Maombolezo 4

Maombolezo 4

Yerusalemu baada ya kuangamia

1Jinsi gani dhahabu yetu ilivyochujuka,

dhahabu safi kabisa ilivyobadilika!

Mawe ya thamani yametawanywa

yamesambaa barabarani kote.

2Watoto wa Siyoni waliosifika sana,

waliothaminiwa kama dhahabu safi,

jinsi gani sasa wamekuwa kama vyombo vya udongo,

kazi ya mikono ya mfinyanzi!

3Hata mbwamwitu huwa na hisia za mama

na kuwanyonyesha watoto wao;

lakini watu wangu wamekuwa wakatili,

hufanya kama mbuni nyikani.

4Midomo ya watoto wachanga imekauka kwa kiu,

watoto wanaomba chakula lakini hakuna anayewapa.

5Watu waliojilisha vyakula vinono

sasa wanakufa njaa barabarani.

Waliolelewa na kuvikwa kifalme

sasa wanafukua kwa mikono kwenye majaa.

6Watu wangu wamepata adhabu kubwa[#Taz Mwa 19:24]

kuliko watu wa mji wa Sodoma

mji ambao uliteketezwa ghafla

bila kuwa na muda wa kunyosha mkono.

7Vijana wa Siyoni walikuwa safi kuliko theluji,

walikuwa weupe kuliko maziwa.

Miili yao ilikuwa myekundu kama matumbawe,

uzuri wa viwiliwili vyao kama johari ya rangi ya samawati.

8Sasa sura zao ni nyeusi kuliko makaa,

wanapita barabarani bila kujulikana;

ngozi yao imegandamana na mifupa yao

imekauka, imekuwa kama kuni.

9Afadhali waliouawa kwa upanga

kuliko waliokufa kwa njaa,

ambao walikufa polepole

kwa kukosa chakula.

10Kina mama ambao huwa na huruma kuu[#Taz Kumb 38:57; Eze 5:10]

waliwapika watoto wao wenyewe,

wakawafanya kuwa chakula chao

wakati watu wangu walipoangamizwa.

11Mwenyezi-Mungu alionesha uzito wa ghadhabu yake,

aliimimina hasira yake kali;

aliwasha moto huko mjini Siyoni

ambao uliteketeza misingi yake.

12Wafalme duniani hawakuamini

wala wakazi wowote wa ulimwenguni,

kwamba mvamizi au adui

angeweza kuingia malango ya Yerusalemu.

13Hayo yalisababishwa na dhambi za manabii wake,

yalitukia kwa sababu ya uovu wa makuhani wake

ambao walimwaga damu ya waadilifu mjini kwake.

14Walitangatanga barabarani kama vipofu,

walikuwa wamekuwa najisi kwa damu,

hata asiwepo mtu yeyote wa kuwagusa.

15Watu waliwapigia kelele wakisema:

“Tokeni, nendeni zenu enyi mlio najisi!

Tokeni, tokeni, msiguse chochote.”

Hivyo wakawa wakimbizi na kutangatanga;

watu wa mataifa walitamka:

“Hawa hawatakaribishwa kukaa kwetu!”

16Mwenyezi-Mungu mwenyewe aliwatawanya,

wala hatawajali tena.

Makuhani hawatapata tena heshima,

wazee hawatapendelewa tena.

17Tulichoka kukaa macho kungojea msaada;

tulikesha na kungojea kwa hamu

taifa ambalo halikuweza kutuokoa.

18Watu walifuatilia hatua zetu,

tukashindwa kupita katika barabara zetu.

Siku zetu zikawa zimetimia;

mwisho wetu ukawa umefika.

19Waliotufuatia walikuwa wepesi kuliko tai,

walitukimbiza milimani,

walituvizia huko nyikani.

20Walimnasa yule ambaye maisha yetu yalimtegemea,

yule mfalme aliyewekwa wakfu wa Mwenyezi-Mungu,

yule ambaye tulisema: “Chini ya ulinzi wake

tutaishi miongoni mwa mataifa.”

21Wakazi wa Edomu, mwaweza kushangilia kwa sasa,

mwaweza kwa sasa kufurahi enyi wakazi wa Uzi;

lakini kikombe hiki cha adhabu kitawajia pia,

nanyi pia mtakinywa na kulewa,

hata mtayavua mavazi yenu!

22Adhabu ya uovu wako ewe Siyoni imekamilika;

Mwenyezi-Mungu hatawaacha zaidi uhamishoni.

Lakini nyinyi Waedomu atawaadhibu kwa uovu wenu,

atazifichua dhambi zenu.

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania