1 Samueli 5

1 Samueli 5

Sanduku la agano kati ya Wafilisti

1Baada ya Wafilisti kuliteka sanduku la Mungu, walilibeba kutoka mji wa Ebenezeri hadi mji wao wa Ashdodi.

2Kisha, wakalipeleka sanduku la Mwenyezi-Mungu kwenye hekalu la mungu wao Dagoni na kuliweka karibu naye.[#5:2 Huyu alikuwa mungu maarufu kuliko miungu yote ya Wafilisti na alikuwa mungu wa mvua na rutuba. Awali aliabudiwa kule Mesopotamia laini yapata 2000 K.K. alijulikana karibu kila mahali katika Mashariki ya Kati ya Kale.]

3Kesho yake asubuhi, watu wa mji wa Ashdodi walipoamka waliona sanamu ya Dagoni imeanguka kifudifudi mbele ya sanduku la Mungu. Wakaisimamisha tena sanamu ya Dagoni na kuiweka tena mahali pake.

4Lakini, kesho yake asubuhi walipoamka, waliona kuwa sanamu ya Dagoni imeanguka kifudifudi mbele ya sanduku la Mwenyezi-Mungu, kichwa, miguu na mikono ya sanamu hiyo, vyote vilikuwa vimekatika, vikawa vimelala chini kwenye kizingiti cha mlango. Kiwiliwili cha sanamu ya Dagoni ndicho tu kilikuwa kimebakia.

5Ndio maana makuhani wa Dagoni na wote wanaoingia kumwabudu Dagoni huko Ashdodi, wanapoingia kwenye hekalu la Dagoni hawakanyagi kizingiti cha hekalu la Dagoni hadi leo.[#5:5 Hapa mwandishi anaeleza desturi ya ajabu ya wakati huo na ambayo sasa yamkini haieleweki.]

6Mwenyezi-Mungu aliwaadhibu vikali na kuwatisha watu wa Ashdodi. Aliwaadhibu, hata na majirani zao, kwa kuwaletea ugonjwa wa majipu.[#5:6 Au: “ugonjwa wa tauni” ambao huenezwa na panya (taz 6:4-5 ambapo Wafilisti wanawakilisha hali hiyo kwa kupeleka vinyago vya panya).]

7Wakazi wa Ashdodi walipoyaona mambo yaliyowapata, wakasema, “Mungu wa Israeli anatuadhibu vikali sisi pamoja na mungu wetu Dagoni. Sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu haliwezi kukaa kwetu.”

8Walituma wajumbe na kuwakusanya wakuu wote wa Wafilisti na kuwauliza, “Je, tutafanya nini na sanduku hili la Mungu wa Israeli?” Wakuu wao wakajibu, “Sanduku hilo la Mungu wa Israeli lipelekeni Gathi.” Basi, wakalipeleka kwenye mji wa Gathi.

9Lakini baada ya kulipeleka huko Gathi, Mwenyezi-Mungu akauadhibu mji huo, akisababisha hofu kuu mjini, na akawapiga wanaume wa mji huo, vijana kwa wazee, kwa kuwaletea majipu.

10Hivyo, wakalipeleka sanduku hilo la Mungu kwenye mji wa Ekroni. Lakini sanduku hilo la Mungu lilipofika huko, watu wa mji huo walipiga kelele, “Wametuletea sanduku la Mungu wa Israeli ili kutuua sisi na watu wetu.”[#5:8-10 Hapa panatajwa miji miwili “Gathi” na “Ekroni” ambayo ni mojawapo ya miji mitano mikuu ya Wafilisti. Jina “Gathi” lina maana ya “mahali pa kusindikia zabibu”.]

11Kisha wakatuma ujumbe na kukusanya wakuu wa Wafilisti na kuwaambia, “Lirudisheni sanduku la Mungu wa Israeli mahali pake, ili lisituue sisi pamoja na watu wetu.” Walifanya hivyo kwa sababu kulikuwa na hofu kubwa katika mji mzima kwa sababu Mungu alikuwa anawaadhibu vikali.

12Nao wale ambao hawakufa walipatwa na majipu hata kilio cha mji kilifika mbinguni.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania