The chat will start when you send the first message.
1Katika mwaka wa saba wa enzi ya mfalme Yehu wa Israeli Yoashi alianza kutawala Yuda huko Yerusalemu, naye akatawala kwa muda wa miaka arubaini huko Yerusalemu. Mama yake alikuwa Sibia, kutoka Beer-sheba.[#12:1 Huyu alikuwa mfalme wa saba wa Yuda. Alitawala kuanzia 835 mpaka 796 K.K.]
2Wakati wa maisha yake yote alitenda mema mbele ya Mwenyezi-Mungu, kwa sababu kuhani Yehoyada alikuwa akimfundisha.[#12:2 Kufundisha juu ya sheria ya Mwenyezi-Mungu ilikuwa ni moja ya majukumu muhimu ya makuhani (Kumb 31:9-13; Yer 18:18; Eze 7:26).]
3Hata hivyo, mahali pa juu pa kuabudia miungu hapakuharibiwa, na watu waliendelea kutambika na kufukiza ubani huko.
4Yoashi akaita makuhani na kuwaamuru, akisema, “Fedha yote inayoletwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu ikiwa imetokana na uuzaji wa vitu vitakatifu, fedha ya kila mtu kadiri alivyoandikiwa, na fedha ambayo mtu huvutwa kuitoa kwa hiari katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu,[#12:4 Kila mwanamume kuanzia umri wa miaka ishirini na kuendelea alitakiwa kulipa kodi kwa ajili ya kazi za makuhani. Taz Kut 30:11-16; Lawi 22:17-23.]
5makuhani wazipokee kutoka kwa kila mtu; nao warekebishe nyumba popote panapohitajika marekebisho.”
6Lakini hata baada ya miaka ishirini na mitatu ya mfalme Yoashi makuhani walikuwa bado hawajafanya marekebisho yoyote ya nyumba.
7Kwa hiyo mfalme Yoashi alimwita kuhani Yehoyada na makuhani wengine na kuwauliza, “Mbona hamrekebishi nyumba? Basi, msichukue fedha kutoka kwa watu mnaowatumikia, bali mtazileta, ili nyumba irekebishwe.”
8Makuhani wakakubali wasipokee fedha tena kutoka kwa watu na pia wakaahidi kutofanya marekebisho ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu.
9Yehoyada akachukua sanduku na kutoboa tundu kwenye kifuniko chake, kisha akaliweka kwenye madhabahu upande wa kulia, mtu anapoingia katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Nao makuhani waliokuwa katika zamu langoni waliweka fedha zote zilizoletwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu.
10Kila walipoona kuwa mna fedha nyingi sandukuni, katibu wa mfalme na kuhani mkuu waliingia na kuhesabu na kuzifunga katika vifurushi fedha zote zilizopatikana katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu.
11Kisha baada ya kuzipima waliwapa wafanyakazi waliosimamia nyumba ya Mwenyezi-Mungu, nao wakawalipa maseremala na wajenzi, waliorekebisha nyumba ya Mwenyezi-Mungu;
12pia waashi na wakata-mawe, zikatumiwa kununulia mbao na mawe yaliyochongwa ili kufanyia marekebisho nyumba ya Mwenyezi-Mungu na kutimiza mahitaji mengine yote ya marekebisho ya nyumba.
13Lakini pesa hizo hazikutumiwa kwa kulipia utengenezaji wa mabirika ya fedha, mikasi ya kukatia tambi za mishumaa, mabakuli, tarumbeta, wala kwa vyombo vingine vyovyote vya dhahabu au vya fedha.
14Zote zilitumiwa kwa kuwalipa wafanyakazi waliozitumia kufanya marekebisho ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu.
15Wafanyakazi waliosimamia kazi hii walikuwa waaminifu kabisa, kwa hiyo hapakuwa na haja ya kuwataka watoe hesabu ya matumizi ya fedha hizo.
16Fedha zilizotolewa kuwa sadaka za hatia na sadaka za kuondoa dhambi hazikuingizwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu; hizo zilikuwa ni mali ya makuhani.[#12:16 Fedha hizo zilikuwa mapato ya makuhani na hazikutumiwa kufanya marekebisho ya hekalu.]
17Wakati huo Hazaeli mfalme wa Aramu akaushambulia mji wa Gathi na kuuteka. Lakini Hazaeli alipoelekea Yerusalemu ili aushambulie,[#12:17 Huu ulikuwa mji wa Wafilisti kwenye tambarare ya pwani ya Mediteranea Kusini mwa Palestina (taz 1Sam 6:17). Mfalme Hazaeli alitaka pia kuushambulia mji wa Yerusalemu lakini mfalme Yoashi alimzuia kwa kulipa kiasi kikubwa cha kodi (aya 18).]
18Yoashi mfalme wa Yuda alichukua sadaka zote zilizowekwa wakfu na babu zake wafalme wa Yuda: Yehoshafati, Yehoramu na Ahazia, na kuongeza zile zake, pamoja na dhahabu yote iliyokuwa katika hazina ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu na katika ikulu, akazituma kwa Hazaeli mfalme wa Aramu. Naye Hazaeli akatoka Yerusalemu.
19Matendo mengine yote ya mfalme Yoashi yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Yuda.
20Maofisa wake walikula njama dhidi yake, wakamuulia katika nyumba ya Milo kwenye barabara inayoelekea Sila.[#12:20-21 Mfalme Yoashi ambaye aliponea chupuchupu yale mauaji ya malkia Athalia (2Fal 11:1-3) baadaye aliuawa na watumishi wake mwenyewe. Sababu za kuuawa kwake hazikutolewa.]
21Waliomuua ni Yozakari mwana wa Shimeathi na Yehozabadi mwana wa Shomeri watumishi wake. Halafu walimzika katika makaburi ya kifalme katika mji wa Daudi; naye Amazia, mwanawe, akatawala mahali pake.