, “Tazameni! Mpango wetu haufanyi kazi. Watu wote wanamfuata Yesu!”

Yesu Azungumza Kuhusu Kifo Chake

20Hapo Yerusalemu walikuwepo pia Wayunani. Hawa walikuwa ni miongoni mwa watu walioenda mjini humo kuabudu wakati wa sikukuu ya Pasaka.

21Hao walimwendea Filipo, aliyetoka Bethsaida kule Galilaya. Wakasema, “Bwana, tunahitaji kumwona Yesu.”

22Filipo alienda na kumwambia Andrea hitaji lao. Kisha Andrea na Filipo walienda na kumwambia Yesu.

23Yesu akawaambia Filipo na Andrea, “Wakati umefika kwa Mwana wa Adamu kuupokea utukufu wake.

24Ni ukweli kwamba mbegu ya ngano inapaswa kuanguka katika ardhi na kuoza kabla ya kukua na kuzaa nafaka nyingi ya ngano. Kama haitakufa, haitaongezeka zaidi ya hiyo mbegu moja.

25Yeyote anayeyapenda maisha yake aliyonayo atayapoteza. Yeyote atakayetoa maisha yake kwa Yesu katika ulimwengu huu atayatunza. Nao wataupata uzima wa milele.

26Kama mtu atanitumikia inampasa anifuate. Watumishi wangu watakuwa pamoja nami popote nitakapokuwa. Mtu atakayenitumikia Baba yangu atamheshimu.

Yesu Azungumza Kuhusu Kifo Chake

27Sasa ninapata taabu sana rohoni mwangu. Nisemeje? Je! niseme, ‘Baba niokoe katika wakati huu wa mateso’? Hapana, nimeufikia wakati huu ili nipate mateso.

28Baba yangu, ufanye yale yatakayokuletea wewe utukufu!”

Kisha sauti kutoka mbinguni ikasikika ikisema, “Tayari nimekwisha upata utukufu wangu. Nitaupata tena.”

29Watu waliokuwa wamesimama hapo wakaisikia sauti hiyo. Wakasema ilikuwa ni ngurumo. Lakini wengine wakasema, “Malaika amesema naye!”

30Yesu akasema, “Sauti hiyo ilikuwa ni kwa ajili yenu si kwa ajili yangu.

31Sasa ni wakati wa ulimwengu kuhukumiwa. Sasa mtawala wa ulimwengu huu atatupwa nje.[#12:31 Huyu ni Shetani. Tazama katika Orodha ya Maneno.]

32Nami nitainuliwa juu kutoka katika nchi. Mambo hayo yatakapotokea, nitawavuta watu wote waje kwangu.”[#12:32 Hapa “Kuinuliwa juu” ina maana ya kupigiliwa misumari msalabani na “kuinuliwa” nao. Pia katika mstari wa 34.]

33Yesu alisema hili kuonesha jinsi ambavyo atakufa.

34Watu wakasema, “Lakini sheria yetu inasema kwamba Masihi ataishi milele. Sasa kwa nini unasema, ‘Ni lazima Mwana wa Adamu ainuliwe juu’? Ni nani huyu ‘Mwana wa Adamu’?”

35Kisha Yesu akasema, “Nuru itabaki pamoja nanyi kwa muda mfupi tu. Kwa hiyo mtembee mkiwa bado na hiyo nuru. Hapo giza halitaweza kuwakamata. Watu wanaotembea gizani hawajui kule wanakoenda.[#12:35 Ina maana ya Kristo, kama katika Yh 1:5-9. Pia ni ishara ya wema na kweli unahusiana na Kristo na ufalme wake.; #12:35 Giza au usiku ni ishara ya aina zote za mambo yanayoueleza ufalme wa Shetani, kama vile dhambi na maovu.]

36Hivyo wekeni matumaini yenu katika nuru wakati bado mkiwa nayo. Jinsi hiyo mtakuwa watoto wa nuru.” Yesu alipomaliza kusema mambo hayo, aliondoka na kwenda mahali ambapo watu wasingeweza kumwona.

Baadhi ya Wayahudi Wakataa Kumwamini Yesu

37Watu wakaona ishara hizi zote alizozifanya Yesu, lakini bado hawakumwamini.[#12:37 Ni tendo la kushangaza linalodhihirisha nguvu za Mungu.]

38Haya yalikuwa hivyo ili kuthibitisha yale aliyoyasema nabii Isaya kuwa:

“Bwana, ni nani aliyeamini yale tuliyowaambia?

Ni nani aliyeziona nguvu za Bwana?”

39Hii ndiyo sababu watu hawakuweza kuamini. Kwani Isaya alisema pia,

40“Mungu aliwafanya baadhi ya watu wasione.

Aliufunga ufahamu wao.

Alifanya hivi ili wasiweze kuona kwa macho yao

na kuelewa kwa ufahamu wao.

Alifanya hivyo ili wasiweze kugeuka

na kuponywa.”

41Isaya alisema hivi kwa sababu aliuona ukuu wa Mungu ndani ya Yesu. Naye alizungumza habari zake Yesu.[#12:41 Kihalisia, “utukufu”, ni neno linaloonyesha sifa maalumu za Mungu. Tazama katika Orodha ya Maneno.]

42Lakini watu wengi wakamwamini Yesu. Hata wengi miongoni mwa viongozi wa Wayahudi wakamwamini, lakini walikuwa na hofu juu ya Mafarisayo, hivyo hawakusema kwa uwazi kwamba wameamini. Hao walikuwa na hofu kwamba wangeamriwa watoke na kukaa nje ya sinagogi.

43Wao walipenda kusifiwa na watu zaidi kuliko kupata sifa zinazotoka kwa Mungu.

Mafundisho ya Yesu Yatawahukumu Watu

44Kisha Yesu akapaza sauti, “Mtu yeyote anayeniamini basi kwa hakika anamwamini yule aliyenituma.

45Yeyote anayeniona mimi hakika anamwona yeye aliyenituma.

46Nimekuja katika ulimwengu huu kama mwanga. Nimekuja ili kila mmoja atakayeniamini asiendelee kuishi katika giza.

47Sikuja ulimwenguni humu kuwahukumu watu. Nimekuja ili kuwaokoa watu wa ulimwengu huu. Hivyo mimi siye ninayewahukumu wale wanaosikia mafundisho yangu bila kuyafuata.

48Isipokuwa yupo hakimu wa kuwahukumu wote wanaokataa kuniamini na wasiokubaliana na yale ninayoyasema. Ujumbe ninaousema utawahukumu ninyi siku ya mwisho.

49Hiyo ni kwa sababu yale niliyofundisha hayakutoka kwangu. Baba aliyenituma ndiye aliyeniambia yale nitakayosema na kuyafundisha.

50Nami najua amri za Mungu kwamba lolote alisemalo na kutenda litawaletea watu uzima wa milele, kama watazifanya. Hivyo mambo ninayosema ni yale ambayo Baba yangu ameniambia niyaseme.”

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International