Matendo 11

Matendo 11

Taarifa ya Petro kwa kanisa la Yerusalemu

1Mitume na ndugu kule Yudea walisikia kwamba watu wa mataifa mengine pia walikuwa wamelipokea neno la Mungu.

2Basi, Petro aliporudi Yerusalemu, wale Wayahudi waumini waliopendelea watu wa mataifa mengine watahiriwe, walimlaumu wakisema:[#11:2 Neno kwa neno: Yaani, awali ya yote, ni Wayahudi lakini vilevile yamkini walisisitiza umuhimu wa kutahiriwa hata kwa watu wa mataifa mengine kama vile katika Gal 2:12 ambapo pia panataja Wakristo Wayahudi lakini ambao walisisitiza kutahiriwa kwa waumini wasio Wayahudi.]

3“Wewe umekwenda kukaa na watu wasiotahiriwa na hata umekula pamoja nao![#11:3 Kuingia nyumbani kwa mtu asiye Myahudi kulikatazwa kwa Wayahudi (taz maelezo ya Mate 10:28); tena kula na watu wasio Wayahudi ilikuwa jambo baya zaidi.]

4Hapo Petro akawaeleza kinaganaga juu ya yale yaliyotendeka tangu mwanzo:

5“Siku moja nikiwa nasali mjini Yopa, niliona maono; niliona kitu kama shuka kubwa ikishushwa chini kutoka mbinguni ikiwa imeshikwa pembe zake nne, ikawekwa kando yangu.

6Nilichungulia ndani kwa makini nikaona wanyama wenye miguu minne, wanyama wa mwituni, wanyama watambaao na ndege wa angani.

7Kisha nikasikia sauti ikiniambia: ‘Petro amka, chinja, ule.’

8Lakini mimi nikasema: ‘La, Bwana; maana chochote kilicho najisi au kichafu hakijapata kamwe kuingia kinywani mwangu.’

9Ile sauti ikasikika tena kutoka mbinguni: ‘Usiviite najisi vitu ambavyo Mungu amevitakasa.’

10Jambo hilo lilifanyika mara tatu, na mwishowe vyote vilirudishwa juu mbinguni.

11Ghafla, watu watatu waliokuwa wametumwa kwangu kutoka Kaisarea waliwasili kwenye nyumba nilimokuwa nakaa.

12Roho aliniambia niende pamoja nao bila kusita. Hawa ndugu sita waliandamana nami pia kwenda Kaisarea na huko tuliingia nyumbani mwa Kornelio.[#11:12 Au: bila kubagua: (Neno lilelile la Kigiriki latumiwa pia katika Mate 15:9). taz Mate 10:23,45.]

13Yeye alitueleza jinsi alivyokuwa amemwona malaika amesimama nyumbani mwake na kumwambia: ‘Mtume mtu Yopa akamwite mtu mmoja aitwaye Simoni, kwa jina lingine Petro.[#11:13 Hii ni mara ya nne tukio hilo linatajwa (taz 10:3,5,32) na hivyo kudhihirisha umuhimu wake.]

14Yeye atakuambia maneno ambayo kwayo wewe na jamaa yako yote mtaokolewa.’[#11:14 Kwa maana ya wote walioishi nyumbani kwake (taz 10:7).]

15Na nilipoanza tu kuongea, Roho Mtakatifu aliwashukia kama alivyotushukia sisi pale awali.[#11:15 Yaani wakati wa Pentekoste.]

16Hapo nilikumbuka yale maneno Bwana aliyosema: ‘Yohane alibatiza kwa maji, lakini nyinyi mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu.’

17Basi, kama Mungu amewapa pia watu wa mataifa mengine kipawa kilekile alichotupa sisi tulipomwamini Bwana Yesu Kristo, je, mimi ni nani hata nijaribu kumpinga Mungu?”

18Waliposikia hayo, waliacha ubishi, wakamtukuza Mungu wakisema, “Mungu amewapa watu wa mataifa mengine nafasi ya kutubu wapate uhai!”[#11:18 Petro anatoa sababu ya kumpokea mtu asiye Myahudi katika Ukristo. Kadiri ya Luka Petro alikuwa wa kwanza kufanya hivyo licha ya tukio la Antiokia ambalo Luka ataligusia baadaye na pia licha ya lile tukio la towashi Mwethiopia 8:26-39 ambapo Filipo anahusika.]

Kanisa la Antiokia

19Kutokana na mateso yaliyotokea wakati Stefano alipouawa, waumini walitawanyika. Wengine walikwenda mpaka Foinike, Kupro na Antiokia wakihubiri ule ujumbe kwa Wayahudi tu.[#11:19 Huu ulikuwa mji mkuu wa mkoa wa utawala wa Roma huko Siria na kwa umaarufu wake ulikuwa mji wa tatu wa dola la Waroma (si sawa na Antiokia nyingine huko Pisidia). Kufika eneo hilo ilikuwa kufika ndani kabisa ya eneo la watu wasio Wayahudi (Mate 1:8) ingawaje huko nako kulikuwa na Wayahudi wengi.]

20Lakini baadhi ya waumini waliotoka Kupro na Kurene, walikwenda Antiokia wakautangaza huo ujumbe kwa watu wa mataifa mengine wakiwahubiria Habari Njema juu ya Bwana Yesu.

21Bwana aliwasaidia na idadi kubwa ya watu iliamini na kumgeukia Bwana.

22Habari ya jambo hilo ikasikika kwa lile kanisa la Yerusalemu. Hivyo wakamtuma Barnaba aende Antiokia.[#11:22 Alikuwa mwenyeji wa Kupro (Mate 4:36); kadiri ya aya 2, baadhi ya waumini kutoka kisiwa hiki walikuwa wamewasili Antiokia kuhubiri Injili.]

23Alipofika huko na kuona jinsi Mungu alivyowaneemesha wale watu, alifurahi na kuwahimiza wote wadumu katika uaminifu wao kwa Bwana.[#11:23 Kuwafariji; au: . Ling Mate 4:36, ambapo Barnaba anaitwa]

24Barnaba alikuwa mtu mwema na mwenye kujaa Roho Mtakatifu na imani. Kundi kubwa la watu lilivutwa kwa Bwana.

25Kisha, Barnaba alikwenda Tarso kumtafuta Saulo.[#11:25 Mahali alipozaliwa Paulo (Mate 21:39; 22:3); huo ulikuwa mji mkuu wa mkoa wa Kilikia na Asia Ndogo.; #11:25 Tangu hapo habari za Paulo zinaendelea baada ya karibu miaka kumi (taz Gal 1:10—2:12).]

26Alipompata, alimleta Antiokia. Nao wote wawili walikaa na ile jumuiya ya kanisa kwa mwaka wote mzima wakifundisha kundi kubwa la watu. Huko Antiokia, ndiko kwa mara ya kwanza, wafuasi waliitwa Wakristo.[#11:26 Neno ambalo katika Kigiriki linatajwa hapa, katika Mate 26:28 na 1Pet 4:16. Neno hilo lilitumiwa kuwataja waumini.]

27Wakati huohuo, manabii kadhaa walikuja Antiokia kutoka Yerusalemu.[#11:27 Kuhusu Wakristo: taz 1Kor 14:1 (maelezo) na pia Mate 13:1; 15:32; 1Kor 12:28; Efe 2:22; 3:5; 4:11; Ufu 22:9.]

28Basi, mmoja wao aitwaye Agabo alisimama, na kwa uwezo wa Roho akabashiri kwamba kutakuwa na njaa kubwa katika nchi yote. (Njaa hiyo ilitokea wakati wa utawala wa Klaudio).[#11:28 (Ling Mate 18:2). Huyo alikuwa mfalme mkuu wa Waroma tangu mwaka 41 B.K. mpaka 54 B.K. Mnamo wakati huo kulizuka njaa kubwa, mojawapo ikiwa ile njaa ya mwaka 46 B.K. ambayo iliathiri sana nchi ya Yudea. Mwanahistoria Yosefu Flavio anagusia njaa hiyo.]

29Wale wanafunzi waliamua kila mmoja kwa kadiri ya uwezo wake apeleke chochote ili kuwasaidia wale ndugu waliokuwa wanaishi Yudea.

30Basi, wakafanya hivyo na kuwapa Barnaba na Saulo mchango huo wauwasilishe wao wenyewe kwa wazee wa kanisa.[#11:30 Katika kitabu cha Matendo neno hilo latumika kuwataja hasa wale waliokuwa na mamlaka au madaraka katika kanisa. (Taz pia Gal 2:1-10 na maelezo ya Mate 15:1-21). Hatujui kwa nini hapa mwandishi hakuwataja mitume. Yaonekana kwamba hao wazee waliteuliwa na kupewa wadhifa wao na mitume (Mate 14:23) na majukumu yao yanatajwa katika Mate 20:28.]

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania