Warumi 4

Warumi 4

Mfano wa Abrahamu

1Basi tuseme nini kuhusu Abrahamu, baba wa watu wetu?[#4:1 Au “Tuseme tumeona nini [katika Sheria] kuhusu Abrahamu?”]

2Ikiwa Abrahamu alifanywa kuwa mwenye haki kutokana na matendo yake, hicho ni kitu cha kujivunia! Lakini kama Mungu anavyoona, hakuwa na sababu ya kujivuna.

3Hili ni wazi kama Maandiko yanavyosema, “Abrahamu alimwamini Mungu, na kwa sababu ya kuamini kwake, Mungu alimhesabu kuwa mwenye haki.”[#4:3 Mwa 15:6. Pia katika mstari wa 9 na 22.]

4Watu wanapofanya kazi, mshahara wao hautolewi kama zawadi. Ni kitu wanachopata kutokana na kazi waliyofanya.

5Lakini watu hawawezi kufanya kazi yoyote itakayowafanya wahesabiwe kuwa wenye haki mbele za Mungu. Hivyo ni lazima wamtumaini Yeye. Kisha huikubali imani yao na kuwahesabia haki. Yeye ndiye anayewahesabia haki hata waovu.

6Daudi alisema mambo hayo hayo alipozungumzia baraka wanazopata watu pale Mungu anapowahesabia haki pasipo kuangalia matendo yao:

7“Ni heri kwa watu

wanaposamehewa kutokana na mabaya waliyotenda,

dhambi zao zinapofutwa!

8Ni heri kwa watu,

Bwana anapozifuta dhambi zao kutoka katika kumbukumbu yake!”

9Je! baraka hii ni kwa ajili ya waliotahiriwa tu? Au pia ni kwa ajili ya wale wasiotahiriwa? Tumekwisha sema ya kwamba Abrahamu alikubaliwa kuwa ni mwenye haki mbele za Mungu kutokana na imani yake.

10Sasa katika mazingira gani hili lilitokea? Je! Mungu alimkubali Abrahamu na kumhesabia haki kabla au baada ya kutahiriwa? Mungu alimkubali kabla ya kutahiriwa kwake.

11Abrahamu alitahiriwa baadaye ili kuonesha kuwa Mungu amemkubali kuwa mwenye haki. Tohara yake ilikuwa uthibitisho kwamba Mungu alimhesabia haki kwa njia ya imani hata kabla ya kutahiriwa. Hivyo Abrahamu ni baba wa wote wanaoamini lakini hawajatahiriwa. Kama Abrahamu, wao pia wamekubaliwa na Mungu kuwa wenye haki kwa sababu ya imani yao tu.

12Pia Abrahamu ni baba wa waliotahiriwa, lakini si kwa sababu ya kutahiriwa kwao. Ni baba yao kwa sababu wao nao wamemwamini Mungu vile vile kama Abrahamu alivyofanya kabla hajatahiriwa.

Ahadi ya Mungu Hupokelewa kwa Imani

13Mungu aliweka ahadi kwa Abrahamu na wazaliwa wake ya kuwapa ulimwengu wote. Lakini kwa nini Mungu aliweka ahadi hii? Haikuwa kwa sababu Abrahamu aliifuata sheria. Ni kwa sababu aliiweka imani yake katika Mungu na akakubaliwa kuwa mwenye haki.

14Watu wa Mungu watarithi yote ambayo Mungu alimwahidi Abrahamu, lakini si kwa sababu wanaifuata sheria. Ikiwa ni lazima tuitii sheria ili tupate kile alichoahidi Mungu, badi imani ya Abrahamu haina maana yoyote na ahadi ya Mungu haina manufaa.

15Ninasema hivi kwa sababu sheria ndiyo huleta hasira ya Mungu kwa wale wasioitii. Lakini ikiwa sheria haipo, basi hakuna hatia ya kutoitii.

16Hivyo watu hupokea ahadi ya Mungu kwa imani. Hili hutokea ili ahadi hiyo iwe kipawa cha bure. Na ikiwa ahadi ni kipawa cha bure, basi watu wote wa Abrahamu watapata ahadi hiyo. Ahadi hii si tu kwa ajili ya wale wanaoishi chini ya Sheria ya Musa. Bali ni kwa ajili ya wote wanaoishi kwa kuweka imani yao kwa Mungu kama Abrahamu alivyofanya. Ni baba yetu sote.

17Kama Maandiko yanavyosema, “Nimekufanya uwe baba wa mataifa mengi.” Abrahamu aliposikia ahadi hii, aliiweka imani yake kwa Mungu. Mungu ndiye awapaye uhai waliokufa na kwa amri yake huumba kisichokuwepo.[#Mwa 17:5]

18Halikuwepo tumaini kwamba Abrahamu angepata watoto, lakini alimwamini Mungu na akaendelea kutumaini. Na ndiyo sababu akafanyika kuwa baba wa mataifa mengi. Kama Mungu alivyomwambia kuwa, “Utakuwa na wazaliwa wengi.”[#Mwa 15:5]

19Abrahamu alikuwa na umri uliokaribia miaka 100, hivyo alikuwa amevuka umri wa kupata watoto. Pia, Sara hakuweza kuwa na watoto. Abrahamu alilijua hili vizuri, lakini imani yake kwa Mungu haikudhoofika.

20Hakutilia shaka kuwa Mungu angetenda kile alichoahidi. Hakuacha kuamini. Kwa hakika, aliendelea kuimarika katika imani yake. Alitukuza Mungu

21na alikuwa na uhakika kuwa Mungu anaweza kutenda alichoahidi.

22Ndiyo sababu “Mungu alimkubali kuwa ni mwenye haki”.

23Maneno haya, “alikubaliwa”, yaliandikwa siyo tu kwa ajili ya Abrahamu.

24Pia yaliandikwa kwa ajili yetu. Mungu atatukubali sisi pia kwa sababu tunaamini. Tunamwamini yule aliyemfufua Yesu Bwana wetu kutoka kwa wafu.

25Yesu alitolewa afe kwa ajili ya dhambi zetu, na akafufuliwa kutoka kifo ili Mungu atuhesabie haki.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International