1 Wafalme 11

1 Wafalme 11

Solomoni anamwasi Mungu

1Solomoni alipenda sana wanawake wa kigeni: binti Farao, wanawake wa Wamoabu, Waamoni, Waedomu, Wasidoni, na Wahiti;[#11:1-40 Sura hii inatoa picha mbaya ya Solomoni ambaye mpaka sasa amekuwa anasifika si kwa ujenzi wa hekalu bali pia kwa hekima yake. Katika aya 6 panatajwa wazi wazi kwamba Solomoni alitenda mabaya mbele ya Mwenyezi-Mungu. Solomoni alifuata miungu mingine (4-5), hakushika agano la Mungu, yaani zile Amri Kumi (aya 11), n.k. Matokeo yake yalikuwa dhahiri: kunyang'anywa utawala wake (aya 29-39).; #11:1 Wanawake hao wote walikuwa wa mataifa ya jirani na Israeli. Jambo la Solomoni kuoa wanawake wengi hivyo kwa jumla lilikuwa kwa lengo la kufanya mikataba na mataifa hayo iwe kwa ajili ya siasa au biashara (taz 1Fal 3:1 maelezo).]

2wanawake wa mataifa ambayo Mwenyezi-Mungu alikuwa amewakataza Waisraeli akisema, “Msioe kwao wala wao wasioe kwenu kwa sababu wanawake hao watapotosha mioyo yenu ili muitumikie miungu yao.” Solomoni aliwapenda sana wanawake hao.

3Solomoni akawa na wanawake 700, wote mabinti wa kifalme; na masuria 300. Hao wanawake wakampotosha.

4Maana, alipokuwa mzee, wake zake walimpotosha hata akaitumikia miungu mingine, wala hakuwa mwaminifu kabisa kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, kama baba yake Daudi alivyokuwa mwaminifu.

5Solomoni alimtumikia Ashtarothi aliyekuwa mungu wa kike wa Wasidoni, na alimfuata Milkomu chukizo la Waamoni.[#11:5 Mungu wa kike wa watu wa Kanaani. Taz Amu 2:13 maelezo.; #11:5 Milkomu ambaye anajulikana pia kama “Moleki” alikuwa mungu wa taifa la Waamoni (taz 2Fal 23:13). Mwandishi anamwita “Chukizo la Waamoni” kwa dharau. Taz pia aya 7 ambapo naye mungu Kemoshi wa Wamoabu anaitwa pia “Chukizo” (rejea Isa 66:3; Yer 4:1; Eze 5:11; 20:7-8).]

6Hivyo, Solomoni alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, wala hakufuata kwa ukamilifu matakwa ya Mwenyezi-Mungu kama baba yake Daudi alivyokuwa amefanya.

7Juu ya mlima ulio mashariki ya Yerusalemu, Solomoni alijenga mahali pa kumtambikia Kemoshi, chukizo la Wamoabu, na mahali pa kumtambikia Moleki, chukizo la Waamoni.[#11:7 Huyu alikuwa mungu wa Wamoabu; wengi wanafikiri ndiye yule ambaye mfalme wa Moabu alimtambikia mwanawe wakati alipoona anashindwa vitani (2Fal 3:26-27). Taz pia Hes 21:29 na 2Fal 23:13.]

8Kadhalika, aliwajengea wake zake wote wa kigeni mahali pa kufukizia ubani na kuitambikia miungu yao.

9Basi, Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, alimkasirikia Solomoni, kwa sababu alikuwa amemwacha Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, ingawa yeye alikuwa amemtokea mara mbili,

10na kumwamuru asiiabudu miungu ya kigeni; Solomoni hakutii amri ya Mwenyezi-Mungu.

11Kwa hiyo Mwenyezi-Mungu akamwambia Solomoni, “Kwa kuwa umeamua kufanya hivyo, ukavunja agano langu nawe, na kuasi amri zangu nilizokupa, hakika nitakunyang'anya huo utawala na kumpa mtumishi wako.

12Hata hivyo, kwa ajili ya baba yako Daudi, sitafanya hivyo maishani mwako, bali nitauondoa utawala huo mikononi mwa mwanao.

13Hata yeye sitamnyang'anya milki yote, bali nitamwachia mwanao kabila moja, kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi, na kwa ajili ya mji wa Yerusalemu ambao nimeuchagua kuwa wangu.”

Maadui wa Solomoni

14Ndipo Mwenyezi-Mungu akamfanya Hadadi aliyekuwa wa ukoo wa mfalme wa Edomu, kuwa adui ya Solomoni.[#11:14 Waisraeli waliamini kwamba Mwenyezi-Mungu ndiye aliyekuwa peke yake Mungu, na kwamba alikuwa na mamlaka juu ya vitu vyote na hata watawala wa dunia kama huyu Hadadi.]

15Wakati Daudi alipowaangamiza Waedomu Yoabu, mkuu wa jeshi la Daudi, alikwenda huko kuwazika waliouawa. Yoabu aliwaua wanaume wote wa Edomu.[#11:15 Eneo hili lilikuwa kusini mwa Bahari ya Chumvi. Waedomu walikuwa na ujamaa na Waisraeli kwa sababu walikuwa wazawa wa ndugu yake Yakobo, yaani Esau (taz Mwa 25:24-26). Mara kwa mara Waedomu wanaelezwa katika Biblia kama maadui wa Waisraeli.]

16(Yoabu alikaa huko na wanajeshi wake kwa muda wa miezi sita, apate kuwaangamiza kabisa wanaume wote wa Edomu.)

17Lakini Hadadi ambaye wakati huo alikuwa kijana alitorokea Misri pamoja na Waedomu kadhaa, watumishi wa baba yake.

18Hadadi na wenzake walisafiri kutoka Midiani, wakawachukua watu wengine huko Parani, wakaenda nao mpaka Misri, kwa Farao mfalme wa nchi hiyo. Farao akampatia Hadadi nyumba, akaamuru awe akipewa chakula, akampa na ardhi.

19Farao alipendezwa sana na Hadadi. Hivyo Farao akamruhusu shemeji yake, mdogo wa malkia Tapenesi, aolewe na Hadadi.

20Huyo dada wa Tapenesi akamzalia Hadadi mwana aliyeitwa Genubathi. Genubathi alilelewa na Tapenesi katika nyumba ya Farao, pamoja na wana wa mfalme.

21Lakini Hadadi aliposikia huko Misri kwamba Daudi na Yoabu mkuu wa jeshi, walikuwa wamefariki, alimwambia Farao, “Uniruhusu niondoke nirudi nchini kwangu.”

22Lakini Farao akamwuliza, “Nimekunyima nini hata uamue sasa kurudi nchini kwako?” Naye Hadadi akamsihi akisema, “Uniache tu niende.”

23Vilevile, Mungu alimfanya Rezoni mwana wa Eliada, awe adui ya Solomoni. Rezoni alikuwa amemtoroka bwana wake, mfalme Hadadezeri wa Soba.[#11:23-25 Rejea 2Sam 8:3-8; 10:15-19. Kuanzishwa kwa ufalme wa Rezoni kule Damasko, eneo ambalo lilikuwa chini ya mamlaka ya Daudi hapo awali, ilikuwa ni dalili ya kusambaratika kwa utawala wake.]

24Baada ya Daudi kufanya mauaji huko Soba, Rezoni alikusanya watu na kuunda genge la maharamia, naye mwenyewe akawa kiongozi wao. Basi, wakaenda Damasko, wakakaa huko na kumfanya Rezoni mfalme wa Damasko.

25Rezoni alikuwa adui wa Israeli siku zote za utawala wa Solomoni, akamsumbua sana Solomoni kama naye Hadadi alivyomsumbua. Basi, Rezoni aliidharau Israeli, naye alitawala nchi ya Aramu.

Ahadi ya Mungu kwa Yeroboamu

26Yeroboamu mwana wa Nebati, Mwefraimu wa Sereda, mtumishi wa Solomoni, ambaye mama yake mjane, aliitwa Zerua, pia alimwasi mfalme.[#11:26 Huyu atakuwa mfalme wa makabila kumi ya Waisraeli upande wa kaskazini wa utawala wa Daudi (taz 11:31-32).]

27Kisa cha uasi huo ni hiki: Solomoni alipokuwa akishughulika na kusawazisha sehemu ya Milo, na kuimarisha kuta za mji wa baba yake Daudi,

28Yeroboamu alionekana kuwa kijana hodari na shujaa. Ndipo Solomoni alipoona kwamba huyo kijana alikuwa mwenye bidii, akamweka awe msimamizi wa kazi za kulazimishwa zilizofanywa na watu wa ukoo wa Yosefu.[#11:28 Yaani makabila ya Efraimu na Manase. Taz Yos 16:1 maelezo.]

29Siku moja, Yeroboamu alipokuwa akisafiri kutoka Yerusalemu, nabii Ahiya wa Shilo alikutana naye njiani. Ahiya alikuwa amevaa vazi jipya. Wote wawili walikuwa peke yao mashambani.

30Mara, Ahiya akalivua vazi lake jipya, akalirarua vipande kumi na viwili,[#11:29-30 Mara kwa mara manabii walitumia vitendo kuonesha ukweli wa mambo ambayo Mungu alikusudia kutenda (taz pia 1Sam 15:27-28; 1Fal 22:10-11; Eze 4; 37:15-28). Kwamba vazi hili lilikuwa jipya huenda ni njia mojawapo ya kuonesha kwamba kitendo hicho ni lazima kitukie.]

