The chat will start when you send the first message.
1Katika mwaka wa pili wa enzi ya Yehoashi mwana wa Yehoahazi huko Israeli, Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda alianza kutawala.[#14:1 Amazia alikuwa mfalme wa nane wa Yuda, mwaka 796-766 K.K. Wakati huo wa utawala wake, mwanawe aitwaye Azaria alitawala pamoja naye. Amazia alikuwa mmoja wa wafalme wachache sana ambao inasemekana kuwa walitenda mema ingawaje kwa kiasi fulani, maana hata yeye aliabudu miungu ya Waedomu (2Nya 25:14-16).]
2Alipoanza kutawala alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano, naye alitawala katika Yerusalemu kwa muda wa miaka ishirini na tisa. Mama yake aliitwa Yehoadani wa Yerusalemu.
3Alitenda yaliyo mema mbele ya Mwenyezi-Mungu, lakini hakuwa kama babu yake Daudi. Bali alifanya mambo yote kama Yoashi baba yake;
4isipokuwa mahali pa ibada milimani hapakuharibiwa na watu waliendelea kutambika na kufukiza ubani mahali hapo.[#14:4 Sheria ya Mungu iliagiza mahali pote pa ibada na kutambikia miungu ya kigeni milimani paharibiwe (Hes 33:52; Kumb 7:5; 12:3).]
5Mara tu Amazia alipojiimarisha mamlakani, aliwaua watumishi waliomuua mfalme, baba yake.
6Lakini hakuwaua watoto wa wauaji; kama ilivyoandikwa katika Kitabu cha Sheria za Mose, Mwenyezi-Mungu anapotoa amri akisema, “Wazazi hawatauawa kwa ajili ya watoto wao, wala watoto hawatauawa kwa ajili ya wazazi wao; bali kila mtu atauawa kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe.”[#14:6 Sheria inayonukuliwa hapa kuhusu kuwajibika wazazi kwa makosa ya watoto wao au watoto kwa makosa ya wazazi wao karibu ni sawa kabisa na Kumb 24:16. Taz Yer 31:29-30 maelezo, na Eze 18:1-32 maelezo.]
7Amazia aliwaua Waedomu 10,000 katika Bonde la Chumvi; aliutwaa kwa nguvu mji wa Sela na kuuita Yoktheeli, na hivi ndivyo unavyoitwa mpaka sasa.[#14:7 “Bonde la Chumvi” lilikuwa eneo kusini na mashariki ya Bahari ya Chumvi.]
8Kisha Amazia akatuma wajumbe kwa Yehoashi mwana wa Yehoahazi, mwana wa Yehu mfalme wa Israeli akisema, “Njoo tupambane.”
9Lakini Yehoashi mfalme wa Israeli alimpelekea ujumbe Amazia mfalme wa Israeli, akisema, “Siku moja mbaruti wa Lebanoni uliuambia mwerezi, wa huko Lebanoni pia, ‘Mwoze binti yako kwa mwanangu.’ Lakini mnyama wa mwituni akapita hapo na kuukanyagakanyaga mbaruti huo.
10Sasa wewe Amazia umewashinda kabisa Waedomu, na moyo wako unakufanya ujivune. Ridhika na utukufu wako, ukakae nyumbani; ya nini kujitafutia taabu zitakazokuangamiza wewe mwenyewe pamoja na watu wako wa Yuda?”[#14:8-10: Yehoashi, mfalme wa Israeli, anajibu wito wa mapambano na mfalme wa Yuda kwa kitendawili ambacho kinafanana na kile cha Yothamu katika Amu 9:8-15. “Mbaruti” ni mti ambao, kama mti, haufai kitu; lakini “mwerezi” (mkangazi) ni mti maarufu sana kwa uzuri wake na kwa mbao zake za harufu nzuri.]
11Lakini Amazia hakujali. Kwa hiyo Yehoashi mfalme wa Israeli alitoka akakabiliana uso kwa uso na Amazia huko vitani Beth-shemeshi, nchini Yuda.[#14:11 Huo ulikuwa mji magharibi ya mji wa Yerusalemu.]
12Watu wa Yuda walishindwa na watu wa Israeli na kila mmoja alirudi kwake.
13Yehoashi mfalme wa Israeli alimteka Amazia mfalme wa Yuda, mwana wa Yehoashi, mwana wa Ahazia huko Beth-shemeshi; halafu akauendea Yerusalemu na kuubomoa ukuta wake kutoka Lango la Efraimu mpaka Lango la Pembeni, umbali wa karibu mita 200.
14Alichukua dhahabu yote na fedha, hata na vifaa vyote vilivyokuwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu na katika hazina ya ikulu; pia alichukua mateka, kisha akarudi Samaria.
15Matendo mengine yote ya Yehoashi, ushujaa wake na vita alivyopigana na mfalme Amazia wa Yuda yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Israeli.
16Yehoashi alifariki, akazikwa katika makaburi ya kifalme huko Samaria. Mwanae, Yeroboamu akatawala mahali pake.
17Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda aliishi miaka kumi na mitano baada ya mfalme Yehoashi wa Israeli kufariki.
18Matendo mengine yote ya Amazia yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Yuda.
19Njama za kumwua Amazia zilifanywa Yerusalemu, kwa hiyo alikimbilia Lakishi, lakini maadui walituma watu wa kumwua huko.[#14:19 Mji huu ulikuwa mji mkubwa kuliko yote katika Yuda baada ya Yerusalemu.]
20Maiti yake ililetwa juu ya farasi na kuzikwa katika makaburi ya kifalme katika Yerusalemu katika mji wa Daudi.
21Kisha watu wote wa Yuda wakamchukua Azaria akiwa na umri wa miaka kumi na sita, wakamtawaza mahali pa Amazia baba yake.[#14:21 Alikuwa mfalme wa tisa wa Yuda. Nabii Isaya aliitwa kuwa nabii mwaka ule alipokufa mfalme huyu (Isa 6:1). Azaria anaitwa pia “Uzia”. Alitawala mwaka 779-740 K.K. Wakati wake ulikuwa wa utulivu na fanaka kiasi fulani, hata kwa ufalme wa kaskazini.]
22Azaria, baada ya kifo cha baba yake, aliujenga upya mji wa Elathi na kuurudisha kwa Yuda.
23Katika mwaka wa kumi na tano wa enzi ya Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda, Yeroboamu mwana wa Yehoashi mfalme wa Israeli alianza kutawala huko Samaria, akatawala kwa muda wa miaka arubaini na mmoja.[#14:23 Huyu ni Yeroboamu wa pili. Anaitwa wa pili kutofautisha na yule Yeroboamu aliyetawala ufalme wa Kaskazini mara baada ya kufa kwa mfalme Solomoni (rejea 1Fal 11:26-40; 12:1—14:20). Wakati wa mfalme Yeroboamu huyu wa pili ndipo huduma za manabii wakubwa zilipoanza. Nabii Amosi, k.m. alitangaza ujumbe wake kwa utawala wa kaskazini wa Israeli wakati wa Yeroboamu wa pili (Amo 1:1). Kasisi mmoja aitwaye Amazia akamshtaki Amosi kwa mfalme Yeroboamu wa pili akisema kwamba Amosi alikuwa msaliti (Amo 7:10-17).]
24Alimwasi Mwenyezi-Mungu akafuata mfano wa mtangulizi wake mfalme Yeroboamu mwana wa Nebati, aliyewapotosha watu wa Israeli wakatenda dhambi.
25Aliikomboa nchi yote iliyokuwa mali ya Israeli, kutoka Pito la Hamathi mpaka Bahari ya Araba. Hivi ndivyo alivyoahidi Mwenyezi-Mungu kwa njia ya mtumishi wake Yona mwana wa Amitai, nabii, kutoka Gath-heferi.[#14:25 Huyu “Yona” huenda ni nabii Yona (Yona 1:1) au Yona mwingine.]
26Maana Mwenyezi-Mungu aliona taabu kubwa kwa waliyopata Waisraeli kwani hapakuwa na mtu yeyote wa kuwasaidia.
27Lakini Mwenyezi-Mungu hakuwa amesema ya kwamba ataangamiza Israeli kabisa, hivyo aliwaokoa kwa njia ya mfalme Yeroboamu mwana wa Yehoashi.
28Matendo mengine yote ya Yeroboamu, vita alivyopigana kwa ushujaa, na jinsi alivyoikomboa Damasko na Hamathi na kuifanya mali ya Israeli, yote yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Israeli.
29Yeroboamu alifariki na kuzikwa katika makaburi ya kifalme na mwanawe Zekaria akatawala mahali pake.