The chat will start when you send the first message.
1Kwa nini mataifa yanafanya ghasia?[#Taz Mate 4:25-26]
Mbona watu wanafanya njama za bure?
2Wafalme wa dunia wanajitayarisha;
watawala wanashauriana pamoja,
dhidi ya Mwenyezi-Mungu na mteule wake.
3Wanasema: “Tujiondoe katika utawala wao;
tutupilie mbali minyororo yao!”
4Mwenyezi-Mungu atawalaye juu mbinguni,
anawacheka na kuwadhihaki.
5Kisha, anawakaripia kwa ghadhabu,
na kuwatisha kwa hasira, akisema:
6“Nimemtawaza mfalme niliyemteua,
anatawala Siyoni, mlima wangu mtakatifu!”
7Mfalme asema: “Nitatangaza azimio la Mwenyezi-Mungu.[#Taz Mate 13:33; Ebr 1:5; 5:5; #2:7 Kwanza wafalme wanasema (aya ya 3), pili Mwenyezi-Mungu anasema (aya ya 6), tatu mfalme mteule anasema (aya ya 7).]
Mungu aliniambia:
‘Wewe ni mwanangu,
mimi leo nimekuwa baba yako.
8Niombe nami nitakupa mataifa yawe urithi wako,
na dunia nzima kuwa mali yako.
9Utawaponda kwa fimbo ya chuma;[#Taz Ufu 2:26,27; 12:5; 19:15]
utawavunja kama chungu cha mfinyanzi!’”
10Sasa enyi wafalme, tumieni busara;
sikilizeni onyo hili, enyi watawala wa dunia.
11Mtumikieni Mwenyezi-Mungu kwa uchaji;
12msujudieni na kutetemeka;[#2:12 Kiebrania: Mbusuni mwana kwa kutetemeka. Lakini maana yake si dhahiri.]
asije akakasirika, mkaangamia ghafla;
kwani hasira yake huwaka haraka.
Heri yao wote wanaokimbilia usalama kwake!