2 Wafalme 1

2 Wafalme 1

Elia na mfalme Ahazia

1Baada ya kifo cha Ahabu, watu wa Moabu waliasi wasitawaliwe na Israeli.[#1:1 Ahabu alikuwa mfalme wa saba wa Israeli. Alitawala tangu 874-853 K.K. (1Fal 22:29-40). Mtoto wake, Ahazia, alitwala baada yake.; #1:1 Habari za uasi wa Wamoabu dhidi ya Ahazia ziko katika 2Fal 3:4-27.]

2Mfalme Ahazia alipokuwa Samaria alianguka kutoka chumba kilichokuwa paani mwa nyumba yake, akaumia vibaya. Kwa hiyo akawatuma wajumbe, akawaambia, “Nendeni kwa Baal-zebubu, mungu wa mji wa Ekroni, mkamwulize kama nitapona ugonjwa huu.”[#1:2 Jina hili lina maana ya “Bwana wa nzi”, jina ambalo yamkini lilitumiwa na watu waliomwabudu Baali kumtaja mungu wa dhoruba ambaye alikuwa na uwezo wa kuthibiti magonjwa yaliyosababishwa na nzi. Wengine wanafikiri jina hili lilitumiwa kwa kudharau “Baalzebuli” ambalo ni jina la mungu wa watu wa Kanaani. Aliabudiwa hasa mjini Ekroni, moja ya miji mikubwa mitano ya Wafilisti. Katika A.J., jina linalofanana na hili ni “Beelzebuli” ambalo linatumiwa kumtaja Shetani (Mat 12:24; Marko 3:22; Luka 11:15).]

3Lakini malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwambia nabii Elia kutoka Tishbe, aende kukutana na wajumbe hao na kuwauliza, “Kwa nini mnakwenda kwa Baal-zebubu, mungu wa Ekroni? Je, hakuna Mungu nchini Israeli?[#1:3 Taz Mwa 16:7 maelezo; Kut 3:2 maelezo.; #1:3 Jina “Elia” lina maana ya “Mungu wangu ni Mwenyezi-Mungu”. Huyu alipigania ibada ya kweli kwa Mwenyezi-Mungu dhidi ya Ahabu na mkewe Yezebeli ambao waliwatia moyo Waisraeli wamwabudu Baali (1Fal 17—22). Aliwapa watu ujumbe wa Mungu mnamo karne ya tisa K.K. Baadaye Wayahudi wengi walitazamia kwamba angerudi kumtayarishia Masiha njia yake (Malaki 4:1-6; Mat 17:10-11; Marko 9:11-12).]

4Mwambieni mfalme kwamba Mwenyezi-Mungu amesema hivi: ‘Hutashuka katika kitanda ulichokipanda; hakika utakufa!’”

5Basi, Elia akawaendea. Wale wajumbe wakarudi kwa mfalme, naye akawauliza, “Mbona mmerudi?”

6Wakamjibu, “Tumekutana na mtu ambaye alitutuma turudi kukuambia kwamba Mwenyezi-Mungu amesema hivi: ‘Kwa nini unatuma wajumbe kwa Baal-zebubu, mungu wa Ekroni? Je, hakuna Mungu nchini Israeli? Hutashuka katika kitanda ulichokipanda; bali hakika utakufa!’”

7Mfalme akauliza, “Ni mtu gani huyo aliyekutana nanyi na kuwaambieni mambo hayo?”

8Wao wakamjibu, “Alikuwa amevaa vazi la manyoya na mshipi wa ngozi kiunoni.” Mfalme akasema, “Huyo ni Elia kutoka Tishbe!”[#1:8 Kadiri ya Zek 13:4 na Mat 7:15 manabii kwa desturi walivaa mavazi yasiyo ya kawaida. Ndivyo pia alivyovaa Yohane Mbatizaji (Mat 3:4; Marko 1:6).]

9Hapo mfalme akamtuma kapteni mmoja na watu wake hamsini wamlete Elia. Kapteni huyo akamkuta Elia ameketi mlimani, akamwambia, “Ewe mtu wa Mungu, mfalme anakuamuru ushuke.”[#1:9 Yamkini yahusu Mlima Karmeli.]

10Elia akamjibu huyo kapteni wa watu hamsini, “Kama mimi ni mtu wa Mungu, moto na ushuke kutoka mbinguni na kukuteketeza wewe pamoja na watu wako!” Mara moto ukashuka kutoka mbinguni, ukamteketeza pamoja na watu wake hamsini.

11Mfalme akamtuma kapteni mwingine na watu wake hamsini wamlete Elia. Naye akapanda juu akamwambia Elia, “Ewe mtu wa Mungu, mfalme anakuamuru ushuke mara moja!”

12Elia akamjibu, “Kama kweli mimi ni mtu wa Mungu, moto na ushuke kutoka mbinguni, ukuteketeze wewe pamoja na watu wako!” Papo hapo moto wa Mungu ukashuka kutoka mbinguni, ukamteketeza pamoja na watu wake hamsini.

13Kwa mara nyingine tena, mfalme akatuma kapteni mwingine na watu wake hamsini. Kapteni wa tatu akapanda mlimani, akapiga magoti mbele ya Elia na kumsihi akisema, “Ewe mtu wa Mungu, nakusihi uyathamini maisha yangu, na ya watu wako hawa, usituangamize!

14Maofisa wawili waliotangulia na watu wao, wameteketezwa na moto ulioshuka kutoka mbinguni; lakini sasa nakuomba uyahurumie maisha yangu.”

15Hapo malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwambia Elia, “Shuka pamoja naye, wala usimwogope.” Basi, Elia akainuka, akashuka pamoja naye mpaka kwa mfalme,

16akamwambia, “Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Kwa sababu ulituma wajumbe kumtaka shauri Baal-zebubu, mungu wa Ekroni — kana kwamba hapakuwa na Mungu katika Israeli ambaye ungemwomba shauri — basi, hutashuka katika kitanda ulichopanda; hakika utakufa.’”

17Baadaye Ahazia akafariki kama Mwenyezi-Mungu alivyomwambia nabii wake Elia. Na, kwa kuwa Ahazia hakuwa na mtoto wa kiume, Yoramu akawa mfalme mahali pake, katika mwaka wa pili wa utawala wa Yehoramu mwana wa Yehoshafati, mfalme wa Yuda.[#1:17 Makala ya Kiebrania ina “Yehoramu”. Huyu alikuwa ndugu yake Ahazia.]

18Mambo mengine aliyoyatenda mfalme Ahazia, yote yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Israeli.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania