The chat will start when you send the first message.
1Daudi alikwenda kwa kuhani Ahimeleki huko Nobu. Ahimeleki akatoka kumlaki huku akiwa anatetemeka, akamwuliza, “Kwa nini umekuja hapa peke yako?”[#21:1-6 Mat 12:3-4; Marko 2:25-26; Luka 6:3-4. Yesu anakitaja kisa hiki kuonesha kwamba sheria fulani za kidini zina vipengee vyake, lakini zinapaswa kuwa kwa ajili ya kuhifadhi uhai (taz pia Luka 6:9-11).; #21:1 Mji huu ulikuwa katika eneo au nchi ya Benyamini (Isa 10:32), kaskazini-magharibi ya Yerusalemu.; #21:1 Alikuwa mmoja wa wazawa wa kuhani Eli (1Sam 22:9; rejea 14:3).]
2Daudi akamjibu, “Niko hapa kutokana na amri ya mfalme. Aliniambia nisimweleze mtu yeyote juu ya kile ambacho amenituma. Nimeagana na watu wangu kwamba tukutane mahali fulani.
3Je, una kitu chochote? Nakuomba mikate mitano au chochote kilichoko.”
4Kuhani Ahimeleki akamwambia, “Hapa sina mkate wa kawaida. Ninayo tu ile mikate mitakatifu. Mnaweza kupewa mikate hiyo ikiwa watu wako hawajalala na wanawake hivi karibuni.”[#21:4 Lawi 24:5-9; rejea Marko 2:23-28 na sehemu sambamba. Mikate hii pengine inaitwa “mikate ya wonesho” au “mikate iliyowekwa mbele ya Mungu”. Mikate hiyo iliwekwa mahali pa ibada kila juma kama njia ya kumshukuru Mungu kwa kuwapatia watu mkate kwa chakula. Mwishoni mwa juma iliondolewa na mahali pake pakawekwa mikate mipya. Ni makuhani tu ndio walioruhusiwa kula mikate hiyo.; #21:4 Kujamiiana ilikuwa kitendo ambacho kilimzuia mtu kushiriki mambo ya dini kwa muda (taz Kut 19:15; Lawi 15:18); taz pia 1Sam 16:5 maelezo.]
5Daudi akamwambia, “Kwa hakika, daima ninapokwenda kwa ajili ya shughuli maalumu, wanawake wamekuwa mbali nasi! Ikiwa miili ya vijana wangu ni mitakatifu tuwapo kwenye shughuli za kawaida, je, si zaidi katika shughuli hii maalumu?”
6Hivyo kuhani Ahimeleki akampa mikate mitakatifu, kwani hapakuwa na mikate mingine isipokuwa hiyo ya kuwekwa mbele ya Mwenyezi-Mungu, ikabadilishwa na mikate mipya kutoka mekoni.
7Basi kulikuwa hapo siku hiyo mtumishi mmoja wa Shauli ambaye alikuwa amezuiliwa mbele ya Mwenyezi-Mungu. Mtumishi huyo aliitwa Doegi, Mwedomu, msimamizi wa wachungaji wa Shauli.
8Basi, Daudi akamwambia Ahimeleki, “Je, una upanga au mkuki ambao unaweza kunipatia? Kwa kuwa shughuli za mfalme zilinilazimu niondoke haraka, nami niliondoka bila upanga wangu wala silaha nyingine yoyote.”
9Ahimeleki akamjibu, “Ninao ule upanga wa Mfilisti Goliathi uliyemuua kwenye bonde la Ela; uko nyuma ya kizibao cha kuhani umefungwa katika kitambaa. Ikiwa unataka kuuchukua huo basi, uchukue kwani hakuna upanga mwingine hapa.” Daudi akamwambia, “Hakuna upanga mwingine kama huo; nakuomba unipe.”[#21:9 Taz 2:28. Jina hili hutaja kwa wingi sana mojawapo ya vazi la kuhani ambalo aghalabu lilikuwa na kifuko chenye vitu viwili au mawe mawili ya kujua matakwa ya Mungu. Lakini hapa si dhahiri kwamba yahusu vazi hilo. Wengine wanafikiri ilikuwa tu namna ya kinyago kama kile cha Gideoni (Amu 8:27). Taz pia Kut 28:6.]
10Siku hiyo, Daudi alimkimbia Shauli, akaenda kwa mfalme Akishi wa Gathi.
11Watumishi wa mfalme wakamwambia Akishi, “Huyu si Daudi, mfalme wa nchi ya Israeli? Je, si huyu ambaye walikuwa wakiimbiana juu yake katika ngoma, wakisema, ‘Shauli ameua maelfu yake na Daudi ameua makumi elfu yake?’”
12Maneno hayo Daudi hakuweza kuyasahau, akaanza kumwogopa sana Akishi mfalme wa Gathi.[#21:12 Taz Zab 56 (Maneno yanayotangulia Zaburi yenyewe au “kichwa cha Zaburi” katika Kiebrania).]
13Hivyo, akabadilisha tabia yake, akijifanya mwendawazimu, akawa anakwaruzakwaruza kwenye malango ya mji, na mate yake akayaacha yatiririke kwenye ndevu zake.[#21:13 Taz Zab 34 (Maneno yanayotangulia Zaburi yenyewe au “kichwa cha Zaburi” katika Kiebrania).]
14Akishi akawaambia watumishi wake, “Mnajua kuwa mtu huyu ni mwendawazimu; kwa nini mmemleta kwangu?
15Je, nawahitaji wendawazimu zaidi? Kwa nini mnaniletea mwendawazimu aje kunisumbua na vitendo vya wendawazimu? Je, mtu huyu ataingia nyumbani kwangu?”