The chat will start when you send the first message.
1Baadhi ya wanaume kutoka mji wa Zifu walimwendea Shauli huko Gibea wakamwambia kwamba Daudi alikuwa anajificha kwenye mlima Hakila, upande wa mashariki wa Yeshimoni.[#26:1 Huu ulikuwa mji wake Shauli na makao yake makuu (taz 10:3-5).; #26:1 Hii ni mara ya pili watu wa Zifu kumsaliti Daudi. Taz Zab 54 Maneno yanayotangulia Zaburi yenyewe au “kichwa cha Zaburi” katika Kiebrania; “Mara ya pili” taz 23:19.]
2Mara moja, Shauli alikwenda kwenye nyika za Zifu kumtafuta Daudi akiwa na askari waliochaguliwa 3,000 wa Israeli.
3Shauli akapiga kambi juu ya mlima Hakila, karibu na barabara, mashariki ya Yeshimoni. Lakini Daudi alikuwa bado huko nyikani. Daudi alipojua kwamba Shauli alikuwa amekuja nyikani kumtafuta,
4alituma wapelelezi, akafahamishwa kwamba ni kweli.
5Daudi akatoka, akaenda mahali Shauli alipopiga kambi. Akapaona mahali ambapo Shauli alikuwa amelala na Abneri mwana wa Neri, kamanda wa jeshi la Shauli, alikuwa amelala karibu na Shauli. Shauli alikuwa amelala katikati ya kambi huku akizungukwa na jeshi lake.
6Daudi akamwambia Ahimeleki ambaye alikuwa, Mhiti, na Abishai ndugu yake Yoabu (mama yao aliitwa Seruya), “Nani atakwenda pamoja nami kwenye kambi ya Shauli?” Abishai akamwambia; “Mimi nitakwenda pamoja nawe.”[#26:6 Huyu si yule Ahimeleki ambaye ni kuhani (21:1). Wahiti walitoka eneo ambalo sasa ni nchi ya Uturuki. Hao walivamia na kuteka karibu eneo lote la Mashariki ya Kati ya Kale mnamo 1600 na 1200 K.K. Wahiti wengine walifanya makao yao katika maeneo ambayo baadaye yalikuwa ya Waisraeli (Mwa 23:3; Hes 13:29; Yos 1:4). Wachache waliobaki wakati wa Waisraeli walichukua majina ya Kiisraeli na kujumlishia hapo majina ya Kihiti.; #26:6 Abishai na Yoabu walikuwa watoto wa mama mmoja aitwaye Seruya. Na huyu Seruya alikuwa dada mkubwa wa Daudi; hivyo Abishai na Yoabu walikuwa mabinamu wa Daudi. (Taz 1 Nya 2:12-17 na 2Sam 17:25). Yoabu alikuwa kamanda wa majeshi ya Daudi kwa muda mrefu.]
7Hivyo usiku, Daudi na Abishai wakaingia kwenye kambi ya Shauli, wakamkuta Shauli amelala katikati ya kambi hiyo, na mkuki wake umechomekwa ardhini karibu na kichwa chake. Abneri pamoja na askari walikuwa wamelala kumzunguka Shauli.
8Abishai akamwambia Daudi, “Leo Mungu amemtia adui yako mikononi mwako. Basi, niache nimbane udongoni kwa pigo moja tu la mkuki; sitampiga mara mbili.”
9Lakini Daudi akamwambia Abishai, “Usimwangamize; maana hakika Mwenyezi-Mungu atamwadhibu mtu yeyote atakayeunyosha mkono wake dhidi ya mteule wake aliyepakwa mafuta.
10Naapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai, kwamba Mwenyezi-Mungu mwenyewe atamuua Sauli; ama siku yake ya kufa itafika, au atakwenda vitani na kufia huko.
11Lakini Mwenyezi-Mungu anakataza nisinyoshe mkono wangu dhidi ya mtu ambaye amemteua kwa kumpaka mafuta. Lakini chukua mkuki wake ulio karibu na kichwa chake pamoja na gudulia lake la maji, halafu tujiendee zetu.”[#26:11 Baadaye, Daudi atavitumia vitu hivi vya binafsi vya Shauli kuonesha kwamba angaliweza kuua mfalme Shauli na kutawala mahali pake (26:16), sawa kabisa kama lile tukio la kukata vazi lake (24:11).]
12Hivyo, Daudi alichukua ule mkuki na gudulia la maji karibu na kichwa cha Shauli nao wakajiendea zao. Lakini hakuna mtu aliyeona au kujua tukio hilo, wala hakuna aliyeamka, kwa kuwa Mwenyezi-Mungu aliwaletea usingizi mzito.
13Kisha, Daudi akaenda upande wa pili wa bonde hilo, akasimama juu mlimani mbali na kundi la Shauli.
14Akaliita kwa sauti jeshi la Shauli na Abneri mwana wa Neri akisema, “Abneri, je, unanisikia?” Abneri akauliza, “Ni nani wewe unayemwita mfalme?”
15Daudi akamjibu, “Je, wewe si mwanamume? Nani aliye sawa nawe katika Israeli? Mbona basi, hukumlinda bwana wako mfalme? Mtu mmoja wetu aliingia hapo kumwangamiza bwana wako mfalme!
16Ulilotenda si jambo jema. Ninaapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai, kwamba unastahili kufa, kwa kuwa hukumlinda bwana wako, ambaye Mwenyezi-Mungu amempaka mafuta. Sasa hebu angalia, mkuki wa mfalme na lile gudulia la maji lililokuwa karibu na kichwa chake kama vipo!”
17Shauli alitambua sauti ya Daudi, akamwuliza, “Je, hiyo ni sauti yako mwanangu Daudi?” Daudi akamjibu, “Bwana wangu, mfalme, ni sauti yangu.”[#26:17 Kusema kweli Daudi hakuwa mwanawe Shauli. Lakini mtindo huu wa kusema ni sawa na ule wa 24:16 (labda namna ya kujisingizia kwamba kuna uhusiano wa upendo kati yake na Daudi, jambo ambalo hutokea wakati mtu anapofikia hali ngumu).]
18Halafu akaendelea kusema, “Lakini kwa nini, wewe bwana wangu unifuatilie mimi mtumishi wako? Nimefanya nini? Ni ovu gani nimekufanyia?
19Basi, sasa bwana wangu mfalme, usikie maneno ya mtumishi wako. Ikiwa Mwenyezi-Mungu ndiye aliyekuchochea uje dhidi yangu, basi, na apokee tambiko itakayomfanya abadili nia yake. Lakini kama ni watu, basi, Mwenyezi-Mungu na awalaani watu hao kwani wamenifukuza kutoka urithi aliotupa Mwenyezi-Mungu wakisema, ‘Nenda ukaitumikie miungu mingine.’[#26:19 Katika fikira za watu wa nyakati hizo, kulikuwa na uhusiano au umoja kati ya taifa au watu, nchi yao na mungu wao. Na mtu akifukuzwa kutoka nchi yake amefukuzwa pia mbali na mungu wa nchi hiyo na kwenda kwa mungu mwingine.]
20Usiniache nife katika nchi ya kigeni, mbali na Mwenyezi-Mungu. Kwa nini wewe mfalme wa Israeli umetoka kuyatafuta maisha yangu kama mtu anayewinda kware milimani?”
21Ndipo Shauli akajibu, “Mimi nimefanya makosa. Rudi mwanangu Daudi. Sitakudhuru tena kwa kuwa leo maisha yangu yalikuwa ya thamani mbele yako. Mimi nimekuwa mpumbavu na nimekosa vibaya sana.”
22Daudi akajibu, “Ee mfalme, mkuki wako uko hapa, mtume kijana wako mmoja aje auchukue.
23Mwenyezi-Mungu humtunza kila mtu kwa uadilifu na uaminifu wake. Leo Mwenyezi-Mungu alikutia mikononi mwangu, lakini mimi sikunyosha mkono wangu dhidi yako kwa kuwa wewe umeteuliwa naye kwa kutiwa mafuta.
24Tazama kama vile leo maisha yako yalivyokuwa na thamani mbele yangu, ndivyo na maisha yangu yawe na thamani mbele ya Mwenyezi-Mungu; naye akaniokoe kutoka kwenye taabu zote.”
25Shauli akamwambia Daudi, “Mungu na akubariki mwanangu Daudi. Utafanya mambo makuu, nawe utafanikiwa katika yote.” Basi, Daudi akaenda zake; Shauli naye akarudi nyumbani kwake.