Zekaria 9

Zekaria 9

Hukumu juu ya mataifa jirani

1Kauli ya Mwenyezi-Mungu:

Mwenyezi-Mungu ametamka siyo tu dhidi ya nchi ya Hadraki

bali pia dhidi ya Damasko.

Maana nchi ya Aramu ni mali ya Mwenyezi-Mungu,

kama vile yalivyo makabila yote ya Israeli.

2Hali kadhalika mji wa Hamathi unaopakana na Hadraki;

na hata miji ya Tiro na Sidoni

ingawaje yajiona kuwa na hekima sana.

3Mji wa Tiro umejijengea ngome kumbwa,

umejirundikia fedha kama vumbi,

na dhahabu kama takataka barabarani.

4Lakini Bwana ataichukua mali yake yote,

utajiri wake atautumbukiza baharini,

na kuuteketeza mji huo kwa moto.

5Mji wa Ashkeloni utaona hayo na kuogopa,

nao mji wa Gaza utagaagaa kwa uchungu;

hata Ekroni, maana tumaini lake litatoweka.

Mji wa Gaza utapoteza mfalme wake,

nao Ashkeloni hautakaliwa na watu.

6Mji wa Ashdodi utakaliwa na machotara.

Mwenyezi-Mungu asema hivi:

“Kiburi cha Filistia nitakikomesha.

7Nitawakomesha kula nyama yenye damu,

na chakula ambacho ni chukizo.

Mabaki watakuwa mali yangu,

kama ukoo mmoja katika Yuda.

Watu wa Ekroni watakuwa kama Wayebusi.

8Mimi mwenyewe nitailinda nchi yangu,

nitazuia majeshi yasipitepite humo.

Hakuna mtu atakayewadhulumu tena watu wangu,

maana, kwa macho yangu mwenyewe,

nimeona jinsi walivyoteseka.”

Mfalme wa amani

9Shangilieni sana enyi watu wa Siyoni!

Paazeni sauti, enyi watu wa Yerusalemu!

Tazama, mfalme wenu anawajieni,

anakuja kwa shangwe na ushindi!

Ni mpole, amepanda punda,

mwanapunda, mtoto wa punda.

10Atatokomeza magari ya vita nchini Efraimu,

na farasi wa vita kutoka mjini Yerusalemu;

pinde za vita zitavunjiliwa mbali.

Naye ataleta amani miongoni mwa mataifa;

utawala wake utaenea toka bahari hata bahari,

toka mto Eufrate hata miisho ya dunia.

Kurudishwa kwa watu wa Mungu

11Mwenyezi-Mungu asema hivi:

“Kwa sababu ya agano langu nanyi,

agano lililothibitishwa kwa damu,

nitawakomboa wafungwa wenu

walio kama wamefungwa katika shimo tupu.

12Enyi wafungwa wenye tumaini;

rudini kwenye ngome yenu.

Sasa mimi ninawatangazieni:

Nitawarudishieni mema maradufu.

13Yuda nitamtumia kama uta wangu;

Efraimu nimemfanya mshale wangu.

Ee Siyoni! Watu wako nitawatumia kama upanga

kuwashambulia watu wa Ugiriki;

watakuwa kama upanga wa shujaa.”

14Mwenyezi-Mungu atawatokea watu wake;

atafyatua mishale yake kama umeme.

Bwana Mwenyezi-Mungu atapiga tarumbeta;

atafika pamoja na kimbunga cha kusini.

15Mwenyezi-Mungu wa majeshi atawalinda watu wake,

nao watawaangamiza maadui zao.

Watapiga kelele vitani kama walevi

wataimwaga damu ya maadui zao.

Itatiririka kama damu ya tambiko

iliyomiminwa madhabahuni kutoka bakulini.

16Wakati huo, Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, atawaokoa,

maana wao ni kundi lake;

nao watang'aa katika nchi yake

kama mawe ya thamani katika taji.

17Jinsi gani uzuri na urembo wake ulivyo!

Wavulana na wasichana watanawiri

kwa wingi wa nafaka na divai mpya.

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania