The chat will start when you send the first message.
1Uniokoe, ee Mungu, kwa jina lako;
unitetee kwa nguvu yako.
2Uisikie, ee Mungu, sala yangu;
uyategee sikio maneno ya kinywa changu.
3Watu wenye kiburi wananishambulia;
wakatili wanayawinda maisha yangu,
watu ambao hawamjali Mungu.
4Najua Mungu ni msaada wangu,
Mwenyezi-Mungu hutegemeza maisha yangu.
5Yeye atawaadhibu maadui zangu kwa uovu wao wenyewe;
kwa uaminifu wako, ee Mungu, uwaangamize.
6Nitakutolea tambiko kwa moyo mkunjufu;
nitakushukuru kwa kuwa ni vema.
7Maana umeniokoa katika taabu zangu zote,
nami nimewaona maadui zangu wameshindwa.