31halafu akamwambia Yeroboamu, “Jitwalie vipande kumi maana Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, asema hivi: ‘Tazama, karibu nitaurarua ufalme na kuuondoa mikononi mwa Solomoni, nami nitakupa wewe makabila kumi.’

32Lakini yeye nitamwachia kabila moja kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi, na kwa ajili ya mji wa Yerusalemu ambao nimeuchagua kuwa wangu katika makabila yote ya Israeli.[#11:31-32 Makabila kumi ni yale ya kaskazini ambayo yalijulikana pia kama “Israeli”; lakini kuhusu hilo kabila moja analoachiwa Solomoni yafaa kukumbuka kwamba kabila la Simeoni wakati huo lilikwisha kuwa sehemu ya kabila la Yuda. Mungu anararua huo utawala wa Solomoni lakini kwa kumwachia kabila moja, kabila la Yuda, inaonekana kwamba bado ni mwaminifu kwa ile ahadi aliyompa Daudi (taz aya 33-39). Tafsiri ya kale ya Kigiriki ya Septuajinta (LXX) ina makabila mawili badala ya kabila moja.]

33Nitafanya hivyo kwa sababu Solomoni ameniacha, akaabudu miungu ya kigeni: Ashtarothi mungu wa kike wa Wasidoni, Kemoshi, mungu wa Wamoabu na Milkomu mungu wa Waamoni. Solomoni ameniasi, ametenda maovu mbele yangu, na wala hakutii sheria zangu na maagizo yangu kama Daudi baba yake alivyofanya.

34Hata hivyo, sitamnyang'anya milki yote, wala sitamwondolea mamlaka maishani mwake, kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi ambaye nilimchagua, na ambaye alifuata amri zangu na maongozi yangu.

35Lakini, nitamnyang'anya mwanawe ufalme huo, nami nitakupatia wewe Yeroboamu makabila kumi.

36Huyo mwanawe Solomoni nitamwachia kabila moja, ili wakati wote mzawa wa mtumishi wangu Daudi awe anatawala Yerusalemu, awe taa inayoangaza daima mbele yangu katika mji ambao nimeuchagua uwe mahali pa kuniabudia.

37Basi, wewe Yeroboamu, nitakufanya kuwa mfalme wa Israeli, nawe utatawala kama upendavyo.

38Na kama utazingatia yote nitakayokuamuru, kama utaishi kulingana na matakwa yangu, kama utatenda mema mbele zangu kwa kushika maongozi yangu na amri zangu, kama mtumishi wangu Daudi alivyofanya, mimi nitakuwa pamoja nawe daima. Na nitakupatia nchi ya Israeli na kuufanya utawala wako uwe thabiti kama nilivyomfanyia Daudi.[#11:37-38 Ahadi ya Mungu kwa Yeroboamu karibu ni sawa na ile aliyopewa Daudi na pia Solomoni (2Sam 7:8-16; na 1Fal 3:14).]

39Kutokana na hayo, nitawaadhibu wazawa wa Daudi, lakini si daima.”

40Kwa sababu hiyo, Solomoni alijaribu kumuua Yeroboamu; lakini Yeroboamu akakimbilia Misri kwa Shishaki mfalme wa Misri, akakaa huko mpaka Solomoni alipofariki.

Kifo cha Solomoni

(2 Nya 9:29-31)

41Mambo mengine ya Solomoni, yote aliyotenda na hekima yake, yameandikwa katika Kitabu cha Matendo ya Solomoni.[#11:41 Karibu kila mfalme aliyetawala alikuwa na makarani ambao walifanya kazi ya kuandika mambo wafalme waliyotenda na matukio mbalimbali. Hao waandishi walikuwa wanahistoria wa nyakati hizo. Katika 2Nya 9:29 mwandishi anasema kuwa matendo ya Solomoni yaliandikwa katika kitabu cha historia ya Nabii Nathani na katika Maono ya Ido mwonaji.]

42Kwa muda wa miaka arubaini, Solomoni aliitawala nchi yote ya Israeli; makao yake yakiwa Yerusalemu.[#11:42 Muda wa ufalme wa Solomoni ni sawa na ule wa Daudi (1Fal 2:11), yaani miaka arubaini. Jambo hili limewafanya wengi kufikiri kwamba idadi hiyo ya arubaini ni idadi ya jumla na sio kamili. Taz Amu 3:11 maelezo.]

43Hatimaye, Solomoni alifariki, akazikwa katika mji wa baba yake Daudi. Rehoboamu, mwanawe Solomoni, akatawala mahali pake.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania