Warumi 13

Warumi 13

Kutii Watawala

1Watiini watawala wa serikali. Hakuna anayeweza kutawala bila mamlaka ya Mungu. Mamlaka ya kutawala hutoka kwa Mungu.

2Hivyo yeyote anayekuwa kinyume na serikali hakika anakuwa kinyume na kitu ambacho Mungu amekiweka. Wale walio kinyume na serikali wanajiletea adhabu wao wenyewe.

3Watu wanaotenda mema hawawaogopi watawala. Bali wale wanaotenda mabaya ni lazima wawaogope watawala. Je! mnataka kuwa huru mbali na kuwaogopa hao? Basi mfanye yaliyo sahihi tu, nao watawasifu ninyi.

4Watawala ni watumishi wa Mungu kwa ajili ya kuwasaidia ninyi. Lakini mkifanya yasiyo sahihi, mnayo sababu ya kuwa na woga. Hao wanayo mamlaka ya kuwaadhibu, na watayatumia mamlaka hayo. Wao ni watumishi wa Mungu ili wawaadhibu wale wanaofanya yale yasiyo sahihi.

5Kwa hiyo mnapaswa kuitii serikali, siyo tu kwa sababu mtaadhibiwa, bali kwa sababu mnajua kuwa ni jambo lililo sahihi kufanya hivyo.

6Na hii ndiyo sababu mnalipa kodi. Watawala hawa wanapaswa kulipwa kwa ajili ya kutimiza wajibu wao wote walionao wa kutawala. Hakika wanatumika kwa ajili ya Mungu.

7Wapeni watu wote vile wanavyowadai. Kama wanawadai aina yoyote ya kodi, basi lipeni. Onesheni heshima kwa wale mnaopaswa kuwaheshimu. Na onesheni uadilifu kwa wale mnaopaswa kuwafanyia hivyo.

Kuwapenda Wengine Ndiyo Sheria Pekee

8Msidaiwe chochote na mtu, isipokuwa mdaiwe upendo baina yenu. Mtu anayewapenda wengine anakuwa amefanya yote yanayoamriwa na sheria.

9Sheria inasema, “Usizini, usiue, usiibe, usitamani kitu cha mtu mwingine.” Amri hizo zote na zingine hakika zinajumlishwa na kuwa kanuni moja tu, “Mpende jirani yako kama unavyojipenda wewe mwenyewe.”[#Kut 20:13-15,17; #13:9 Au “wengine”. Mafundisho ya Yesu katika Lk 10:25-37 yanaonesha kwa uwazi kuwa hii ni pamoja na yeyote mwenye uhitaji.; #Law 19:18]

10Upendo hauwaumizi wengine. Hivyo kupenda ni sawa na kuitii sheria yote.

11Nalisema hili kwa sababu mnajua kwamba tunaishi katika wakati ulio muhimu. Ndiyo, ni wakati wenu sasa kuamka kutoka usingizini. Wokovu wetu sasa uko karibu zaidi kuliko ilivyokuwa tulipoamini kwa mara ya kwanza.

12Usiku karibu umekwisha. Na mchana karibu unaingia. Hivyo tunapaswa kuacha kufanya chochote kinachohusiana na giza. Tunapaswa kujiandaa kuupiga uovu kwa silaha za nuru.

13Tunapaswa kuishi katika njia sahihi, kama watu walio wa mchana. Hatupaswi kuwa na tafrija za ovyo ama kulewa. Hatupaswi kujihusisha katika dhambi ya uzinzi au ya aina yoyote ya mwenendo usiofaa. Hatupaswi kusababisha mabishano au kuwa na wivu.

14Bali, muwe kama Kristo Yesu katika kila jambo mnalolitenda, ili watu watakapowaangalia, waweze kumwona yeye. Msifikirie namna ya kuridhisha matakwa ya udhaifu wa mwanadamu na tamaa zake.[#13:14 Kwa maana ya kawaida, “Bali mvaeni Bwana Yesu Kristo.”]

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International