The chat will start when you send the first message.
1Msemo huu ni wa kweli: mtu anayetaka kuwa askofu, huyo anatamani kazi nzuri.[#3:1 Taz 1Tim 1:15.; #3:1 Tazama Fil 1:1. Katika barua zinazojulikana kama za kichungaji majukumu ya wenye kuuongoza kanisa au jumuiya ya waumini yanatiliwa mkazo. Tazama pia Tito 1:6-9. Katika Agano Jipya kuna majina tofauti yanayowataja hao viongozi: “askofu” au msimamizi mkuu (Kigiriki: “episkopos”); “wazee” (Kigiriki’ “presbuteros”); “wasaidizi” (Kigiriki: “diakonoi), n.k.; #3:1-16 Aya 7 za kwanza za sura hii zahusu maagizo kwa maaskofu au wenye kuongoza kanisa la Mungu (3:1-7), hali sura zilizobakia (3:8-16) zahusu tabia na majukumu ya wale wanaoitwa wasaidizi katika kanisa.]
2Basi, askofu anapaswa kuwa mtu asiye na lawama; anapaswa awe na mke mmoja tu, awe mwenye kiasi, nidhamu na utaratibu; ni lazima awe mkarimu na anayeweza kufundisha;[#3:2 Tazama pia 1Tim 5:9 ambapo kama kuna uhusiano na namna hiyo ya kufikiri, maana ya agizo hili ni kwamba askofu awe mtu aliyepata kuoa mara moja tu, jambo ambalo linaipa ndoa sifa yake ya pekee. Baadhi wanafikiri hapa yahusu “kuwa mwaminifu kwa mkewe”.; #3:2 Tabia njema iliyo muhimu sana kwa jumuiya ya kwanza ya Wakristo (taz Rom 12:13 maelezo), na huenda ilihusu kuwa tayari kuwakaribisha waumini nyumbani kwake kwa ajili ya mikutano ya Kanisa (taz pia Rom 16:5 maelezo; rejea Kol 4:15; File 2).]
3asiwe mlevi au mtu wa matata, bali awe mpole, apendaye amani; asiwe mtu wa kupenda fedha;
4anapaswa awe mtu awezaye kuongoza vema nyumba yake, na kuwafanya watoto wake wawe watii kwa heshima yote.
5Maana kama mtu hawezi kuongoza vema nyumba yake, atawezaje kulitunza kanisa la Mungu?
6Mtu ambaye hajakomaa bado katika imani asifanywe kuwa kiongozi katika kanisa, asije akajaa majivuno na kuhukumiwa kama vile Ibilisi alivyohukumiwa.
7Anapaswa awe mwenye sifa njema kati ya watu walio nje ya kanisa, ili asije akalaumiwa na kuanguka katika mtego wa Ibilisi.
8Wasaidizi katika kanisa wanapaswa pia kuwa watu wenye tabia njema na wanyofu; wasiwe wanywaji mno wa divai au wenye tamaa ya fedha;[#3:8-13 Kuhusu sifa zinazotakiwa kwa wengine wenye madaraka katika Kanisa taz 1Tim 3:1-7, na Tito 1:6-9. Neno msaidizi (wasaidizi) limetumika kutafsiri Kigiriki “diakonos” neno ambalo linatumika kumtaja mtu ambaye anatumikia. Mwanzoni mwa Kanisa watu wa namna hiyo walikuwa wasaidizi wa wale walioliongoza au waliolisimamia Kanisa (aya ya 1).]
9wanapaswa kuzingatia kwa dhamiri njema ukweli wa ndani wa imani.[#3:9 Au, “siri ya imani”. Rejea aya ya 16. Maneno hayo yanatumika kueleza ukweli wa Injili, ukweli ambao hapo kwanza haukuwa umedhihirishwa lakini sasa umefunuliwa na Mungu (taz pia Efe 1:9 maelezo; rejea pia 1Kor 2:7-10; Kol 1:25-27; 2:2-3).]
10Ni lazima kwanza wathibitishwe, na wakionekana kuwa wanafaa, basi, watoe huduma yao.
11Wake zao wanapaswa pia kuwa na tabia njema, wasiowasengenya watu, wenye kiasi na waaminifu katika mambo yote.
12Msaidizi katika kanisa lazima awe na mke moja tu, na awezaye kuongoza vema watoto wake na nyumba yake.[#3:12 Taz 3:2 maelezo.]
13Maana wasaidizi wanaofanya kazi yao vizuri hujipatia msimamo mzuri, na wanaweza kusema bila hofu juu ya imani yao katika Kristo Yesu.
14Ninakuandikia barua hii nikiwa na matumaini ya kuja kwako hivi karibuni.
15Lakini kama nikicheleweshwa, basi, barua hii itakufahamisha mwenendo tunaopaswa kuwa nao katika nyumba ya Mungu, ambayo ni kanisa la Mungu aliye hai, na ambalo ni nguzo na msingi wa ukweli.
16Hakuna mashaka yoyote juu ya ukuu wa siri ya dini yetu:
Alionekana katika umbo la kibinadamu,
alithibitishwa na Roho kuwa ni mwadilifu,
akaonekana na malaika.
Alihubiriwa kati ya mataifa,
aliaminiwa ulimwenguni,
akachukuliwa juu katika utukufu.