The chat will start when you send the first message.
1Basi, Agripa akamwambia Paulo, “Unaruhusiwa kujitetea.” Hapo Paulo alinyosha mkono wake akajitetea hivi:
2“Mfalme Agripa, ninajiona mwenye bahati leo kujitetea mbele yako kuhusu yale mashtaka yote ambayo Wayahudi walikuwa wamesema juu yangu.
3Hasa kwa vile wewe mwenyewe ni mtaalamu wa desturi za Wayahudi na migogoro yao, ninakuomba basi unisikilize kwa uvumilivu.[#26:3 Taz Mate 25:13.]
4“Wayahudi wanajua habari za maisha yangu tangu utoto, jinsi nilivyoishi tangu mwanzo kati ya taifa langu huko Yerusalemu.
5Wananifahamu kwa muda mrefu, na wanaweza kushuhudia, kama wakipenda, kwamba tangu mwanzo niliishi kama mmoja wa kikundi chenye siasa kali kabisa katika dini yetu, yaani kikundi cha Mafarisayo.
6Na sasa niko hapa nihukumiwe kwa sababu ninaitumainia ile ahadi ambayo Mungu aliwaahidi babu zetu.[#26:6-8 Ling na Dan 12:2 na pia Mate 23:6; 24:15; 28:20; Paulo anahusisha tumaini la ufufuo wa wafu na kifo na ufufuo wake Kristo (aya 23; Ling 1Kor 15:12-23).]
7Ahadi hiyo ndiyo ileile inayotumainiwa na makabila kumi na mawili ya taifa letu, wakimtumikia Mungu kwa dhati mchana na usiku. Mheshimiwa mfalme, Wayahudi wananishtaki kwa sababu ya tumaini hilo!
8Kwa nini nyinyi mnaona shida sana kuamini kwamba Mungu huwafufua wafu?
9Kwa kweli mimi mwenyewe niliamini kwamba ni wajibu wangu kufanya mambo mengi kulipinga jina la Yesu wa Nazareti.[#26:9 Taz Mate 3:16.]
10Mambo hayo ndiyo niliyoyafanya huko Yerusalemu. Mimi binafsi, nikiwa nimepewa mamlaka kutoka kwa makuhani wakuu, nilipata kuwatia gerezani wengi wa watu wa Mungu. Nao walipohukumiwa kuuawa, nilipiga kura ya kukubali.[#26:10 Neno linalotumika katika Kigiriki cha A.J. ni lile ambalo kwa kawaida hutafsiriwa kwa neno “watakatifu”. Hapa lakini lina maana ya wale waumini au wafuasi wa Yesu. Wengine wanafikiri linatumiwa hapa kutilia mkazo kwamba kitendo alichofanya Paulo ni kosa; au kuonesha kwamba Wakristo, yaani wafuasi wa Yesu Kristo ni watu wa Mungu.; #26:10 Huenda Paulo alikuwa mwanachama wa halmashauri au baraza la huko Yerusalemu.]
11Mara nyingi niliwafanya waadhibiwe katika masunagogi yote nikiwashurutisha waikane imani yao. Hasira yangu kwao ilikuwa kubwa hata nikawasaka mpaka miji ya mbali.
12“Kwa mujibu huohuo, nilikwenda Damasko wakati mmoja, nikiwa na mamlaka na maagizo kutoka kwa makuhani wakuu.
13Mheshimiwa, wakati nilipokuwa njiani, saa sita mchana, niliona mwanga mkubwa kuliko wa jua ukiangaza kutoka mbinguni, ukanizunguka mimi na wale wasafiri wenzangu.
14Sisi sote tulianguka chini, nami nikasikia sauti ikiniambia kwa Kiebrania: ‘Saulo, Saulo! Kwa nini unanitesa? Unajiumiza bure kama ng'ombe anayepiga teke fimbo ya bwana wake.’[#26:14 Labda au chenyewe kwa vile lugha hiyo ilijulikana kuwa lugha ya dini (taz Mate 21:40).; #26:14 Msemo karibu wa methali wa wakati huo.]
15Mimi nikauliza: ‘Ni nani wewe Bwana?’ Naye Bwana akajibu: ‘Mimi ni Yesu ambaye wewe unamtesa.
16Haidhuru, inuka sasa; simama wima. Nimekutokea ili nikuweke rasmi kuwa mtumishi wangu. Utawathibitishia watu wengine mambo uliyoyaona leo na yale ambayo bado nitakuonesha.
17Nitakuokoa na watu wa Israeli na watu wa mataifa mengine ambao mimi ninakutuma kwao.
18Utayafumbua macho yao na kuwawezesha watoke gizani na kuingia katika mwanga; watoke katika utawala wa Shetani, wamgeukie Mungu; ili kwa kuamini, wapate kusamehewa dhambi na kuchukua nafasi yao kati ya wale ambao wamepata kuwa watu wa Mungu.’[#26:18 Ling na Isa 42:6-7,16; Kol 1:12-14. Katika Biblia giza hutumika kuhusu mahali pa maumivu na mateso (taz Zab 107:10). Katika Efe 6:12 wale wanaopingana na Mungu wanaitwa “wanaomiliki ulimwengu … wa giza”. Lakini, kwa upande mwingine, mwanga unatumiwa kuelezea juu ya Mungu au neno lake (1Yoh 1:5; Zab 119:105).]
19“Hivyo, mfalme Agripa, sikuweza kuwa mkaidi kwa maono hayo ya mbinguni.
20Ila nilianza kuhubiri kwanza kwa watu wa Damasko, halafu kwa wale wa Yerusalemu na nchi yote ya Yudea, na pia kwa watu wa mataifa mengine. Niliwahimiza wamgeukie Mungu na kuonesha kwa vitendo kwamba wamebadilisha mioyo yao.[#26:20 Mate 9:19-22,28-29.; #26:20 Ling na Mate 3:19; 9:35; 14:15; 15:19; 20:21.; #26:20 Ling na Mat 3:8; Efe 2:10; Tito 2:14; 3:8.]
21Kwa sababu hiyo, Wayahudi walinikamata nikiwa hekaluni, wakajaribu kuniua.
22Lakini Mungu alinisaidia; na hivyo mpaka siku ya leo nimesimama imara nikitoa ushuhuda kwa wote, wakubwa na wadogo. Ninayosema ni yale ambayo manabii na Mose walisema yatatukia;[#26:22 Ling na alichosema Yesu katika Luka 24:27,44; na pia Rom 1:2; 16:26; 1Kor 15:3-4.]
23yaani ilimpasa Kristo ateseke na kuwa wa kwanza kufufuka kutoka kwa wafu, ili atangaze kwamba mwanga wa ukombozi unawaangazia sasa watu wote, Wayahudi na pia watu wa mataifa mengine.”[#26:23 Taz 26:6-8; Ling na pia 1Kor 15:20; Kol 1:18.]
24Paulo alipofika hapa katika kujitetea kwake, Festo alisema kwa sauti kubwa, “Paulo! Una wazimu! Kusoma kwako kwingi kunakutia wazimu!”
25Lakini Paulo akasema, “Sina wazimu mheshimiwa Festo. Ninachosema ni ukweli mtupu.
26Wewe Mfalme unayafahamu mambo haya, kwa hiyo ninaweza kuongea bila woga mbele yako. Sina mashaka kwamba matukio hayo yanajulikana kwako maana jambo hili halikutendeka mafichoni.
27Mfalme Agripa, je, una imani na manabii? Najua kwamba unaamini.”
28Agripa akamjibu Paulo, “Kidogo tu utanifanya Mkristo!”[#26:28 Agripa lakini anatumia jina hilo kwa dharau; taz Mate 11:26. Ona vilevile kwamba, kwa suala hilo Agripa anakwepa kumjibu Paulo.]
29Paulo akamjibu, “Namwomba Mungu kwamba, kwa muda mfupi au mrefu, si wewe tu bali wote wanaonisikia leo wapate kuwa kama nilivyo mimi, lakini bila hii minyororo.”
30Hapo mfalme Agripa, mkuu wa mkoa, Bernike na wale wote waliokuwa pamoja nao, walisimama.
31Walipokwisha ondoka, waliambiana, “Mtu huyu hakufanya chochote kinachostahili adhabu ya kifo au kifungo.”
32Naye Agripa akamwambia Festo, “Mtu huyu angeweza kufunguliwa kama asingalikuwa amekata rufani kwa Kaisari.”