The chat will start when you send the first message.
1Siku moja, Daudi aliuliza, “Je, kuna mtu yeyote aliyesalia katika jamaa ya Shauli? Kama yuko, ningependa kumtendea wema kwa ajili ya Yonathani.”[#9:1 Daudi anachukua hatua ya kutimiza ahadi yake kwa Yonathani katika 1Sam 20:14-17.]
2Kulikuwa na mtumishi wa jamaa ya Shauli aliyeitwa Siba. Siba aliitwa kwenda kwa Daudi. Mfalme Daudi alimwuliza, “Je wewe ndiye Siba?” Naye akamjibu, “Naam, mimi mtumishi wako ndiye.”
3Mfalme akamwuliza, “Je, hakuna mtu yeyote aliyesalia katika jamaa ya Shauli? Kama yuko, ningependa kumtendea wema wa Mungu.” Siba akamjibu, “Yuko mwana wa Yonathani, lakini yeye amelemaa miguu.”
4Mfalme akamwuliza, “Yuko wapi?” Siba akamjibu, “Yuko nyumbani kwa Makiri mwana wa Amieli huko Lo-debari.”[#9:4 Mji huu ulikuwa katika Gileadi, mashariki ya Mto Yordani, kwenye eneo lililomilikiwa na kabila la Manase.]
5Basi, mfalme Daudi akatuma watu, naye akaletwa kutoka nyumbani kwa Makiri mwana wa Amieli huko Lo-debari.
6Basi, Mefiboshethi mwana wa Yonathani, na mjukuu wa Shauli akaenda kwa mfalme Daudi, akaanguka kifudifudi mbele ya mfalme Daudi, akasujudu. Daudi akamwita, “Mefiboshethi.” Naye akamjibu, “Naam! Mimi hapa mtumishi wako.”[#9:6 Taz maelezo ya 4:4.]
7Daudi akamwambia, “Usiogope. Mimi nitakutendea wema kwa ajili ya baba yako Yonathani. Ile ardhi yote iliyokuwa ya babu yako Shauli nitakurudishia. Nawe, daima utakula mezani pangu.”[#9:7 Daudi anampa heshima Mefiboshethi. Huenda pia alifanya hivyo ili Mefiboshethi awe mwaminifu kwake.]
8Mefiboshethi akasujudu, na kusema, “Mimi ni sawa na mbwa mfu; kwa nini unishughulikie hivyo?”[#9:8 Taz 3:8 maelezo. Hapa Mefiboshethi alitaka bila shaka kunyenyekea mbele ya Daudi kwa hofu kwamba Daudi alikuwa na nia ya kuuangamiza kabisa ukoo wa Shauli (taz 21:8-9 jinsi walivyotendewa jamaa zake yaani watoto wa Shauli).]
9Kisha, mfalme Daudi akamwita Siba mtumishi wa Shauli, akamwambia, “Ile mali yote iliyokuwa ya Shauli na jamaa yake nimempa mjukuu wa bwana wako.
10Wewe, watoto wako na watumishi wako mtakuwa mnamlimia Mefiboshethi na mtamletea mavuno ili mjukuu wa bwana wako awe daima na chakula. Lakini yeye atakula mezani pangu.” Wakati huo, Siba alikuwa na watoto wa kiume kumi na watano na watumishi ishirini.
11Kisha, Siba akamwambia mfalme, “Mimi mtumishi wako, nitafanya yote kulingana na amri yako.” Basi, Mefiboshethi akawa anapata chakula chake mezani pa Daudi, kama mmojawapo wa watoto wa mfalme.
12Mefiboshethi alikuwa na mtoto mdogo wa kiume aliyeitwa Mika. Watu wote wa jamaa ya Siba wakawa watumishi wa Mefiboshethi.
13Hivyo, Mefiboshethi aliyekuwa amelemaa miguu yake yote akawa anaishi mjini Yerusalemu, na kupata chakula chake mezani pa mfalme daima.