Matendo 16

Matendo 16

Timotheo anajiunga na Paulo na Sila

1Paulo alifika Derbe na Lustra, ambako aliishi mfuasi mmoja aitwaye Timotheo. Mama yake ambaye pia alikuwa mfuasi, alikuwa Myahudi; lakini baba yake alikuwa Mgiriki.[#16:1 Sehemu alizotembelea Paulo wakati wa safari yake ya kwanza pamoja na Barnaba (taz 14:6-23).; #16:1 Mwenzake Paulo katika ziara zake nyingi (Rom 16:21; 1Kor 4:17; 16:10-11; Fil 2:19-24; 1Thes 3:2-6), na anaonekana kuhusika kwa namna nyingi na barua za Paulo (Fil 1:1; Kol 1:1; 1Thes 1:1; taz pia barua mbili za kichungaji ambazo zinamtaja yeye Timotheo kama mwandikiwa). Katika 1Tim mama yake ni Euniko na nyanya yake ni Loisi.]

2Timotheo alikuwa na sifa kubwa kati ya wale ndugu wa Lustra na Ikonio.

3Paulo alitaka Timotheo aandamane naye safarini, kwa hiyo alimtahiri. Alifanya hivyo kwa sababu Wayahudi wote walioishi sehemu hizo walijua kwamba baba yake Timotheo alikuwa Mgiriki.[#16:3 Kulingana na desturi za Kiyahudi, Timotheo alichukuliwa kama Mwisraeli kwa kuwa mwana wa mama Myahudi (ling na 16:1; 2Tim 1:5), lakini kwa sababu fulani hakuwa ametahiriwa.]

4Walipokuwa wanapita katika ile miji waliwapa watu yale maagizo yaliyotolewa na mitume na wazee kule Yerusalemu, wakawaambia wayazingatie.

5Hivyo, yale makanisa yalizidi kuwa imara katika imani, na idadi ya waumini ikaongezeka kila siku.

Paulo anaona maono kule Troa

6Walipitia sehemu za Frugia na Galatia kwani Roho Mtakatifu hakuwaruhusu kuhubiri huo ujumbe mkoani Asia.

7Walipofika kwenye mipaka ya Musia, walijaribu kuingia mkoani Bithunia, lakini Roho wa Yesu hakuwaruhusu.[#16:7 Kifungu cha maneno ambacho katika A.J. chapatikana hapa tu. Baadhi ya hati za mkono hazina Taz Rom 8:9. Labda hapa hamna tofauti ya kitheolojia na yale maneno ya kawaida yaani Roho Mtakatifu au Roho wa Mungu.]

8Basi, walipitia Musia, wakaenda moja kwa moja mpaka Troa.[#16:8-9 Bandari katika bahari ya Aegea na mahali pa kuanzia safari kwenda mkoa wa Kiroma uliopakana upande wa kaskazini na Ugiriki.]

9Usiku huo, Paulo aliona maono ambayo alimwona mtu mmoja wa Makedonia amesimama pale na kumwomba: “Vuka, uje Makedonia ukatusaidie.”

10Mara baada ya Paulo kuona maono hayo, tulijitayarisha kwenda Makedonia bila kukawia, tukiwa na hakika kwamba Mungu ametuita tuwahubirie Habari Njema.[#16:10 Katika aya hii habari tunazoambiwa zinasimuliwa na kuhusu - kwa uchache - watu wawili (wingi): … Namna hii ya kusema inapatikana katika 16:10-17; 20:5-15; 21:1-8 na 27:1—28:16 na inaonesha kwamba mwandishi alikuwako au alihusika katika mambo na matukio yanayotajwa. Wengine wanafikiri ni namna tu ya kuandika.]

Kuongoka kwa Ludia

11Kutoka Troa, tulisafiri kwa meli moja kwa moja mpaka Samothrake, na kesho yake tukatia nanga Neapoli.[#16:11 Bandari ya bahari ya Aegea iliyotumiwa na mji wa]

12Kutoka huko, tulikwenda mpaka Filipi, mji wa wilaya ya kwanza ya Makedonia, na ambao pia ni koloni la Waroma. Tulikaa katika mji huo siku kadhaa.[#16:12 Makoloni ya Waroma yalikuwa miji fulani fulani ambayo ilipata mapendeleo au nafuu fulanifulani za pekee, kama vile kulipa kodi na ushuru.]

13Siku ya Sabato tulitoka nje ya mji, tukaenda kando ya mto ambapo tulidhani ya kuwa ni mahali pa kusali. Tuliketi, tukaongea na wanawake waliokusanyika mahali hapo.[#16:13 Yaonekana kwamba huko Filipi hakukuwa na sunagogi na wakazi Wayahudi wa huko walikutana siku ya Sabato ambapo kulikuwa na maji ya kutawadha.]

14Miongoni mwa wale waliotusikiliza alikuwa mwanamke mmoja mcha Mungu aitwaye Ludia mwenyeji wa Thuatira, ambaye alikuwa mfanyabiashara ya nguo za kitani za rangi ya zambarau. Bwana aliufungua moyo wake hata akayapokea yale maneno Paulo aliyokuwa anasema.[#16:14 Yamkini Ludia hakuwa Myahudi lakini alishiriki ibada ya Wayahudi (Mate 10:2).; #16:14 Mji wa mkoa wa Asia maarufu kwa nguo za kitani rangi zambarau. Kwa vile ulikuwa mji wa biashara kubwa yaonekana kwamba Ludia alikuwa mwanamke wa tabaka la juu.]

15Baada ya huyo mama pamoja na jamaa yake kubatizwa, alitualika akisema, “Kama kweli mmeona kwamba mimi namwamini Bwana, karibuni nyumbani kwangu mkakae.” Akatuhimiza twende.[#16:15 Yaani watu walioishi nyumbani kwake kama vile watumishi, wafanyakazi n.k. Labda Ludia hakuwa ameolewa au alikuwa mjane.]

Paulo na Sila wanatiwa nguvuni

16Siku moja, tulipokuwa tunakwenda mahali pa kusali, msichana mmoja aliyekuwa na pepo mwenye uwezo wa kuagua alikutana nasi. Msichana huyo alikuwa anawapatia matajiri wake fedha nyingi kwa uaguzi wake.[#16:16 Neno kwa neno: kukumbuka nyoka (chatu) ambaye alikuwa mlinzi wa mahali pa uaguzi pa Delfi huko Ugiriki.]

17Basi, huyo msichana alimfuata Paulo na sisi, akipiga kelele na kusema, “Hawa watu ni watumishi wa Mungu Mkuu. Wanawatangazieni njia ya wokovu.”

18Akawa anafanya hivyo kwa siku nyingi hata siku moja Paulo alikasirika, akamgeukia na kumwambia huyo pepo, “Nakuamuru kwa jina la Yesu Kristo, mtoke huyu!” Mara huyo pepo akamtoka.

19Matajiri wa yule msichana walipoona kwamba tumaini lao la kupata mali limekwisha, waliwakamata Paulo na Sila, wakawaburuta mpaka hadharani, mbele ya wakuu.[#16:19 Neno kwa neno: ambapo katika miji ya Wagiriki kulikuwa ni mahali ambapo matatizo ya raia yalitatuliwa na uamuzi kufanywa. Katika miji mikubwa kama Athene mahali hapo palikuwa na ukumbi wa mazungumzo ya wasomi.]

20Wakawashtaki kwa mahakimu wakisema, “Watu hawa ni Wayahudi na wanafanya fujo katika mji wetu.

21Wanafundisha desturi ambazo sisi raia wa Roma haturuhusiwi kuzikubali wala kuzifuata.”

22Kundi la watu likajiunga likawashambulia; na wale mahakimu wakawavua nguo zao kwa nguvu, wakaamuru wapigwe viboko.

23Baada ya kupigwa sana wakatiwa ndani, na askari wa gereza akaamriwa kuwaweka chini ya ulinzi mkali.

24Kutokana na maagizo hayo, huyo askari aliwaweka katika chumba cha ndani kabisa cha gereza na kuifunga miguu yao kwenye nguzo.

25Karibu na usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa wakisali na kuimba nyimbo za kumsifu Mungu, huku wafungwa wengine wakiwa wanasikiliza.

26Ghafla, kulitokea mtetemeko mkuu wa ardhi ambao uliitikisa misingi ya gereza. Mara, milango yote ikafunguka na minyororo iliyowafunga hao wafungwa ikaachana.

27Askari wa gereza alipoamka na kuiona milango ya gereza imefunguliwa, alidhani kwamba wafungwa wote walikuwa wametoroka, na hivyo akauchomoa upanga wake, akataka kujiua.[#16:27 Kitendo ambacho chaeleweka kwa vile kwa taratibu za nyakati hizo askari mlinzi aliyemwachia mfungwa kutoroka alipata adhabu ya huyo mfungwa (taz 12:19b na 27:42).]

28Lakini Paulo akaita kwa sauti kubwa: “Usijidhuru mwenyewe kwa maana sisi sote tuko hapa.”

29Baada ya kumwita mtu alete taa, huyo askari wa gereza alikimbilia ndani, akajitupa mbele ya miguu ya Paulo na Sila huku akitetemeka kwa hofu.

30Halafu aliwaongoza nje, akawauliza, “Waheshimiwa, nifanye nini nipate kuokoka?”

31Wao wakamjibu, “Mwamini Bwana Yesu nawe utaokolewa pamoja na jamaa yako yote.”

32Basi, wakamhubiria neno la Bwana yeye pamoja na jamaa yake.

33Yule askari aliwachukua saa ileile ya usiku akawasafisha majeraha yao, kisha yeye na jamaa yake wakabatizwa papo hapo. [

34Halafu akawachukua Paulo na Sila nyumbani kwake, akawapa chakula. Yeye na jamaa yake yote wakafanya sherehe kwa vile sasa walikuwa wanamwamini Mungu].

35Kesho yake asubuhi, mahakimu waliwatuma maofisa wao wakisema, “Wafungueni wale watu.”

36Yule askari wa gereza alimpasha habari Paulo: “Mahakimu wametuma ujumbe ili mfunguliwe. Sasa mnaweza kutoka na kwenda zenu kwa amani.”

37Lakini Paulo alimjibu, “Ati nini? Ingawa hatukuwa na kosa, walitupiga viboko hadharani hali sisi ni raia wa Roma. Tena, walitutia ndani na sasa wanataka kutufungulia kwa siri! Hata kidogo! Ni lazima wao wenyewe waje hapa watufungulie.”[#16:37-38 Sheria ya Kiroma ilikataza kabisa kuwapiga mijeledi raia wake (taz 22:25-29).]

38Hao maofisa waliwapasha habari mahakimu juu ya jambo hilo, nao waliposikia kwamba Paulo na Sila walikuwa raia wa Roma, waliogopa.

39Hivyo, walikwenda kuwataka radhi na baada ya kuwatoa ndani waliwaomba watoke katika mji ule.

40Paulo na Sila walitoka gerezani, wakaenda nyumbani kwa Ludia. Huko walionana na ndugu waumini na baada ya kuwatia moyo wakaondoka.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania