Mika 6

Mika 6

Lalamiko la nabii

1Sikilizeni anachosema Mwenyezi-Mungu:

“Wewe nabii, nenda ukailalamikie milima,

navyo vilima visikie sauti yako.”

2Sikilizeni kesi ya Mwenyezi-Mungu enyi milima,

sikilizeni enyi misingi ya kudumu ya dunia!

Mwenyezi-Mungu anayo kesi dhidi ya watu wake.

Yeye atatoa mashtaka dhidi ya Waisraeli.

3Mwenyezi-Mungu asema hivi:

“Enyi watu wangu, nimewatendea nini?

Nimewachosha kwa kitu gani?

Nijibuni!

4Mimi niliwatoa nchini Misri;

niliwakomboa kutoka utumwani;

niliwapeni Mose, Aroni na Miriamu kuwaongoza.

5Enyi watu wangu,

kumbukeni njama za Balaki mfalme wa Moabu,

na jinsi Balaamu mwana wa Beori alivyomjibu.

Kumbukeni yaliyotukia njiani kati ya Shitimu na Gilgali.

Kumbukeni mtambue matendo yangu ya kuwaokoa!”

Swali la watu

6Nimwendee Mwenyezi-Mungu na kitu gani,

nipate kumwabudu Mungu aliye juu?

Je, nimwendee na sadaka za kuteketezwa,

nimtolee ndama wa mwaka mmoja?

7Je, Mwenyezi-Mungu atapendezwa

nikimtolea maelfu ya kondoo madume,

au mito elfu na elfu ya mafuta?

Je, nimtolee mzaliwa wangu wa kwanza

kwa ajili ya kosa langu,

naam, mtoto wangu

kwa ajili ya dhambi yangu?

Jibu la nabii

8Mungu amekuonesha yaliyo mema, ewe mtu;

anachotaka Mwenyezi-Mungu kwako ni hiki:

Kutenda mambo ya haki,

kupenda kuwa na huruma,

na kuishi kwa unyenyekevu na Mungu wako.

9Mwenyezi-Mungu anawaita wakazi wa mji,

na ni jambo la busara sana kumcha yeye:

“Sikilizeni, enyi watu wa Yuda;

sikilizeni enyi mliokusanyika mjini.

10“Je, nitavumilia maovu

yaliyorundikwa nyumbani mwao,

mali zilizopatikana kwa udanganyifu,

na matumizi ya mizani danganyifu,

jambo ambalo ni chukizo?

11Je, naweza kusema hawana hatia

watu wanaotumia mizani ya danganyifu

na mawe ya kupimia yasiyo halali?

12Matajiri wa miji wamejaa dhuluma,

wakazi wake husema uongo,

kila wasemacho ni udanganyifu.

13Kwa hiyo nami, nimeanza kuwaangusha chini,

na kuwaangamiza kwa sababu ya dhambi zenu.

14Mtakula lakini hamtashiba;

ndani mwenu njaa itazidi kuwauma.

Mkiweka akiba haitahifadhiwa,

na mkihifadhi kitu nitakiharibu kwa vita.

15Mtapanda mbegu, lakini hamtavuna.

Mtasindika zeituni, lakini hamtatumia hayo mafuta.

Mtasindika zabibu, lakini hamtakunywa hiyo divai.

16Nyinyi mnafuata mfano mbaya wa mfalme Omri

na mfano wa jamaa ya mfalme Ahabu

na mfano mbaya wa jamaa ya mwanawe, Ahabu,

na mmefuata mashauri yao.

Kwa hiyo nitawaleteeni maangamizi,

na kila mtu atawadharau.

Watu watawadhihaki kila mahali.”

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania