The chat will start when you send the first message.
1Mimi Paulo, Silwano na Timotheo, kwa jumuiya ya kanisa la Thesalonike, ambayo ni watu wake Mungu Baba yetu na wa Bwana Yesu Kristo.
2Tunawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo.[#1:2 Kama kawaida ya barua nyakati hizo, hii Barua kwa Wathesalonike inaanza kwa kumtambulisha mwandishi, na pia kwa namna inayofanana na 1Thes Silwano (Sila) na Timotheo wanatajwa. Taz 1Thes 1:1 maelezo.]
3Ndugu, tunapaswa kumshukuru Mungu daima kwa ajili yenu. Inafaa kwetu kufanya hivyo kwani imani yenu inakua sana na kupendana kwenu kunaongezeka sana.
4Ndio maana sisi tunajivunia nyinyi katika makanisa ya Mungu. Tunaona fahari juu ya jinsi mnavyoendelea kuamini na kustahimili katika udhalimu wote na mateso mnayopata.[#1:4 Rejea 1Thes 1:6; 2:14; 3:3 (ambapo panatajwa wazi lazima ya mateso).]
5Hayo yote yanathibitisha kwamba hukumu ya Mungu ni ya haki, na matokeo yake, nyinyi mtastahili ufalme wake ambao kwa ajili yake mnateseka.
6Mungu atafanya jambo la haki: atawalipa mateso wale wanaowatesa nyinyi
7na kuwapeni nafuu nyinyi mnaoteseka, na sisi pia. Atafanya jambo hilo wakati Bwana atakapotokea kutoka mbinguni pamoja na malaika wake wenye nguvu[#1:7 Mat 25:31; Marko 8:38; taz 1Thes 3:11-13 maelezo.]
8na miali ya moto, kuwaadhibu wale wanaomkataa Mungu na wale wasiotii Habari Njema ya Bwana wetu Yesu.[#1:8 Katika A.K. picha au mfano wa moto ulitumiwa mara kwa mara kuandamana na kutokea au kuweko kwake Mungu (Kut 19:18; 24:17; Kumb 4:11-13; Eze 1:4; 8:2); katika mazingira mengine, picha ya moto inahusikana na hukumu, na hiyo ndiyo inayohusika hapa (aya 8-9). Rejea Isa 66:15; Mat 25:41; 1Kor 3:13-15.]
9Adhabu yao itakuwa kuangamizwa milele na kutengwa mbali na utukufu wake mkuu,
10wakati atakapokuja siku ile kupokea utukufu kutoka kwa watu wake na heshima kutoka kwa wote wanaoamini. Nyinyi pia mtakuwa miongoni mwao, kwani mmeuamini ule ujumbe tuliowaletea.
11Ndiyo maana tunawaombeeni daima. Tunamwomba Mungu wetu awawezesheni kustahili maisha aliyowaitia muyaishi. Tunamwomba, kwa uwezo wake, atimize nia yenu ya kutenda mema na kukamilisha kazi yenu ya imani.
12Kwa namna hiyo, jina la Bwana wetu Yesu litapata utukufu kutoka kwenu, nanyi mtapata utukufu kutoka kwake kwa neema ya Mungu wetu na ya Bwana Yesu Kristo.